Pages

Tuesday, January 20, 2015

NCHEMBA AWATUMIA SALAMU WANAOIBA FEDHA ZA UMMA

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba.
Chama Cha Mapinduzi CCM kimetoa onyo kali kwa yaliyoiba  na watakaoiba fedha za umma kwamba hawatabaki salama kwa kuwa watafungwa jela.
Onyo hilo lilitolewa na  Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika uwanja wa Orofea wilayani Muheza, mkoani Tanga. Alisema kuwa Chama hakitamvumia mtu yeyote aliyekula fedha za umma na atakaekula hatabaki salama kwa lengo la kurejesha imani ya wananchi kwa serikali na CCM.
Nchemba alisema kuwa CCM kupitia serikali yake itahakikisha inawachukulia hatua za sheria na nidhamu wanachama wake na viongozi watakaojihusisha na  ufisadi wa kula fedha za umma. Aidha aliwataka viongozi wote waliyochaguliwa katika uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji, vitongoji,na mitaa na wajumbe kusimamia haki itendeke na kuwawajibisha watendaji wabadhirifu.
Nchemba aliwaagiza kusimamia, kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu utaratibu mzima wa ugawaji wa dawa na upatikanaji wake kwa wagonjwa katika hospitali wilayani Muheza. Alimwagiza mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, kwamba muuguzi yeyote atakayekamatwa na kosa la kuiba dawa hospitali na kupeleka katika maduka yao ya kuuza dawa amkamate na kumpeleka polisi ashtakiwe kwa vile ni muuaji na awaachie vibaka walioiba simu ama kuku.
Nchemba aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura huku akipongeza  CCM wilaya ya Muheza kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi  wa wenyeviti wa serikali za vijiji na vitongoji. Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilaya ya Muheza, Fikirini Masokola, alisema kuwa chama katika wilaya hiyo kimejipanga vizuri katika uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Muheza, Peter Jambele na Katibu Mwenezi wa CCM wilaya hiyo, Makame Seif, kwa nyakati tofauti walisema kuwa wamepata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo kutokana na kazi kubwa ya uhamasishaji wanayoifanya ndani ya chama hicho.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment