Wajumbe wa kamati tatu za Kudumu
za Bunge ambazo wenyeviti wake wanatakiwa kuvuliwa nyadhifa zao kutokana
na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ‘wanasuasua’
kuwaondoa na kuchagua viongozi wengine.
Kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati hizo ambazo
ni Bajeti, Nishati na Madini na Katiba, Sheria na Utawala wamekuwa
wakishangazwa na hatua za wahusika hao kuendelea kujitambulisha kuwa ni
wenyeviti, sambamba na kuongoza vikao vya kamati hizo, wakati wakijua
wazi kuwa hawatakiwi kufanya hivyo.
Wenyeviti wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba) na
Andrew Chenge (Bajeti).
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah aliliambia
gazeti hili jana kwamba jukumu la kuwaondoa wenyeviti hao lipo mikononi
mwa wajumbe wa kamati hizo, kwamba kama wakishindwa Spika wa Bunge
atachukua jukumu hilo. Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge liliazimia
kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow
wakiwepo viongozi wa Kamati hizo tatu, wachukuliwe hatua za haraka na
Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge
unaotarajiwa kuanza Januari 27 mwaka huu. Akinukuu azimio hilo Kashilillah alisema, “Wajumbe
husika ndiyo wanaotakiwa kuwaondoa wenyeviti hao, hilo ni lazima
mlitambue jamani. Waulizeni ni lini watafanya hivyo.”
Alisema ndiyo maana kamati ikiwa haina mwenyekiti,
wajumbe wenyewe huchagua mmoja kati yao kwa ajili ya kuongoza kikao cha
kamati. “Spika hawezi kumwondoa mwenyekiti wa kamati
husika, anachoweza kufanya Spika ni kumhamisha mwenyekiti kutoka kamati
moja kwenda nyingine. Akifanya hivyo maana yake ni kwamba mwenyekiti
husika anapoteza sifa za kuwa mwenyekiti,” alisema.
Alisema jambo hilo Spika Makinda anaweza kulifanya
kama wajumbe wa kamati hizo tatu zitashindwa kuchagua wenyeviti
wengine. Kuhusu Chenge ambaye aliteuliwa na Spika Makinda kuwa
mwenyekiti wa kamati ya Bajeti alisema, “Chenge aliteuliwa katika
kipindi cha mpito ambacho kikiisha atachaguliwa mwenyekiti mwingine.
Hivyo naye anaweza kuondolewa tu na wajumbe wa kamati.”
Mvutano katika kamati
Taarifa kutoka ndani ya kamati ya Bajeti zilieleza
gazeti hili kwamba, juzi kamati hiyo ilikutana na Wizara ya Maji na
Uchukuzi na Chenge alijitambulisha kama mwenyekiti, jambo ambalo
liliwashangaza wajumbe wa kamati hiyo. “Tumeshangazwa jinsi alivyojitambulisha kwa sababu
awali kamati tulikubaliana kuwa akae pembeni na kumwachia Makamu
mwenyekiti, Dk Limbu (Festus) kuongoza vikao vya kamati. Inavyoonekana
ni kama anang’ang’ania nafasi hii,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati
hiyo.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo alisema, “Ilitushangaza kwa
sababu Dk Limbu alikuwapo na kamati ndiyo iliamua kuwa yeye awe
mwenyekiti wetu kwa muda. Hili jambo linatuchanganya na ni vyema
likapatiwa ufumbuzi.” Alisema wajumbe wa kamati wanashindwa kuchukua
hatua zaidi kwa sababu Chenge aliteuliwa kushika nafasi hiyo na Spika wa
Bunge, Anne Makinda na kwamba yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumwondoa.
Mapema wiki hii, Dk Limbu alikaririwa na gazeti
hili akisema, “Suala la Chenge linasubiri uamuzi utakaotolewa na Spika
wa Bunge, Anne Makinda. “Kamati imeamua kwa busara Chenge akae pembeni na
makamu mwenyekiti aongoze vikao huku ikisubiri hatua atakazozichukua
Spika (Makinda),”
Kwa upande wake Ngeleja aliliambia gazeti hili
kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa uchunguzi wa
suala hilo bado unaendelea, ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi
ambao alidai yupo tayari kuutekeleza. Akizungumzia sakata hilo Makamu Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Gosbert Blandes alisema kuwa wamekwama kutekeleza maagizo
ya Bunge ya kumwondoa kwenye madaraka Ngeleja, baada ya kukosa mwongozo
ndani ya kanuni. “Kamati ilijadili kwa kina suala hilo kwamba ni
vipi tunaweza kulishughulikia, tulipata utata mkubwa sana hatujaona
kanuni ambayo tunaweza kuitumia, hivyo Ngeleja anaendelea kuongoza vikao
kihalali,” alisema Blandes.
Alisema bado hawajapokea mwongozo wowote kutoka
kwa spika, hivyo wanaendelea kusubiri huku wakijadiliana kwa amani
tofauti na inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kwa uapnde wake Mwambalaswa alisema, “Kamati haina
jukumu hilo ambalo Katibu (Kashilillah) amekueleza, ila kama amekueleza
hivyo sawa tu.”
Wabunge walia na Profesa Muhongo
Katika hatua nyingine wabunge walikosoa kitendo
cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuendelea na
kazi licha ya maazimo ya Bunge kuitaka mamlaka ya uteuzi kumwajibisha.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema,
“Profesa Muhongo anaweza kuwa anafaa kufanya kazi nyingine lakini si hii
na naomba ieleweke kwamba maazimio yale si ya Bunge bali ni ya wananchi
hivyo lazima yakatekelezwa.” Aliongeza: “Lakini atafanya kazi na nani (Muhongo)? Bajeti yake ataipitisha nani? Tutamwachia hatutampa ushirikiano.”
Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya PAC alisema, “Profesa Muhongo anamwaibisha Rais (Jakaya Kikwete) na
anampa wakati mgumu sana.” Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Esther Matiko
alisema, “Rais Kikwete alishasema kuwa fedha za IPTL siyo za Umma hivyo
kwa kauli yake hii ni dhahiri hatachukua uamuzi wa utekelezaji wa
maazimio ya Bunge.” “Ila cha kushangaza na kuona jinsi hawa CCM
wanacheza na akili za Watanzania, Swali la msingi fedha si za Umma kwa
nini wanatumia fedha za umma kushughulikia masuala binafsi,” alisema
Matiko.
Aliongeza: “Rais Kikwete kwa kofia ya Mwenyekiti
wa CCM wakiwa katika kikao cha Kamati Kuu yao huko Zanzibar wamebariki
utekelezaji wa maazimio ya Bunge...upande mmoja Rais Kikwete anakana si
fedha za umma upande mwingine anakubari maazimio ya Bunge hii
inawachanganya Watanzania na wasijue msimamo wa Rais Kikwete ni upi.” Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msingwa alisema, “Kutochukua uamuzi ni udhaifu wa taasisi ya Rais na ni
ombwe la uongozi...ndiyo maana ana sita sita kuchukua uamuzi.” Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Agripina
Buyogela alisema, “Ukimya wa Rais unatupa mtihani ina maana hakuna mtu
mwingine anayeweza kuwa Waziri wa Nishati na Madini mpaka ang’ang’aniwe
Profesa Muhongo.”
Mbunge wa Mgogoni (CUF), Kombo Khamis Kombo
alisema, “Ni jambo la dharau kwa wabunge na wananchi. Haiwezekani
yatolewe maazimio lakini hayatekelezwi. Huyo Muhongo atachunguzwa vipi
wakati bado anaendelea na wadhifa wake wa uwaziri.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment