Spika wa Bunge, Anne Makinda akipokea kutoka kwa Balozi wa China hapa
Nchini, Dk Lu Youquing baadhi ya vifaa vya Tehama vilivyotolewa na
serikali ya China kwa ajili ya kusaidia shughuli za Bunge, katika hafla
iliyofanyika kwenye ofisi ya spika Dar es Salaam jana. Kulia ni Kamishna
wa Bunge, Dk Maua Daftari.
Spika wa Bunge,
Anne Makinda amesema hawatambui wenyeviti wa kamati tatu za kudumu za
Bunge ambao Bunge liliazimia wavuliwe nyadhifa zao kutokana na kutajwa
katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow. Pamoja na kuwapo kwa maagizo ya Bunge, baadhi yao
wanaendelea kujinasibu kuwa bado ni wenyeviti huku mmoja wao akiongoza
vikao vya kamati. Akizungumza Dar es Salaam jana, Makinda alisema
anachofahamu ni kuwa wenyeviti hao tayari wamaeshajiuzulu na kamati zao
zinatakiwa kufanya uchaguzi wa wenyeviti wengine.
Wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni Victor
Mwabalaswa (Nishati na Madini), Andrew Chenge (Bajeti) na William
Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), ambaye hadi jana mchana alikuwa
akiongoza kikao cha kamati hiyo. Siku tano zilizopita Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashilillah alieleza kuwa kamati hizo zinatakiwa kufanya uchaguzi na
kwamba wenyeviti hao hawakutakiwa kuongoza vikao, lakini hadi jana,
hakuna uchaguzi wowote uliokuwa umefanyika na baadhi wanaendelea na
majukumu yao.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge katika
azimio lake la tatu, liliazimia kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya
miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakiwamo viongozi wa kamati hizo
tatu, wachukuliwe hatua kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge
unaotarajiwa kuanza Januari 27.
Ngeleja alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni
akisema kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa
uchunguzi sakata hilo bado unaendelea na ikithibitika ndipo Bunge
litachukua uamuzi ambao alisema atakuwa tayari kuutekeleza.
Bunge lapata msaada
Katika hatua nyingine, Makinda amesema Bunge
litaanza kutumia vifaa teknolojia kuwasilisha taarifa mbalimbali na
kuachana na utaratibu wa kudurufu nyaraka nyingi ili kuepusha gharama.
“Bunge linatumia zaidi ya Sh1 bilioni kudurufu
miswada na nyaraka nyingine za wabunge. Sasa tunataka kutumia mfumo wa
kisasa. Kila kitu kitakuwa katika kompyuta za wabunge,” alisema.
Kauli ya Makinda imekuja wakati akishukuru baada
ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali vya mawasiliano na kazi kutoka
Serikali ya China. Balozi wa China nchini, Lu Youqing alimpatia Spika
Makinda misaada ya vifaa hivyo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) vyenye thamani ya Dola100,000.
Vifaa hivyo ni printa kubwa 10, mashine 10 za kudurufu 10,
nukushi 10, scanner 10, printa ndogo 11, kamera 10, kompyuta mpakato 23,
ipad 13 na hard disk 91. Balozi Youqing alisema mbali na misaada hiyo,
Serikali ya China iko katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa bandari ya
Bagamoyo pamoja na kuboresha reli ya Tazara.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment