
Vyama vya siasa visivyokuwa na uwakilishi bungeni
vimeitaka serikali kusitisha mikataba ya wawekezaji wa makampuni
yanayozalisha umeme nchini kutokana na baadhi kuuza nishati hiyo kwa
bei ya juu na kuliumiza Shirika la Umeme (Tanesco) na hivyo kuwaongezea
wananchi mzigo wa umeme usiobebeka.
Tamko hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na makatibu wakuu wa
vyama vya CCK, AFP, SAU, UMD, Chausta, UPDP, NRA, Jahazi na Chauma.
Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Ali Kaniki, akitoa msimamo
huo kwa niaba ya makatibu wenzake, alisema hatua ya baadhi ya
makampuni kuendelea kuiuzia Tanesco umeme kunalifanya shirika hilo
kujiendesha kwa hasara kila mwaka na kutishia uhai wake.“Serikali inataka kupitia mikataba upya ya makampuni yanayozalisha umeme nchini ili makampuni yale ambayo yanauza umeme kwa bei ya juu mikataba yao isitishwe, bila kufanya hivyo hakuna hata siku moja Tanesco itapata faida,”alisema.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tanesco makampuni ambayo hadi sasa yanendelea kuuza umeme kwa shirika hilo ni kampuni ya Independent Power (IPTL), Songas, Symbion na Aggreco, Pan Africa Energy. Kaniki alisema kulingana na takwimu za Tanesco hadi kufikia Novemba mwaka jana kampuni ya IPTL ndiyo ilikuwa ikiuza umeme kwa bei ndogo ya senti 0.23 za Dola za Marekani kwa kilowati moja kwa saa.
Alisema makampuni mengine yanauza kati ya senti 0.24 hadi 0.36 sento za Dola za Marekani kwa kilowati moja kwa saaa. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii, Renatus Muabhi, alisema kutokana na hali ya uchumi ya Watanzania kuwa mbaya na makampuni kuendelea kuuza umeme kwa bei ya juu ni dhahiri yanawakandamiza na kuwaongezea umasikini kwa kuwa wanategemea nishati hiyo kwa maendeleo yao ya kila siku. Muabhi alisema serikali kama imedhamiria kuwasaidia wananchi ihakikishe suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika linakuwepo na kwa bei ya chini.
Hata hivyo licha ya makampuni hayo kuilangua Tanesco Watanzania wanabeba mizigo mizito ya kuwanunua gesi ama mafuta mazito, pia huwalipia bima wafanyakazi hao na kuwabeba kwa kila kitu japo tena wanaiuzia umeme. Hata hivyo umeme unakatika kila wakati na kusababisha wazalishaji hasa viwanda na kampuni kutumia jenereta kuzalisha hivyo kuongeza gharama zaidi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment