Wakati wowote
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga safu mpya ya Baraza la Mawaziri
kwa kuteua waziri mwingine wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada
ya kumwondoa aliyekuwepo, Profesa Anna Tibaijuka.
Mara nyingi katika uteuzi wake Rais Kikwete
amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa
mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka
katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa. Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba
Kusini mkoani Kagera anakuwa waziri wa tatu kutoka mkoa wa Kagera
kuondolewa madarakani katika uwatala wa Rais Kikwete. Ameondolewa
kutokana na kukabiliwa na kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya
Tegeta Escrow. Wengine walioondolewa kutoka mkoa huo ni aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutokana na
kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili
pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi
aliyeondolewa kutokana na sakata la Richmond.
Iwapo Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa
kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka anatoka, huenda
nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Tibaijuka kuchukuliwa na Charles
Mwijage (Muleba Kaskazini), Gosbert Blandes (Karagwe).
Assumpter Mshama (Nkenge), Jasson Rweikiza (Bukoba
Vijijini), Eustace Katagira (Kyelwa), Deogratius Ntukamazina (Ngara) na
Dk Antony Mbasa (Biharamulo Magharibi). Kama akitumia utaratibu wa kumpandisha naibu
mawaziri, huenda nafasi hiyo ikachukuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa
Kibakwe au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine kama alivyowahi kufanya
mara nyingi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa
marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa
ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee. Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza. Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame
Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na
Madini), na Saada Mkuya (Nishati na Madini) na Janet Mbene (Naibu Waziri
Viwanda na Biashara) na Dk Asha-Rose Migiro. Dk Migiro aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria. Wabunge ambao wameteuliwa na Rais, lakini hakuwapa uwaziri
mpaka sasa ni Zakia Meghji na James Mbatia.
Waliowahi kupandishwa
Pia Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri. Amefanya hivyo kwa Dk Nchimbi ambaye kabla ya
kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Naibu Waziri wa Habari,
Vijana na Michezo. Awali alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa. Mwingine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Ezekiel Maige, ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa naibu
waziri wa wizara hiyo wakati huo ikiongozwa na Shamsa Mwangunga.
Kagasheki pia alipandishwa kutoka naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hadi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Rais Kikwete alipoingia madarakani alimpandisha
aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya
Tatu, Anthony Diallo kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo. Mwingine aliyepandishwa ni William Ngeleja, ambaye
aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, baadaye alipandishwa
kuwa waziri kamili katika wizara hiyo. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuitumikia nafasi ya naibu Waziri
wa Wizara ya Ujenzi.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara,
Dk Cyril Chami, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo baada ya
kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Celina Kombani aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baadaye alipandishwa na
kupewa Wizara ya Katiba na Sheria. Hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utumishi), ofisi aliyopewa kuiongoza tangu mwaka 2012. Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Mawaziri waliohimili mitikisiko
Pamoja na kuwapo kwa panga pangua ndani ya baraza la mawaziri,
wapo baadhi yao ambao wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais
Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya,
Stephen Wassira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli. Wengine ni
Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Dk Mary
Nagu.
Kauli ya wasomi
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Faraja Christoms, alisema; “Tatizo ni mfumo. Serikali ya awamu
ya nne imekuwa na udhaifu katika mfumo wake wa kufuatilia utendaji kazi
wa watumishi wa Serikali. Rais Kikwete alipoingia madarakani alitembelea
kila wizara na kusisitiza uwajibikaji, ila sidhani kama amekuwa
akifuatilia wizara zinatenda yapi.” Aliongeza, “Nadhani hata watendaji wa Serikali wameshajua kuwa Rais siyo mfuatiliaji nao wanafanya mambo watakavyo.”
Alisema jambo kubwa linaloitafuna nchi ni vigogo
wa Serikali kufanya kazi kwa kulindana, kukosekana kwa dhamira ya
uwajibikaji na kupeana nafasi za kazi kwa kujuana na akisisitiza kuwa
mtumishi bora ni yule mwenye uwezo na dhamira ya kufanya kazi. Profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Chris Maina alisema; “Ili kupata kiongozi mzuri ni lazima
anayemteua au kumpendekeza awe na uhakika kuwa mtu hisika ni mwadilifu,
hicho ndiyo kigezo kikubwa. Pili, lazima mtu huyo awe mtendaji na
utamjua kwa kutazama kazi alizozifanya awali, yaani historia yake katika
utendaji.” Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Tatizo ni mfumo. Hatuna
mfumo unaowandaa watu kimaadili, hilo limesababisha hata jamii nzima
kukosa maadili ambayo ndiko wanakotoka hao mawaziri na viongozi
wengine.” Alisema hata vyombo vya kusimamia uwajibikaji,
rushwa na maadili ni dhaifu. “Vyombo hivi havina meno na unaweza kudhani
kuwa vipo kwa ajili ya kuwalinda watu fulani fulani tu. Nchi za Ulaya
huwezi kukuta yanatokea mambo kama ya hapa kwetu kwa sababu wana vyombo
vinavyofuatilia watendaji kwa ukaribu zaidi na kuwachukulia hatua
wanaokiuka maadili,” alisema Profesa Makulilo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment