Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeongoza mazungumzo ya Geneva, Leon Bernardino
Mazungumzo ya amani kati ya makundi yanayohasimiana nchini Libya
yanaendelea mjini Geneva. Umoja wa Mataifa umeonya mazungumzo hayo
yaliyoanza jana (15.01.2015) huenda ni fursa ya mwisho kuepusha vita.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Leon Bernardino amesema mchakato wa
kuyafikia makubaliano ya amani ya Libya utakuwa mgumu na mrefu.
Bernardino ambaye anayasimamia mazungumzo hayo mjini Geneva nchini
Uswisi amekiri hawatarajii kufikia muafaka leo wala kesho, kwa sababu
kuna pengo kubwa kati ya makundi ya Libya, ambalo linazidi kutanuka
kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.
Bernardino aidha amesema mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa
Mataifa yanalenga kufikia suluhisho la kisiasa na makubaliano ya kuundwa
kwa serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo Walibya wote watawakilishwa.
Serikali hiyo itachukua nafasi ya tawala zinazopingana, ambazo vita vyao
vya kung'ang'ania madaraka vimesababisha vifo vya mamia kadhaa ya watu
katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Mazungumzo ya Geneva yananuia kufikia makubaliano kuhusu mbinu za
kuyakomesha kabisa mapigano na kuhakikisha makundi yote yenye silaha
yanaondoka kutoka miji mikubwa. Bernardino amesema, "Ni muhimu sana
kwamba suluhisho lolote litakalofikiwa katika mazungumzo haya liungwe
mkono kwa dhati na watu wa Libya. Sidhani kama kutakuwa na haja kwa
serikali ya mpito inayotakiwa kuikwamua nchi kutokana na machafuko
kuandaa kura ya maoni. Kuna mapigano yanayoendelea na hali ni ngumu.
Huwezi kuandaa kura ya maoni wala uchaguzi kukiwa na machafuko."
Mkutano wa Geneva ulitarajiwa kuwaleta pamoja wajumbe wa serikali
iliyojitangazia madaraka ambayo iliudhibiti mji mkuu Tripoli mwaka
uliopita, pamoja na serikali inayotambuliwa kimataifa ya waziri mkuu
Abdullah al-Thini, na makundi ya waasi yanayoziunga mkono serikali hizo
mbili. Watawala wa Tripoli walisema bunge leo limeahirisha uamuzi wa
kujiunga na mazungumuzo ya Geneva mpaka Jumapili ijayo kwa sababu ya
wasiwasi kuhusu jinsi yalivyoandaliwa, hatua inayouweka mchakato mzima
mashakani.
Mazungumzo hayatafua dafu
Wachambuzi wameonya kwamba mazungumzo ya Geneva huenda yasiwe na tija
yoyote mpaka viongozi wa makundi yaliyojihami na silaha ya Libya, ambao
baadhi yao hawashiriki mazungumzo hayo, washirikishwe moja kwa moja.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Mohammed al-Ferjani amesema mdahalo
unaoendelea Geneva hautazaa matunda kwa sababu Umoja wa Mataifa
haukuchagua washiriki wanaostahiki.
Bernardino amesema mazungumzo haya ya kwanza yanatarajiwa kuendelea hadi
kesho Ijumaa na kuanza tena wiki ijayo kama kundi la mjini Tripoli
litaamua kuhudhuria, lakini duru zaidi za mazungumzo huenda zikafanyika
katika maeneo mbalimbali.
Umoja wa Ulaya umeyaeleza mazungumzo ya Geneva kuwa fursa ya mwisho
kuutanzua mzozo wa Libya, ambako serikali mbili zinazopingana na makundi
yenye silaha yanalitishia taifa hilo kutumbukia katika vita vya wenyewe
kwa wenyewe, ikiwa ni miaka mitatu tangu kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi
wa nchi hiyo hayati Muammar Gaddafi.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment