Watuhumiwa wa kesi ya kupokea rushwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta
Escrwo, Rugonzibwa Mujunangoma (kushoto) na Theophil Bakwea na
wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa ajili ya kufunguliwa
mashitaka.
Miezi michache
baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi, watumishi
wawili waandamizi wa Serikali wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakituhumiwa kupokea rushwa ya mamilioni ya
fedha zilizotoka kwenye akaunti hiyo.
Mahakama hiyo ilielezwa jana kuwa Mkurugenzi wa
Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti
yake namba 00120102602001.
Kadhalika, Mahakama ilielezwa kuwa Februari 12,
2014, Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati
na Madini, Theophillo Bwakea alipokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia
akaunti yake namba 004101102643901. “Upelelezi wa kesi umekamilika naomba mahakama
izuie akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea fedha hizo za escrow na
kesi ipangwe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali,” alisema Leonard
Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru).
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 11 ya
mwaka 2015 inayomkabili Mujunangoma, Swai alidai mshtakiwa huyo alifanya
kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kupambana na
Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007. Swai alidai kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya
Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, Mujunangoma akiwa
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard
Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na
mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa
kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mujunangoma alikana
na mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa kwa mujibu wa
kifungu cha 15 cha sheria anachoshtakiwa nacho, mshtakiwa huyo hahitaji
kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Hakimu Emilius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo
kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi ya Serikali na
kwamba kila mdhamini asaini hati ya maneno ya Sh10 milioni. Pia, Hakimu Mchauru alimtaka mdhamini ama
mshtakiwa mwenyewe, kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha taslimu
anazodaiwa kuzichukua kama rushwa, ama kuwasilisha hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa masharti hayo,
mshtakiwa alipata wadhamini wawili wanaoaminika , kutoa hati mbili za
mali isiyohamishika ambazo alidai zina zaidi ya thamani ya fedha iliyomo
ndani ya hati ya mashtaka. Kuhusu kuzuia akaunti ya mshtakiwa, Hakimu Mchauru
aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha maombi mahakamani hapo na
kuyaambatanisha na hati ya kiapo itakayounga mkono maombi hayo.
Kwa upande wa Bwakea, aliyefunguliwa kesi namba 12
ya 2015, Swai alidai kuwa siku hiyo ya tukio katika benki ya Mkombozi
alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake.
CHANZO: MWANANCHI
Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha
kama zawadi kwa kushiriki kama mjumbe aliyeandaa sera iliyoruhusu sekta
binafsi kuzalisha na kuuza umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco). Baada ya kusomewa shtaka hilo, Bwakea alikana na
upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na akaomba
kesi hiyo ipangiwe tarehe ya kusomwa kwa maelezo ya awali.
Hata hivyo, Swai aliiomba mahakama hiyo izuie
akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea kiasi hicho cha fedha na
mahakama iliridhia na kutoa amri ya kuizuia mtu yeyote kutoa ama
kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti hiyo. Hakimu Moshi alimtaka mshtakiwa (Bwakea) kuwa na
wadhamini wawili, watumishi wa Serikali ambao kila mdhamini asaini hati
ya maneno ya Sh25 milioni.
Pia, washtakiwa hao wasitoke nje ya Jiji la Dar es
Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama. Hata hivyo, mshtakiwa
(Bwakea) alikamilisha masharti hayo na kuachiwa huru kwa dhamana na kesi
hiyom imeahirishwa hadi Januari 29, 2015. Kashfa hiyo ya Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyoibuliwa na Bunge iliitikisa nchi na hadi sasa imesababisha
kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka
akaunti hiyo.
Pia, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Jaji Frederick Werema alijiuzulu baada ya azimio la Bunge kutaka
awajibishwe na mamlaka yake ya uteuzi akidaiwa kuishauri vibaya Serikali
katika suala hilo.
Pia, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi amesimamishwa kazi kwa uchunguzi. Katika uamuzi wake, Bunge liliagiza watuhumiwa
wote wa kashfa hiyo, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, ambaye bado ameachwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete na
wenyeviti wa kamati za Bunge za kisekta wawajibishwe.
Hao ni pamoja na Andrew Chenge anayeongoza Kamati ya Bunge ya Bajeti aliyedaiwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka akaunti hiyo. Pia, William Ngeleja (Kamati ya Sheria na Katiba)
aliyepokea fedha, Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), ambaye pia
alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco. Hali kadhalika, tayari watumishi kadhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesimamishwa kutokana na kashfa hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment