Social Icons

Pages

Friday, January 16, 2015

LAAC YABAINI UFISADI WA SH 1.7 BIL JIJI LA DSM

Meya wa Jiji, Dk Didas Masaburi 
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini ufisadi wa zaidi ya Sh1.7 bilioni katika Jiji la Dar es Salaam, hivyo kuitaka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kufuatilia kashfa hiyo na kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote waliohusika.
Mbali na hilo, LAAC imeikataa taarifa ya Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe kuhusu makusanyo ya fedha za maegesho ya magari kwa vile haiendani na uhalisia wa idadi ya magari yaliyopo jijini. Mwenyekiti wa LAAC, Rajabu Mbarouk wakati akikutana na watendaji wa jiji jana, alisema fedha hizo zimetumika kuendesha mradi hewa wa kujenga machinjio ya kisasa yenye dalili za kifisadi.
Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Omary Nundu alisema: “Inashangaza, mradi haujaanza lakini tayari meneja kapatikana na kalipwa fedha zote.” Aliongeza: “Tunataka kujua mchakato ulifanyikaje na nani aliyehusika, lakini kusema Sh1.7 bilioni mlichanga na zote zimetumika halafu tunaambiwa hoja hii ifungwe, itakuwa ngumu.” Akizungumzia mradi huo, Meya wa Jiji, Dk Didas Masaburi alisema: “Jambo hili tunalolizungumza lilitokea miaka 10 iliyopita, lakini kwa kuwa mmetuomba tukae basi tutazingatia maelekezo yenu.”
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Margreth Sitta alisema kamati hiyo imekutana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kuhakikishiwa kuwa Serikali itaanzisha Tume ya Ajira ya Walimu kuanzia Julai mwaka huu.
Alisema kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakilalamika kutokana na kusimamiwa na wizara zaidi ya moja, jambo ambalo limekuwa likileta usumbufu. Wakati huohuo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi amesema yuko tayari kuachia madaraka kama itabainika kuwa asilimia 21 ya hisa za jiji hilo zilihamishwa kwenda Kampuni ya Simons Group inayoendesha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Alitoa kauli hiyo jana baada ya mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kangi Lugola kudai ana vielelezo kamili vya mauziano hayo vilivyopo Mamlaka ya Usajili wa Biashara (BRELA).
“Suala hili limenilazimu kwenda BRELA kujua uhalali wake. Nimekuta taarifa zikionyesha hisa zimehamishwa kutoka jiji kwenda Simons Group,” alisema. “Kama kuna ukweli kwenye madai hayo ya Kangi niko tayari kujiuzulu. Nitakuwa wa kwanza kuwajibika.” Awali, mjumbe wa kamati hiyo, Munde Tambwe alisema mikataba kati ya kampuni hiyo na jiji una utata, huku akifafanua kuwa Simons Group inaitumia Kampuni ya Uda bila kulipa chochote. Mjumbe wa kamati hiyo, Israel Natse alisema tangu LAAC ianze kufanya ziara Dar es Salaam, wamegundua kuwapo ujanja mwingi.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: