
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda.
     
Jeshi la Polisi limekubwa na dhahama nyingine baada 
ya  askari wake wawili wa mkoani Tabora, kupewa kipigo kwa madai ya 
kusababisha kifo cha kijana mmoja wa mjini humo.
Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani. Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania 
(JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani 
Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali 
zikiwamo bunduki na risasi.
Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati 
akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa 
lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za  kushiriki mchezo wa 
kamari. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, akizungumza na 
NIPASHE alisema tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu  saa 10.30 
jioni katika mtaa wa Kadinya kata ya Ng’ambo.
Kamanda Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  PC Yohana na MW 
Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete  kutokana na
 kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi. Alisema wananchi walianza kuwashambulia askari hao walipotaka 
kuwakamata vijana watatu waliokuwa wakicheza kamari kijiweni katika eneo
 la Ng’ambo mjini Tabora.  Vijana hao baada ya kubaini wanataka kukamatwa na polisi walianza 
kukimbia na bahati mbaya mmoja wao alitumbukia ndani ya dimbwi la maji 
na kuzama.
Kaganda alisema kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Edwin Kefa 
(19), baada ya kutumbukia katika dimbwi hilo,  alishindwa kuogelea na 
hivyo askari waliokuwa wakimfukuza walimuokoa akiwa katika hali mbaya na
 kukimbizwa katika Hospitali ya Kitete, lakini alifariki  wakati 
akipatiwa matibabu.
Alisema pamoja na askari hao kushambuliwa, Jeshi hilo litaendelea 
kufanya msako mkali ili kuvunja vijiwe vyote vya wacheza kamari, wavuta 
bangi na wanaotumia dawa za kulevya mkoani Tabora. Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wananchi walichukua 
uamuzi wa kuwashambulia askari hao baada ya kuona wakimpiga  kijana 
aliyepoteza maisha kabla ya kufikwa na mauti.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kitete, Dk. Yusuph Bwire,
 alisema hali za askari hao zinaendelea vizuri na kwamba  Isonda 
alijeruhiwa begani na kichwani. Dk. Bwire alisema Yohana alijeruhiwa kichwani na kwamba aliruhisiwa jana asubuhi  baada ya hali yake kuwa nzuri.
JWTZ YAJITIOSA RUFIJI
Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu 
waliokiteka na kukivamia kituo cha polisi Ikwiriri na kuwaua askari 
wawili na kuiba silaha. Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul 
Chagonja, akizungumza katika mahojiano na Redio One katika kipindi cha 
Kumepambazuka, alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania 
(JWTZ) ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanatiwa mbaroni. Kamishna Chagonja alisema hadi kufikia jana jioni hakuna mtu 
aliyekuwa amekamatwa na wamebaini kuwa bomu lililorushwa katika kituo 
hicho halikuwa moja bali yalikuwa mengi.
“Uvamizi ulikuwa mkubwa na inaonekana waliofanya tukio hilo 
 walikuwa si chini ya 15 na baada ya kufanya tukio hilo waliondoka kwa 
kutumia Noah,” alisema. Alisema mabaki ya bomu lililorushwa yamepekwa kwa wataalam kubaini ni bomu la aina gani. Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, alisema tukio la kuvamiwa kituo hicho lilitokea saa 8:00 usiku.
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa kuwa ni PC Judith Timoth na 
 Koplo Edga Mlinga ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na 
kwamba miili ya askari  imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri. Alisema baada ya kukivamia kituo hicho waliiba bunduki aina ya SMG 
mbili, SAR mbili, Shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na bunduki mbili za 
kulipulia mabomu ya machozi.
Matei alisema baadaye walilipua bomu kituoni hapo ambalo 
liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi wa
 Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana. Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jeshi hilo lina idara
 nyingi, hivyo taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kushirikiana 
katika uchunguzi wa tukio hilo zinaweza kuwa za kweli.
CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment