
Mbunge wa Jimbo la Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza (CCM), Charles Tizeba.
Vita vya ndugu wawili wenye itakadi tofauti za vyama
, inatarajiwa kuhamia katika jimbo la Buchosa wilayani Sengerema
mkoani Mwanza baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) mkoa wa Mwanza, Adrian Tizeba, kutangaza nia ya kumng’oa
mbunge wa sasa (CCM), Charles Tizeba.
Wawili hao ambao wamekuwa ‘hawaivi’ kutokana na itikadi za kisiasa,
wanatarajiwa kupambana iwapo wote watapitishwa na vikao vya vyama vyao
muda ukifika.
Akizungumza na wanaadishi wa habari jana, mwenyekiti huyo wa Chadema,
alisema ameamua kutangaza nia baada ya kutafakari na kujipima na kuona
maendeleo ya Buchosa yamedumazwa na mbunge aliyepo madarakani.“Nimetafakari na kujipima, huku hali halisi ya maendeleo yakiwa yamedumazwa kutokana na uongozi mbovu wa CCM uliopo madarakani,” alisema Tizeba.
Alisema licha ya mdogo wake (Charles) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi kuonekana kumpiga vita kisiasa, lakini lazima atahakikisha anamng’oa katika kiti hicho ili aweze kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo. Alieleza kuwa licha ya undugu walio nao, lakini hawezi kumuunga mkono zaidi ya kupigania aondoke pamoja na chama chake ambacho kimeshindwa kukidhi fursa ya wananchi wa jimbo hilo.
“Kufuatia mabadiliko ya demokrasia, Chadema kupitia umoja wa vyama vinavyounda Ukawa, natangaza nia ya kuwania ubunge wa Buchosa ili kumuondoa mbunge wa sasa na chama chake,” alisema.
Alisisitiza kuwa jimbo linashindwa kuendelea kutokana na kufanyika wizi wa kodi ya wananchi na wajanja wachache hususani watendaji wakuu. Tizeba alisema iwapo atafanikiwa kushika nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu mwaka huu, atahakikisha pesa zinazotolewa kwa ajiri ya miradi zinatumika kwa maendeleo ya wananchi jimboni. Hata hivyo, Tizeba amemuonya mdogo wake kuwa siasa ibaki kuwa siasa na masuala ya kindugu yabaki yawe ya kindugu, akidai kuwa mbunge huyo hutumia mbinu chafu za ‘kumuumiza’ mwenyekiti huyo wa Chadema mkoa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment