Pages

Saturday, January 17, 2015

NYOTA 11 WATAKAOKOSEKANA AFCON

Kombe la Afcon 
Malabo, Guinea ya Ikweta Fainali za Mataifa ya Afrika 2015, zimeanza Jumamosi nchini Guinea ya Ikweta kwa timu 16 kusaka ufalme wa taji hilo.
AFCON 2015 kama yanavyojulikana yameanza Januari 17 na yakitarajiwa kumalizika Februari 8. Licha ya kuwa mataifa 16 yatakuwa yakiwania taji hilo la Afrika, hakutakuwa na mabingwa watetezi, Nigeria, ambao wameshindwa kufuzu. Hata hivyo, licha ya kuwa na baadhi ya timu zilizoshindwa kufuzu, kuna kikosi kizima ambacho kinakosa mashindano haya kwa sababu mbalimbali, nacho ni hili.

Senzo Meyiwa (Afrika Kusini)
Kipa na nahodha wa Bafana Bafana hatakuwamo katika mashindano haya baada ya kupoteza maisha alipovamiwa na kupigwa risasi na majambazi Oktoba mwaka jana akiwa katika nyumba ya mpenzi wake mjini Vosloorus, Kusini mwa Johannesburg. Mlinda mlango huyo wa Orlando Pirates, alicheza vizuri katika mechi za kufuzu kwa mataifa ya Afrika katika michezo minne ya Afrika Kusini.

Geoffrey Massa (Uganda)
Nahodha huyu wa University of Pretoria inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini amekuwa katika kiwango kizuri kwa klabu na timu yake, lakini ataendelea kuisubiri Uganda kupata nafasi ya kucheza AFCON. Uganda ilikuwa karibu kupata nafasi ya kufuzu, lakini ilipoteza mbele ya Guinea katika mchezo wao wa mwisho wa kufuzu. Massa alikuwa miongoni mwa wachezaji wazuri katika ufungaji akiwa na mabao manne.

Mehdi Benatia (Morocco)
Beki huyo wa Bayern Munich anaweza pengo kubwa katika fainali za Mataifa ya Afrika msimu huu. Anayakosa mashindano ya msimu huu kutokana na kuenguliwa kwa Morocco. Baada ya Bayern akitokea AS Roma, beki huyo kwa sasa ndiye mchezaji anayelipwa zaidi kati ya nyota wa Afrika wanaocheza Ulaya.

Saladin Said (Ethiopia)
Ethiopia ilikuwamo katika fainali za mwisho za AFCON, lakini wanayakosa mashindano ya msimu huu na nyota kama Said hawatakuwa na nafasi ya kuonyesha vipaji vyao. Mchezaji huyo anaitumikia klabu ya Misri ya Al Ahly SC.

John Obi Mikel (Nigeria)
Unamzungumzia kiungo mwenye uwezo na uzoefu katika soka ya kimataifa akiwa na klabu kubwa Chelsea na Super Eagles ya Nigeria. Lakini mabingwa watetezi wa mashindano haya, Nigeria hawatakuwa na nafasi tena ya kucheza msimu huu baada ya kushindwa kufuzu na Obi atakuwa akiangalia fainali hizi runingani.

Kwadwo Asamoah (Ghana)
Black Stars ya Ghana ambayo imefuzu katika Kundi E itamkosa kiungo wa Juventus kutokana na kuwa majeruhi. Asamoah ambaye pia alikosa mechi mbili za kufuzu dhidi ya Uganda na Togo ameondolewa kikosini na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na maumivu ya goti.

Victor Wanyama (Kenya)
Kiungo huyo ambaye amekuwa katika kiwango kizuri akiwa na Southampton FC ya Ligi Kuu England hayumo katika fainali za msimu huu baada ya Kenya kushindwa kufuzu. Harambee Stars ilishindwa mapema katika ngazi ya awali ya kufuzu kwa fainali hizo kubwa za Afrika kwa upande wa soka.

Mohamed Salah (Misri) 
Fainali za msimu huu zinamkosa pia winga mwenye kasi wa Chelsea na Misri. Timu yake imeshindwa kufuzu kwa fainali hizo. Licha ya kuiwakilisha Misri hatua za awali za kufuzu, pia alikuwamo katika fainali za 2011 za Kombe la Dunia la vijana (U-20) na michezo ya Olimpiki ya 2012. Pia alitwaa tuzo ya CAF ya nyota bora wa Afrika anayechipukia ya 2012.

Emmanuel Adebayor (Togo)
Mshambuliaji huyo wa Tottenham ya England hatakuwa Guinea ya Ikweta katika fainali za msimu huum kuonyesha uwezo wake. Timu yake ilifanikiwa kuifunga Uganda pekee mara mbili katika harakati za kufuzu kutoka Kundi E la michezo ya kufuzu kwa AFCON 2015.

Didier Drogba (Ivory Coast)
Mmoja kati ya wachezaji vipenzi wa Waafrika, mshambuliaji huyu hatakuwa sehemu ya wachezaji wa Ivory Coast nchini Guinea ya Ikweta kutokana na kustaafu soka ya kimataifa. Lakini, aliendelea kucheza kama mchezaji muhimu wa kikosi cha Chelsea kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu Egland na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment