Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Wafanyabiashara wa Soko Kuu Kariakoo mtaa wa Kongo,
jijini Dar es Salaam, jana walifunga maduka yao na kuandamana hadi
katika Kituo cha Polisi Kati, wakishinikiza kuachiwa kwa Mwemyeti wao,
Johnson Minja.
Minja alikamatwa juzi na Jeshi hilo na kusafirishwa kupelekwa mjini
Dodoma kujibu mashitaka yanayomkabili ya kuhamasisha wafanyabiashara wa
mkoa huo wagome kufungua maduka kupinga matumizi ya mshine za
kielektroniki (EFDs). Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Simon Sirro, alithibitisha kukamatwa kwa Mwenyekiti huyo kwa
kosa la kuhamasisha wafanyabishara wa mkoani Dodoma wagome.
Sirro alisema Minja alikamatwa na polisi jijini Dar es Salaam,
lakini kesi yake ipo mjini Dodoma na baada ya kumkamata alipelekwa
mkoani humo ilikujibu tuhuma hizo. Aidha, Sirro alisema walikasirishwa
na wafanyabiashara hao kufanya maandamano kumfuata Minja kituo cha
polisi. “Anayeweza kuzungumza vizuri kuhusiana na swala hilo ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma,” alisema Sirro.
Wakizungumza na NIPASHE wafanyabishara hao walisema kuwa hawatafungua maduka yao hadi hapo Mwenyekiti wao atakapoachiwa huru. Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jafari Mauya, alisema hawatafungua
maduka yao kwani hawafahamu sababu ya kukamatwa kwa Minja. Hata hivyo,
baadhi ya maduka yalifunguliwa majira ya mchana baada ya maandamano.
Walipoulizwa sababu za kufungua maduka yao licha ya kukubaliana
kuyafunga, walisema waliofungua ni miongoni mwa wafanyabishara wachache
ambao hawajajiunga na chama cha wafanyabishara Kariakoo. Msemaji wa wafanyabiashara, Stephen Chamle, alisema wao watafunga safari kwenda Dodoma kumuona Minja. “Tangu jana (juzi) tulikuwa tunamtafuta Minja, lakini hakupatikana,
leo (jana), wamemtafuta kwa njia ya simu yake ya mkononi na kuwapa
taarifa kuwa yuko Dodoma,” alisema Chamle.
Awali, wafanyabishara hao walikusanyika na kuteua wawakilishi ambao
walikwenda kuzungumza na Jeshi la Polisi na kukubaliana kuwa warudi ili
wakafungue maduka. Katibu wa wafanyabishara hao, Christopher Kionda, alisema
walikubaliana kuwa wengine wakafungue maduka na wengine waende Dodoma
kumuona Mwenyekiti wao. “Leo (jana) tunaondoka kwenda Dodoma kumuona Mwenyekiti wetu, wengine wataendelea tu na biashara,” alisema Kionda.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, kwa
njia yasimu alijibu kuwa alikuwa katika kikao na kuelekeza atafutwe
baadaye ingawa hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni. Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Malaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema alisikia taarifa hizo za
kufunga maduka na kuwa wanazifuatilia.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment