Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
Jana katika tovuti hii tulichapisha habari
iliyokuwa ikielezea kikundi cha wahuni wanaojiita ‘Panya Road’ walizua
taharuki jijini Dar es Salaam juzi baada ya kuvamia wananchi na
kuwapora mali zao.
Taarifa za kundi hilo lililopora watu katika
baadhi ya maeneo ya jiji hilo, zilienea kwa kasi ya ajabu kupitia
mitandao ya kijamii watsapp, twitter, jamii forum, blog, instagram na
ujumbe mfupi wa simu.
Kutokana na kuenea kwa taarifa hizo zilizotisha
baadhi wafanyabiashara walifunga maduka, baa na wengine wakijifungia
majumbani mwao kuwakwepa wahalifu hao.
Baadhi ya maeneo ambako kundi hilo linadaiwa
kufanya uporaji ni Tabata, Magomeni Kagera, Sinza, Mwananyamala,
Kinondoni, Kijitonyama, Manzese, Kigogo na Buguruni, huku wanafunzi
wanaoishi katika Hosteli za Chuo Kikuu Dar es Salaam, wakitoka nje ya
mabweni yao kwa kuhofia kuvamiwa na kikundi hicho. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alikaririwa akikiri kuwapo kwa vijana hao waliokuwa
wametanda katika eneo la Magomeni Kagera na kwamba polisi walifika eneo
hilo kuwadhibiti na kufanikiwa kuwakamata wawili.
Alisema kwa sasa wananchi wana hofu tu ya tukio
lile la Magomeni kutokana na kusambaa kwa uvumi na hakukuwa na jambo
tofauti na uhalisia wenyewe. Kova alisema hakuna taasisi inayoitwa Panya Road
na kusisitiza kuwa vijana hao ni watoto wadogo waliokosa msingi wa
malezi katika jamii, huku akiwataka wananchi wakiwaona vijana hao
kutowapiga ili kuepusha vijana hao kulipiza kisasi.
Tunachukua nafasi hii kulishauri Jeshi la Polisi kuacha kutoa taarifa za kisiasa katika jambo kubwa kama hili.
Hatukutarajia kuona Kamanda Kova akitoa taarifa
kama hiyo ya kwamba vijana waliokuwa wakifanya uhalifu huo ni vijana
wadogo waliokosa msingi wa malezi katika familia zao.
Hata makundi makubwa ya wahalifu yaliyopo duniani
yote yanaanza kama hawa Panya Road, huwezi kuwadharau wakati
wamesababisha karibu jiji zima kutikiswa.
Tunajiuliza, hivi jukumu la kulinda raia na mali
zao ni la nani? Ni wazi kuwa ni la polisi ambao sasa Kamanda Kova
anasema kuwa Panya Road ni watoto wadogo waliokosa msingi wa malezi,
hivyo kwa maana nyingine hawana madhara. Jeshi la Polisi sasa lijipange vyema kudhibirti
makundi ya uhalifu kama haya ambayo yapo mengi katika Jiji la Dar es
Salaam na yamekuwa yakifunga mitaa na kupora wananchi bila kudhibitiwa.
Lakini kinachoshangaza ni kwamba Jeshi la Polisi limekuwaa
likionekana kupata taarifa za kiintelijensia mapema zaidi katika
kudhibiti mikutano ya siasa au maandamano ya wanasiasa ambayo Serikali
imeyazuia.
Tulitarajia kwamba Jeshi la Polisi ambalo limejaa
vijana wenye ujuzi wa kuchunguza, Panya Road wangekamatwa kabla ya
kufanya uhalifu huo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment