Lakini uzito mkubwa wa mwili unaweza kutokea pale mtu anapokuwa na
misuli mikubwa, mifupa mikubwa, maji mengi mwilini pamoja na mafuta.
Baadhi ya magonjwa na matumizi ya dawa pia yanaweza kuchagia mtu kuwa na
uzito mkubwa.
Kuwa na mwili wenye unene wa kupindukia ni
tofauti na kuwa na uzito mkubwa kuliko kawaida ingawa watu wengi
huchanganya mambo haya mawili na kufikiri kuwa ni jambo moja.
Unene wa kupindukia unatokana na kuwa na mafuta
mengi mwilini ambayo yanasababisha mtu kuwa na nyama nyingi ambazo
wengine huziita “minyama uzembe” na kitambi.
Lakini uzito mkubwa wa mwili unaweza kutokea pale
mtu anapokuwa na misuli mikubwa, mifupa mikubwa, maji mengi mwilini
pamoja na mafuta. Baadhi ya magonjwa na matumizi ya dawa pia yanaweza
kuchagia mtu kuwa na uzito mkubwa. Watu wenye tatizo la tezi shingo linalofanya kazi
zake chini ya kiwango wanaweza kukabiliwa na tatizo hili. Matumizi ya
dawa kama vile baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango na dawa za magonjwa
ya akili, pia yanaweza kusababisha tatizo la mwili kuwa na uzito
mkubwa.
Wanasayansi wa afya wamekuwa wakieleza kuwa kuna
uhusiano mkubwa na wa karibu sana kati ya unene wa kupindukia na
magonjwa ya moyo, kiharusi, kupanda kwa shinikizo la damu, saratani za
aina mbalimbali, kisukari, kukoroma wakati wa usingizi, maumivu ya
mgongo na uvimbe wa maungio yaani baridi yabisi. Kutokana na kupendelea
kuwa na umbo la kuvutia na sababu za kiafya, watu wengi hulazimika
kupunguza unene na uzito wa miili yao. Lakini maswali ya msingi ambayo watu wengi
wamekuwa wakijiuliza kuhusu kupungua kwa unene wa mwili ni pamoja na
njia ipi iliyo bora ya kupunguza uzito au unene?
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa lishe, njia
bora na salama ya kupunguza unene na uzito ni ulaji unaozingatia kanuni
za afya na lishe bora kwa kujiepusha na vyakula vyenye sukari nyingi na
mafuta mengi.
Njia nyingine ni kufanya mazoezi kila siku na kujishughulisha na kazi mbalimbali zinazohitaji matumizi ya nguvu. “Mazoezi ya kukimbia yanamsaidia mtu kujenga
pumzi, kuondoa maradhi madogo madogo na kupunguza uzito,” anasema
Mwalimu wa mazoezi Chiko Yosia.
Mwandishi wa habari anayeandika masuala ya mazoezi
wa Gazeti la Mwananchi, Maimuna Kubegeya akizungumzia aina ya mazoezi
yanayofanya mtu kuwa na umbo dogo anasema: “Unatakiwa kufanya mazoezi
angalau kwa saa mbili kila siku, ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha
mafuta uliyokula katika siku.”
Ingawa wataalamu wengi wamekuwa wakitoa ushauri wa
lishe na mazoezi kwa ajili ya kupunguza unene, utafiti wa hivi karibuni
uliofanyika huko Australia umebaini kuwa wengi wao hawajui wapi mafuta
yanayo sababisha ‘minyama uzembe’ yanapokwenda wakati mwili unapopunguza
unene.
Zaidi ya asilimia 50 ya wataalamu 150 walioshiriki katika utafiti huo, hawakujua wapi ‘minyama uzembe’ inapokwenda.
Madaktari na wanasayansi wengi wamekuwa wakifikiri kuwa nyama za
mafuta zinazopungua hugeuzwa kuwa nguvu na nyingine huyeyuka wakati
zinapozalisha joto.
Lakini watafiti wa masuala ya kupungua kwa unene
hivi karibuni wameibuka na ushahidi tofauti wa kisayansi kuhusiana na
jambo hili. Katika utafiti huo wamebaini kuwa kiungo muhimu mwilini kwa
ajili ya kupunguza unene ni mapafu. Utafiti wao ulichapishwa katika jarida la afya la Uingereza la The British Medical Journal toleo la 349, Desemba mwaka 2014.
Mtaalamu wa Fizikia, Ruben Meerman akishirikiana
na Mkuu wa Kitivo cha Sayansi za Bayoteknolojia na Baiomolekula, Profesa
Andrew Brown wa Chuo Kikuu cha New South Wales, Australia, wanasema
kiasi kikubwa cha mafuta yanayosababisha unene ni hewa ya ukaa ambayo
hutolewa nje kwa njia ya mapafu pale tunapopumua wakati wa mazoezi na
kazi ngumu.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa kwa kila
kilo 10 za mafuta, kiasi cha kilo 8.4 hugeuzwa kuwa hewa ya ukaa ambayo
hutolewa nje kwa njia ya kupumua na kiasi cha kilo 1.6 huwa maji ambayo
hutolewa nje kama jasho, mkojo na majimaji mengine ya mwili.
Utafiti huo unaongeza kusema kuwa unene hutokea
pale kiasi kikubwa cha wanga, sukari na protini zitokanazo na vyakula
tunavyokula vinapogeuzwa kuwa triglycerides. Hizi hutengenezwa kwa
kaboni, haidrojeni na oksijeni kisha huhifadhiwa katika seli za mafuta.
Ili kupunguza unene, ni lazima kusambaratisha muunganiko wa vimeng’enywa vinavyofanyiza ‘triglycerides’.
Katika utafiti huo pia ilibainika kuwa ili
kupunguza kilo 10 za mafuta ni lazima kuvuta hewa safi ya oksijeni kiasi
cha kilogramu 29 na kwamba mchakato huo huzalisha kiasi cha kilo 28 za
hewa ya ukaa na kilo 11 za maji. “Hakuna kitu kigeni katika elimu hii ya kemikali
za mwili, lakini kwa sababu zisizojulikana inaonekana kwamba hakuna mtu
aliyewahi kufikiria juu ya kufanya hesabu za kukokotoa kiasi hiki,”
wanasema watafiti hao. “Watu hawawezi kubaini kiasi cha hewa ya ukaa kwa
vile haionekani kwa macho wakati tunapopumua,” anasema Meerman mmoja wa
wanasayansi waliofanya utafiti huu.
Hata hivyo, watafiti hao wanaonya kuwa kupumua kwa
nguvu bila kufanya kazi ngumu au kufanya mazoezi hakuwezi kusaidia
kupunguza unene kwa vile hakuwezi kuvunja muunganiko wa vimeng’enywa
vinavyohifadhiwa katika seli za mafuta yanayotengeneza minyama uzembe na
kuzalisha hewa ya ukaa.
Kupumua kwa nguvu pekee kunaweza kusababisha
kizunguzungu, kiherehere cha moyo na kupoteza fahamu kutokana na
kukosekana kwa ulinganifu wa kemikali za mwili kwa kuingiza mwilini
oksijeni nyingi kuliko kiasi cha hewa ya ukaa inayozalishwa.
“Kwa kufanya mazoezi madogomadogo ya kukimbia kwa
muda wa saa moja badala ya kubweteka kwa saa moja, utendaji wa mwili
kushughulikia mafuta huongezeka mara saba zaidi na kuondosha kiasi cha
gramu 40 za kaboni mwilini. Hiyo pia husababisha kuongezea kwa uwezo wa mwili wa kuondosha
kaboni kwa asilimia 20 hadi kufikia kiasi cha gramu 240 kwa siku moja,”
inasema sehemu ya utafiti wa Ruben Meerman na Profesa Andrew Brown. Utafiti huo unatoa angalizo kuwa kiasi kikubwa cha
kaboni zinazopotea wakati wa kupunguza unene zinaweza kurudi mwilini
kwa njia ya kula vyakula na kunywa vinywaji vyenye sukari nyingi.
“Kupunguza unene ni jambo linalohitaji kupunguza
kiasi cha kaboni unazoingiza mwilini kwa njia ya kula kuliko zile
unazotoa mwilini kwa njia ya kupumua,” wanasema watafiti hawa.
Ingawa utafiti huu unatoa ushahidi mpya juu ya
uelewa wa namna mwili unavyopunguza unene, njia za kuupunguza zinabakia
kuwa zilezile zinazofahamika kwa muda mrefu ambazo kwa ufupi ni
kupunguza ulaji na kuongeza mazoezi ya mwili.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment