 
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amewasili 
nchini Ufilipino, nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi barani Asia, huku 
ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa.
Maelfu ya Wafilipino wamejipanga katika misururu mirefu kwenye barabara 
za mji mkuu wa Ufilipino, Manila, wakimkaribisha kiongozi huyo wa Kanisa
 Katoliki duniani anayezuru nchini humo kwa siku tano, akitokea nchini 
Sri Lanka. Serikali ya Ufilipino imetangaza kwamba wakati wote wa ziara 
ya Papa Francis, nchi hiyo itakuwa katika mapumziko ya kitaifa na pia 
imepiga marufuku ya pombe.
Papa atakuwa katika mji mkuu, Manila na mwishoni mwa juma atakwenda 
kwenye jimbo la mashariki la Leyte, ambapo anatarajiwa kukutana na 
wahanga wa kimbunga Haiyan, kilichoikumba nchi hiyo mwaka 2013. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Manila, Mwadhama Luis Kardinali Antonio 
Tagle amesema ziara ya Papa inafanyika wakati ambapo watu watapata 
msaada wa kiroho na kimaadili. Kardinali Tagle, amesema makanisa 
kuzunguka nchi nzima yatapiga kengele kwa wakati mmoja katika hatua ya 
kumkaribisha kiongozi huyo. Amesema wameridhishwa na kufurahishwa na ulinzi uliopo, lakini amewasihi
 watu wa usalama kutomtenganisha Papa na watu wake. Amesema Papa Francis
 ni mchungaji, hivyo anahitaji kuwa pamoja na kundi la watu wake.
Papa kukutana na Rais Aquino
Papa Francis atakutana pia na Rais Benigno Aquino, ambaye aliwahi kuwa 
katika mvutano mkali na viongozi wa Kanisa Katoliki kutokana na muswada 
wa afya ya uzazi uliokuwa unahamasisha matumizi mbalimbali ya kinga ya 
uzazi wa mpango. Hata hivyo, Bunge la Ufilipino lenye washirika wengi wa
 Rais Aquino, waliupitisha muswada huo mwaka 2012, ambao ni kiunyume na 
Kanisa Katoliki.
Mkuu wa Majeshi wa Ufilipino, Jenerali Gregorio Catapang, amesema kwa 
mwaka huu kutakuwa na ulinzi mkali kuliko ilivyo kawaida na kwamba kiasi
 watu milioni sita wanatarajiwa kuhudhuria Ibada ya Misa itakayofanyika 
siku ya Jumapili mjini Manila. Jenerali Catapang amesema karibu wanajeshi na askari polisi 
40,000 wametawanywa kwa ajili ya kumlinda Papa Francis wakati wa ziara 
yake. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufilipino, Mar Roxas amesema 
wanatarajia kuwa msafara wa Papa utazunguza kwa muda wa saa tatu, ili 
kuweza kushuhudiwa na karibu watu nusu milioni.
Akiwa nchini Sri Lanka, Papa Francis alisema dini kamwe haiwezi kuwa 
kisingizio cha kufanya vurugu na kwamba maridhiano hayawezekani bila 
ukweli kubainishwa. Papa aliutembelea msitu mnene kaskazini mwa nchi 
hiyo katika kuonyesha mshikamano na wahanga wa vita vya wenyewe kwa 
wenyewe vilivyodumu kwa miaka 25. Papa Francis ni Papa wa tatu kuzuru Ufilipino. Mwaka 1995 kiasi 
Wakatoliki milioni nne walihudhuria Ibada ya Misa iliyoadhimishwa na 
Papa Yohane Paulo wa Pili katika uwanja wa Rizal, na hivyo kuwa umati 
mkubwa kabisa kuwahi kushuhidiwa katika matukio yote ya Papa. Aidha, 
mnamo mwaka 1970, Papa Paulo wa Sita, alizuru Ufilipino.
CHANZO: DW KISWAHILI 
No comments:
Post a Comment