
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameahidi kuwalinda Wayahudi na Waislamu wanaoishi nchini Ujerumani dhidi ya ubaguzi.
Amesema demokrasia ndiyo njia bora ya kupambana na machafuko
yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali, kama yale matukio ya nchini
Ufaransa wiki iliyopita. Kauli hiyo ameitoa leo baada ya bunge la Ujerumani-Bundestag,
kuwakumbuka kwa dakika moja wahanga 17 waliouawa katika mashambulizi ya
wiki iliyopita mjini Paris. Merkel amesema Uyahudi na Uislamu vyote ni
sehemu ya Ujerumani na ameahidi kwamba suala la kupambana na Uyahudi na
mashambulizi dhidi ya misikiti litakuwa na mashtaka sawa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha bunge kilichohudhuriwa na balozi
wa Ufaransa nchini Ujerumani na viongozi wa kidini, Merkel amesema
Ujerumani na Ufaransa zinahusiana kutokana na urafiki muhimu walionao. ''Ujerumani na Ufaransa zinasimama pamoja wakati wa matatizo haya
magumu. Ujerumani na Ufaransa zinasimama pamoja zikijua wazi kwamba
Ujerumani haiwezi kuwa na usalama, iwapo hakuna usalama Ufaransa,
alisema Merkel .''
Kansela Merkel amesema ni muhimu pia kwa viongozi wa dini ya Kiislamu
kuandaa mwongozo wa wazi unaotofautisha kati ya Uislamu na ugaidi.
Amesema watu wengi nchini Ujerumani siyo maadui wa Uislamu, ingawa watu
wanataka kujua ni kwa nini magaidi hawana huruma na maisha ya binaadamu. Amesema viongozi hao wanapaswa kueleza ni kwa nini mara nyingi ghasia zinafanyika kwa kutumia imani yao.
Ujerumani haitoyumbishwa na vitendo vya itikadi kali
Amebainisha kuwa Ujerumani haitoyumbishwa kwa vitendo vya itikadi kali
na itahakikisha inapambana na mahubiri ya chuki, vurugu na ghasia
zinazofanywa kwa kutumia jina la Usialmu na wale walio nyuma ya ghasia
hizo. Merkel amesema hatua zilizochukuliwa na Ujerumani na Ulaya ili
kuweka ulinzi dhidi ya kitisho cha ugaidi na Uislamu wenye itikadi kali,
hazitowaruhusu magaidi kuigawa jamii.
Amesema baada ya kufanikisha hatua ya kupiga marufuku watu wanaoshukiwa
kuwa wapiganaji wa Jihadi, baraza lake la mawaziri litaweka adhabu kali
kwa watu wanaofadhili ugaidi. Hata hivyo, Ujerumani itaendelea kutoa
msaada wa silaha na mafunzo ya kijeshi kwa majeshi ya Wakurdi
wanaopigana na kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS,
nchini Iraq na Syria. Aidha, Kansela Merkel ameunga mkono wazo la kuwepo uchunguzi zaidi wa
data za mtandaoni ili kupambana na ugaidi na katika hatua za kuhakikisha
usalama. Ametoa wito wa kuanzishwa upya hatua za kuwaruhusu maafisa
kuficha data, suala ambalo wakosoaji wanasema huenda likahujumu uhuru wa
vyombo vya habari na kukiuka haki za kimsingi za umma. Mashambulizi ya Paris yametokea wakati ambapo Ujerumani ikitathmini
namna ya kukabiliana na maandamano katika mji wa mashariki wa Dresden
yanayoongozwa na kundi linalopinga Uislamu linalojiita PEGIDA.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment