Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaanza
mkutano wake wa 18 leo, ambao pamoja na mambo mengine, wabunge
wanatarajia kuhoji utekelezaji wa serikali wa maazimio nane ya Bunge
kuhusu kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni
300 kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Maazimio hayo yaliyopitishwa na Bunge Zima, Novemba 29, mwaka jana,
yalifuatia taarifa maalumu iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo
yaliyofanyika katika akaunti hiyo. Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Taarifa hiyo ya PAC, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Zitto
Kabwe, bungeni, Novemba 26, mwaka jana, ilieleza kuwa mmiliki wa kampuni
ya Pan African Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi,
mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering & Marketing (VIP), James
Rugemalira, walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha
kufanyika miamala haramu ya fedha katika akaunti hiyo kwenda kwa kampuni
hizo. Wengine waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa
hiyo, ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi,
Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo aliyetajwa na PAC kuwa dalali kati ya Rugemalira na Sethi
kufanikisha uchotwaji wa fedha hizo.
Wamo pia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco). Hivyo, Bunge likaazimia kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine
husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria kwa
mujibu wa sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC
kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti
hiyo na wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya PAC, vitendo vilivyofanywa na watu
hao vinaashiria makosa mbalimbali ya jinai, kama vile uzembe, wizi,
ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka,
rushwa na kupokea mali ya wizi. Hata hivyo, licha ya kutokuwapo yeyote kati ya waliotajwa
aliyekwishachukuliwa hatua, ambazo Bunge liliazimia, tayari Prof.
Muhongo na Jaji Werema walikwishajiuzulu nafasi zao serikalini, huku
Maswi akiendelea kuchunguzwa.
Maazimio mengine ya Bunge, ambayo hadi sasa bado hayajatekelezwa ni
pamoja na lile linalotaka mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutaifishwa na
lile linalotaka kuundwa kwa Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza
utovu wa maadili dhidi ya majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa
Eudes Ruhangisa na Aloysius Mujulizi. Majaji hao walitajwa katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Zitto
Kabwe, bungeni, Novemba 26, mwaka jana, kupata mgawo katika fedha
zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo.
Walitajwa kupewa mgawo wa fedha hizo na mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira. Katika taarifa hiyo ya PAC, Jaji Profesa Ruhangisa alitajwa kupata
mgawo wa Sh. milioni 404.25 na Jaji Mujulizi Sh. milioni 40.4 kutoka
katika fedha zilizochotwa katika akaunti hiyo.
Jaji Mkuu, Othman Chande, kupitia Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Ignas Kitusi, alikaririwa hivi karibuni akitaka aachiwe suala
la majaji hao, akisema atalishughulikia yeye mwenyewe. Akihutubia taifa kupitia wazee wa Dar es Salaam Desemba 22, mwaka
jana, Rais Kikwete, alisema amelipokea azimio dhidi ya majaji hao na
kulijadili na washauri wake. Hata hivyo, alisema itabidi wafuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa utaratibu huo, inatakiwa suala
kama hilo lianzie kwenye mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au
Bunge. Alisema Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde
Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua jaji yeyote pale inaporidhika kuwa
amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. “Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa,” alisema Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa PAC, fedha zinazodaiwa kuchotwa kutoka akaunti hiyo,
ni zaidi ya Sh. bilioni 300 wakati kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, ni
Sh. bilioni 202.9. Wengine waliotajwa kufaidika na mgawo wa fedha hizo, ni pamoja na
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna
Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6). Tayari Prof. Tibaijuka ameshatimuliwa kazi na Rais Kikwete kwa
kupokea fedha hizo kupitia akaunti yake binafsi iliyoko benki ya
Mkombozi, badala ya akaunti za shule na kwamba ni kinyume cha maadili.
Wengine waliopata mgawo kutoka katika fedha hizo, ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM),
Andrew Chenge (Sh. bilioni 1.6); Mbunge wa Sengerema (CCM), William
Ngeleja (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga Mjini (CCM),
Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4). Pia wamo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona
(Sh. milioni 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), Jaji Profesa
Ruhangisa (Sh. milioni 404.25) na Jaji Mujulizi (Sh. milioni 40.4)
pamoja na Mkurugenzi mstaafu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).
Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC),
Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8); Askofu Msaidizi wa
Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.9);
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigilwa (Sh. milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh.
milioni 40.4). Azimio lingine, ambalo bado halijatekelezwa, linataka Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco kuwajibishwa. Rais Kikwete akihutubia taifa kupitia wazee wa Dar es Salaam, alisema bodi hiyo tayari ilishamaliza muda wake.
Hata hivyo, kuna hoja, ambazo zimekuwa zikitolewa na watu wa kada
mbalimbali kwamba, bodi hiyo kumalizika muda wake, hakuzuii wajumbe wake
kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kuhusishwa katika kashfa ya
akaunti hiyo.
RATIBA YA MKUTANO WA BUNGE LA 18
Bunge jana lilitoa ratiba ya mkutano wake wa 18 unaoanza leo mjini
hapa, ambao pamoja na mambo mengine, litajadili taarifa za CAG
zilizowasilishwa katika mkutano wa 15. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bunge kupitia Afisa Habari
wake, Owen Mwandumbya, taarifa hizo za CAG zitajadiliwa kwa siku mbili
mfululizo, kuanzia kesho.
Taarifa hizo ni ya hesabu zilizokaguliwa za serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma. Mwandumbya alisema leo Bunge litaanza kwa kiapo cha utii cha
Mwanasheria Mkuu (AG), George Masaju, aliyeteuliwa na Rais Kikwete baada
ya Jaji Werema kujiuzulu nafasi hiyo. Alisema Ijumaa Bunge litajadili taarifa za kamati za kisekta na
zisizo za kisekta, ambazo ni Kamati ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini.
Jumamosi, taarifa za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji zitajadiliwa. Kamati hizo zitaendelea kujadiliwa Februari 2, 3 na 4 na kamati
zitakazojadiliwa ni pamoja na ya Katiba, Sheria na Utawala, ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Masuala ya Ukimwi. Nyingine ni Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara.
Katika mkutano huo wa Bunge, pia jumla ya miswada mitatu itasomwa na kupitishwa na wabunge. Miswada hiyo ni ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa
mwaka 2014, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014 na
Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013.
Kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, linatarajia kupokea taarifa ya
Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali
zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo, maji na uwekezaji ili
kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi. Katika Mkutano huo wa Bunge, maswali ya msingi 125 yanatarajiwa
kuulizwa pamoja na maswali 18 ya msingi yataulizwa papo kwa papo kwa
waziri mkuu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment