Wakati papa Francis amehitimisha ziara yake nchini Sri Lanka, ujumbe
mkuu wa kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani ni wa kuzingatiwa na
ulimwengu mzima, anasema mwandishi wa DW Petersmann Sandra.
Dini kamwe haiwezi kuwa kisingizio cha kufanya vurugu. Na maridhiano
hayawezekani bila ukweli kubainishwa. Masuala hayo mawili ndiyo yalibeba
ujumbe mkuu wa ziara ya papa nchini Sri Lanka. Mtu hapaswi kuipenda
Vatikan au kuwa Mkatoliki safi ili kuona umuhimu wa ujumbe huu. Ndiyo
maneno sahihi kwa wakati sahihi.
Sri Lanka ndiyo imekamilisha mchakato wa mabadiliko ya uongozi ambao
haukuwa unatarajiwa. Taifa hilo la kisiwa lenye wakaazi karibu milioni
21 halionekani mara kwa mara kwenye jukwaa la habari za kimataifa -
ambalo pia lilitokana na ukweli kwamba serikali iliyoondolewa ya rais
Mahinda Rajapaksa ilikuwa imeukanyaga uhuru wa vyombo vya habari. Wakati
huo huo lulu hiyo ya bahari ya Hindi imezidi kupendwa na watalii, hata
kutoka Ujerumani. Kisicho bayana ni iwapo wasafiri wanaipenda pia nchi
hiyo na watu wake.
Ziara katika taifa lililogawika
Papa amefanya ziara katika wakati nyeti kisiasa, kwenye taifa lililoko
pembezoni. Taifa dogo ambako matatizo mengi ya ulimwengu mpana wa sasa
yanaakisiwa. Sri Lanka ni nchi yenye makabila mengi, dini nyingi na
imegawika. Nchi hiyo ndiyo inaanza kutibu majeraha ya vita vya ugaidi
vilivyodumu kwa karibu miongo mitatu. Mwaka 2009 jeshi lililisambaratisha kundi la waasi wa kabila la Tamil,
ambalo lilikuwa likiwatumia watoto na waripuaji wa kujiota muhanga
kulaazimisha kuunda taifa huru la Watamil. Katika vita vya mwisho
vilivyopiganwa kwenye ukanda mdogo wa pwani ya kaskazini, waasi wa Tamil
waliwatumia raia kama ngao - wakati jeshi lililokuwa linasonga mbele,
liliuwa na kushinda.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, pande zote mbili zilihusika na ukiukaji
mkubwa wa haki za binaadamu. Hata hivyo, baada ya ushindi serikali
ilikwenda na kuchora msitari na Sri Lanka ya kaskazini ya Watamil
iliendelea kuwa ukanda maalumu wa vita. Hakukuwa na juhudi zozote za
maridhiano wala upatanishi hadi hii leo. Watu kutoka kabila la walio
wengi la Sinhale wanahodhi nafasi zote muhimu katika serikali, jeshi na
uongozi. Dini yao ya Budha, inaonyesha kuwa dini yoyote inaweza kuwa na sura ya
chuki na itikadi kali - kila wakati watu wanapotumia dini kama silaha
dhidi ya watu wengine. Sri Lanka imeshuhudia katika miaka iliyopita,
mamia ya mashambulizi dhidi ya Wahindu wa kabila ya Tamil, na pia dhidi
ya makundi ya dini za wachache - Wakristu na Waislamu.
Nafasi ya maridhiano
Baada ya utawala wa miaka kumi wa Rajapaksa, Sri Lanka sasa ina rais
mpya. Mbudha Maithripala Sirisena alishukuru ushindi wake hasa kwa
wapiga kura wa Tamil, na Waislamu na Wakristu wa Sri Lanka. Sirisena
sasa anaweza kujenga demokrasia imara nchini Sri Lanka, ikiwa
atazingatia ujumbe wa kimataifa wa papa, unaosema: Kamwe dini isitumiwe
kwa kisingizio cha vurugu. Na maridhiano bila ukweli hayawezekani.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment