Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), limesema kuna tatizo la upatikanaji wa Luku katika
baadhi ya maeneo, lakini jitihada zinaendelea ili kurekebisha hali hiyo.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana na juzi baadhi ya wateja kukosa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi
Felichesmi Mramba alisema jana kuwa: “Tunajua kuna tatizo hilo hasa kwa
wale wanaonunua kwa wakala wetu wa Selcom na Multicom, lakini kampuni
husika ya Itron inalifanyia kazi suala hilo.
“Tumewasiliana nao na wametuhakikishia kuwa baada
ya muda mfupi watarekebisha kasoro zilizojitokeza ili huduma ziendelee
kama kawaida,” alisema Mramba. Mwananchi lilipata malalamiko hayo kutoka kwa wananchi tofauti waliotaka kujua chanzo cha kutokuwapo kwa huduma hiyo.
Mkazi wa Ubungo Riverside, Winnie Mnganga alisema
juzi alilazimika kulala gizani baada ya miamala yote aliyoifanya ya
kununua umeme kutokamilika.
“Nilinunua umeme mara kadhaa lakini sijafanikiwa
kupata units...Nilifanya hivyo tangu saa kumi na moja jioni lakini
hakukuwa na mabadiliko yoyote. Sijui Tanesco wanashida gani, wasipokata
umeme basi tatizo jingine jipya linaibuka,” alisema Mnganga. Mkazi mwingine wa Tabata Bima, Kelvin Julius
alisema alipatwa na tatizo hilo licha ya kujaribu kununua Luku kwa
kutumia njia mbalimbali, ikiwamo ya simu ya mkononi.
“Hata nilipojaribu kwenda katika kituo cha uuzaji
wa Luku hali iliendelea kuwa hivyo, japokuwa leo (jana) asubuhi
nilifanikiwa kukamilisha muamala na sasa hivi umeme upo,” alisema
Julius.
Kuhusu maeneo ya Tegeta, Changanyikeni, Mbezi na
Makongo kukosa umeme, Mramba alisema hali hiyo ilitokana na mvua
zilizonyesha juzi kuathiri miundombinu. “Nguzo tano za umeme zilianguka
Goba pamoja na nyaya kukatika, hali ilisababisha maeneo hayo kukosa
umeme,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment