Social Icons

Pages

Saturday, January 17, 2015

VIGOGO ZAIDI ESCROW KORTINI

Vigogo wengine watatu ambao ni pamoja na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu  (BoT) Julius Angello, wamefikishwa mahakamani Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwenye  akaunti ya Tegeta Escrow.
Fedha hizo  walihamishiwa na James Rugemalira, aliyekuwa mbia wa kampuni ya IPTL iliyokuwa mmiliki wa akaunti ya Escrow. Wengine ni Mwanasheria Mwandamizi wa Shirika la Umeme (Tanesco), Steven Urassa, na Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Kyabukoba Mutabingwa.
Angello alisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Devotha Kisoka  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na upande wa Jamhuri ulioongozwa na mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai akisaidiana na Max Ari. Swai alidai kuwa Februari 6 mwaka jana kwenye Benki ya Mkombozi Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa Fedha wa BoT alipokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kupitia akaunti yake namba 00120102646201 zilizoingizwa na  Rugemalira .
Ilielezwa kuwa mshitakiwa huyo aliidhinisha malipo ya kutoka Tegeta Escrow kwenda Pan African Power Solutions (T) Limited. Angello  alikana shitaka hilo na kutakiwa kukamilisha taratibu za dhamana na  kesi hiyo itatajwa tena Januari 27 mwaka huu. Mshitakiwa wa pili Urassa alisomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi, Janet Karienda ambapo Mwendesha Mashitaka Swai alidai kuwa Februari 14 mwaka jana katika benki hiyo ya Mkombozi akiwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, alipokea rushwa ya Sh milioni 161.7 kupitia akaunti yake  namba 00120102658101  fedha ambayo ni sehemu ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipokea fedha hizo kama zawadi baada ya kuwakilisha Tanesco kuingia mkataba na makampuni mengine mahakamani. Mshitakiwa  Mutabingwa alisomewa mashitaka manne ambapo Swai alidai katika shitaka la kwanza mnano  Januari 27 mwaka jana katika benki ya Mkombozi,  akiwa Meneja wa Msahama wa Kodi wa TRA alijipatia rushwa ya Shilingi bilion 1.6 kupitia akaunti yake   namba 00110202613801.
Kama wengine  fedha hiyo ni sehemu ya Tegeta Escrow ambazo alipokea kutoka kwa Rugemalira. Ilidaiwa kuwa alipokea fedha hizo kama zawadi kuwakilisha TRA na Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo mmiliki wake ni Rugemalira.
Swai alidai kuwa katika shitaka la pili Mutabingwa  inadaiwa kuwa mnamo Julai 15  mwaka jana katika benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya Shilingi milioni  161.7 kwenye  akaunti yake ambazo ni sehemu ya Tegeta Escrow kutoka kwa Rugemalira. Ilidaiwa mshitakiwa huyo alipokea fedha hiyo kama zawadi kwa kuiwakilisha TRA na Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo inamilikiwa na Rugemalira mahakamani.
Shitaka la tatu lilidaiwa kuwa mnamo Agosti 26 mwaka jana katika benki ya Mkombozi  alipokea rushwa ya Shilingi  milioni  161.7 kupitia akaunti yake kutoka kwa Rugemalira. Ilidaiwa kuwa mshtakiwa  alipokea fedha hizo kama zawadi kwa kuiwakilisha mahakamani TRA na Mabibo Beer Wines and Spirits inayomilikiwa na Rugimalira.
Katika shtaka la nne  inadaiwa kuwa Novemba 14 mwaka jana alipokea rushwa  ya Shilingi milioni  161.7 sehemu ya Tegeta Escrow  kutoka kwa Rugemalira ambayo ni zawadi  ya kuiwakilisha mahakamani TRA na Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo mmiliki wake ni Rugemalira. Alikana  mashtaka na Hakimu Karienda alimtaka atimize masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Januari 29 mwaka huu.

TAKUKURU YASISITIZA KUCHUKUA HATUA
Wakati huo huo, Takukuru, imesisitiza kuwa wahusika waliomwaga pesa za Escrow kwa watu mbalimbali wasubiri mtikisiko hatua za kisheria. Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Oseah, alisema  wananchi wategemea kuona mkono wa dola ukiwashukia wahusika wakati wowote kuanzia sasa. Alikuwa akizungumzia hatua za kuwafikisha mahakamani  watuhumiwa wa Escrow wakiwamo viongozi na watendaji wa serikali na taasisi zake.
Akizungumza kwa methali, Dk, Oseah, alisema kinachofanyika  ni kuondoa matawi ya mti na  kitakachofuatia muda mfupi ni kuchimbua na kung’oa mizizi. “Nawaomba wananchi wavute subira, kinachofanyika hivi sawa sawa na kuondoa matawi ya mti wenye  matatizo, lakini huwezi kuondoa matawi peke yake lazima uchimbue na mizizi yote,” alisema Dk. Oseah.
Alisema anajua wananchi wanataka kuona hatua hiyo inakwenda mbali na kuwafikia wale waliohusika waliotoa pesa hizo, lakini lazima utaratibu wa kisheria ufuatwe. “Haya ni mambo ya kisheria, lazima kufuata utaratibu ninachosema watuache tufanye kazi, hakuna atakayeachwa katika jambo hili,” aliongeza kusema.
Pamoja na maofisa waliopandishwa kizimbani jana wengine waliowatangulia ni Mhandisi mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijni (Rea) Theophilo John Bwakea na Mkurugenzi idara ya Fedha, Wizara ya Ardhi na maendeleo ya Makazi Rugonzibwa Theophil Mujunangoma ambao wanakabiliwa na mashitaka ya kupokea rushwa kutoka kwa James Buchard Rugemalira.
Bwakea alidaiwa kuwa February 12 mwaka 2014, alipokea Shilingi milioni 161.7, kutoka kwa Rugemalira  ambayo ni sehemu ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kupitia akaunti  yake iliyoko Mkombozi. Aidha, Mujunangoma alidaiwa kuwa February 5, mwaka jana  alipokea rushwa ya Shilingi milioni 323.4 kutoka kwa  Rugemarila.

CHANZO: NIPASHE

No comments: