
Hawa Kundani (mwenye vazi jeusi), anayedai kuzaa na kutelekelezwa na
mbunge wa Dimani, Abdallah Sharia Ameir, akiwa chini ya ulinzi wa polisi
baada ya kuvamia kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kilichokuwa kikifanyika Dar es Salaam jana.
Mwanamke aliyetambulika kwa jina
la Hawa Kundani amezua taharuki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala, baada ya kuvamia ghafla na kupiga kelele
akidai kutelekezwa na mumewe ambaye ni Mbunge wa Dimani (CCM) visiwani
Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana kwenye
Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, na mwanamke huyo
akiwa ameongozana na mtangazaji wa kituo kimoja cha redio, Joyce Kiria
aliingia na kusababisha mshtuko kwa wajumbe wa kamati hiyo na viongozi
wa dini ya Kikristo waliokuwa wamealikwa hapo. Wakati huo walikuwa
wakijadiliana suala la Mahakama ya Kadhi.
Hawa akizungumza na gazeti hili alidai kwamba
Ameir ni mume wake walifunga ndoa mkoani Arusha mwaka 1999 na kuzaa naye
watoto wanne, lakini mmoja alifariki dunia. “ Nashangaa amebadilika ghafla amekuwa mtu wa kuoa
wanawake na kuacha mara kwa mara, hadi sasa ameshaoa wanawake wanne na
kuwaacha mimi nipo tu, alinioa bado mdogo,” alidai Hawa.
Alidai kuwa watoto wengine wawili, mkubwa ana
miaka tisa na mwingine miaka sita walichukuliwa na mumewe huyo
akawapeleka kulelewa na mwanamke aliyemuoa jambo ambalo alidai
linamuuma.
“ Naumia wanangu sijui wanaishi vipi, huyu
niliyembeba ni mlemavu, hamtaki amekuwa akininanga kwa maneno mengi
sana, mimi nimetoka naye mbali nilibadili dini kwa ajili yake, leo hii
ananitesa, hanitaki anipe haki yangu ili niishi mwenyewe,” alisema Hawa.
Kwa upande wa mbunge hiyo Ameir alidai kwamba kesi
yao ipo kwenye Mahakama ya Kadhi, akidai kwamba mwanamke huyo amekuwa
akimdhalilisha kwa kupitia mtoto huyo mlemavu ambaye alikiri ni mwanaye. “ Huyu ni mwanangu sishindwi kumhudumia, lakini
sitaki fedha ziende kwa huyu mwanamke atazitumia kwa mambo yake mengine,
mimi nilimpeleka kwa mama yake mzazi akakae naye huko lakini yeye
hataki,” alisema Mbunge Ameir. Akizungumzia tukio hilo Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema ni tukio ambalo limewafedhehesha
kwa kuwa hawakulitarajia.
“Tulivamiwa na wanawake kama wanne na wanaume
wawili nafikiri mmoja alikuwa ni mpiga picha, mwanamke mmoja akawa
anapiga kelele, tulitaharuki kwa sababu maaskofu walikuwa wameanza kutoa
maoni yao,” alisema. Alisema kwamba waliomba msaada kwa maofisa usalama
wa ukumbi na walifika na kuwachukua wahusika hao, kisha kuwapeleka
polisi kwa hatua zaidi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment