
Mataifa ya Ulaya yamewakamata washukiwa kadhaa wa Uislamu wa itikadi
kali jana Ijumaa wakati Ubelgiji imesema imesambaratisha,
kikundi cha "magaidi" waliokuwa wakipanga kuwauwa maafisa wa polisi.
Na Ufaransa ikifuatilia taarifa mpya kuhusiana na mashambulio ya wiki iliyopita mjini Paris. Misako hiyo imeleta hofu mpya juu ya maelfu ya vijana wa mataifa ya
Ulaya wanaoaminika kuwa wamekwenda katika mataifa ya mashariki ya kati
kupigana pamoja na kundi linalojiita Dola la Kiislamu na makundi mengine
yenye mafungamano na al-Qaeda kabla ya kurejea nyumbani na kufanya
mashambulio. Washukiwa wawili wa jihadi wamepigwa risasi na kuuwawa katika mapambano
makali ya silaha wakati wa msako dhidi ya ugaidi katika mji wa mashariki
mwa Ubelgiji wa Verviers, karibu na mpaka na Ujerumani, usiku wa
Alhamisi, wamesema waendesha mashtaka.
Washukiwa wakamatwa
Polisi imewakamata watu 13 wakati wa msako huo nchini Ubelgiji, watano
kati yao wamefunguliwa mashitaka baadaye kwa "kushiriki katika shughuli
za kundi la kigaidi", msemaji wa idara ya waendesha mashitaka Eric Van
der Sijpt ameliambia shirika la habari la AFP. Hapo kabla ameuambia mkutano na waandishi habari kuwa kundi hilo, baadhi
yao wamerejea hivi karibuni kutoka Syria, lilikuwa ukingoni mwa kufanya
mashambulizi ya kigaidi kuwauwa maafisa wa polisi mitaani na katika
vituo vya polisi.
Polisi wamepata bunduki nne chapa Kalashnikov, miripuko, risasi na vifaa
vya mawasiliano katika msako huo, pamoja na sare za polisi. Kurasa za Twitter za makundi ya jihadi baadaye zimewatambua watu hao
wawili waliouwawa kuwa ni Radwan Haqawi na Tareq Jadoun na kuchapisha
kile ilichosema ni picha zao wakiwa nchini Syria. Maafisa wa Ubelgiji
hawakuthibitisha majina yao.
Wabelgiji wengine wawili wamekamatwa nchini Ufaransa baada ya kudaiwa
walikuwa wanakimbia msako huo na walikuwa wanaelekea nchini Italia,
chanzo cha polisi kimesema. Ubelgiji imeomba watu hao warejeshwe nchini
humo. Polisi ya Ufaransa imewakamata watu 12 usiku na kuwahoji juu ya
uwezekano kwamba huenda walitoa msaada kwa washambuliaji waliokuwa na
silaha mjini Paris, ndugu wawili Said na Cherif Kouachi na Amedy
Coulibaly, chanzo cha polisi kimesema.
Nchini Ujerumani anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi la Waturuki na Warusi
linalopanga kufanya shambulio nchini Syria na mtu ambaye anahusika na
kutoa fedha za kugharamia shughuli za kigaidi wamekamatwa katika msako
dhidi ya maeneo ya washukiwa wa kundi la Waislamu wenye itikadi kali
ndani na kuzunguka mji wa Berlin ambapo zaidi ya polisi 200 walihusika,
wamesema maafisa.
Maandamano ya kupinga Charlie Hebdo
Maelfu ya watu wameandamana duniani na ghasia zimezuka nchini Niger na
Pakistan wakati Waislamu wakionesha hasira zao kuhusiana na kuchapishwa
kwa katuni mpya za Mtume Muhammad na gazeti la Charlie Hebdo. Watu wanne wameuwawa na 45 wamejeruhiwa katika mji wa pili nchini Niger
wa Zinder katika maandamano ambayo yaligeuka kuwa ya ghasia ambapo
waandamanaji waliingia na kuharibu makanisa matatu na kuchoma moto kituo
cha utamaduni cha Ufaransa.
Kiasi watu watatu wamejeruhiwa wakati waandamanaji wakipambana na polisi
nje ya ubalozi wa Ufaransa mjini Karachi, Pakistan. Miongoni mwao ni
mpiga picha wa shirika la habari la AFP, ambaye alipigwa risasi
mgongoni. Marekani imeshutumu ghasia hizo, ikisema kuna haki za msingi kwa vyombo
vya habari kuchapisha kwa uhuru aina yoyote ya taarifa , ikiwa ni pamoja
na vikatuni.
Mjini Washington , rais Barack Obama na waziri mkuu wa Uingereza David
Cameron wameapa kuisaidia Ufaransa na nchi nyingine kuushinda ugaidi
duniani kwa ushirikiano mkubwa na uchunguzi.
"Tutaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wetu kuisaidia Ufaransa
kutafuta haki inayohitajika .. kuweza kuishinda mitandao hii ya
kigaidi," Obama amesema. Hata hivyo , Obama ameongeza kwamba kuijumuisha jamii ya Waislamu
inawezekana kufanywa kwa ubora zaidi katika bara la Ulaya na kusema " ni
muhimu kwa Ulaya kutojibu kwa kutumia nyundo na sheria pamoja na jeshi
kwa matatizo haya.
Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amesema yuko tayari kuliweka
jeshi mitaani kuhakikisha usalama baada ya misako hiyo. Ameongeza
kiwango cha tahadhari ya ugaidi nchini humo kuwa katika kiwango cha juu
katika nafasi ya nne. Shule za Wayahudi mjini Brussels na mji wa bandari wa Antwerp zimefungwa
jana Ijumaa(16.01.2015). Misako hiyo inakuja chini ya mwaka mmoja baada
ya watu wanne kupigwa risasi na kuuwawa katika shambulio dhidi ya
nyumba ya makumbusho ya Wayahudi mjini Brussels.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment