
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba.
Wagombea wa nafasi ya urais nchini, wametakiwa
kupima afya zao kisha matokeo ya afya zao kutangazwa hadharani, ili umma
wa Watanzania uwafahamu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Upimaji huo wa wagombea hao na wagombea wenza, umetajwa kuweza
kulipunguzia Taifa gharama kubwa za matibabu nje ya nchi kwa viongozi
hao wakishakuwa madarakani. Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa
Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, wakati akizungumza na
waandishi na kutoa taarifa kuhusu masuala ya Katiba na uchaguzi wa
marudio wa Rais nchini Zambia, uliofanyika Januari 20, mwaka huu.
Alisema, kutokana na uzoefu walioupata wakati wa uchaguzi nchini
humo, serikali ya Zambia ilimpa kazi wakala wa kupima afya za wagombea
urais 11 waliokuwa wanawania kiti cha urais. Kauli hiyo imekuja wakati tayari baadhi wa wanaoiwania nafasi hiyo,
hususan ndani ya Chama tawala (CCM) kuonyesha wazi nia ya kuwania
urais.
“Mapendekezo yetu ni hayo wagombea wapimwe afya zao, wapo ambao
tayari wagonjwa, lakini wanataka kuongoza nchi. Ingawaje nchini
hatujawahi kukumbwa na kiongozi kufariki akiwa madarakani, lakini Zambia
wameutumia utaratibu huu wa kupima afya za wagombea kabla, kwani wao
wamewapoteza marais wawili wakiwa mamlakani,” alisema. Mwaka Agosti
2008 alifariki rais aliyekuwa madarakani, Levy Mwanawasa na kufanya
uchaguzi uliompa ushindi, Rupiah Banda.
Pia Oktoba mwaka jana, aliyekuwa Rais Michael Satta alifariki dunia. Mwaka 2001, wakati Benjamin Mkapa akiwa Rais katika serikali ya
awamu ya tatu, Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma, alifariki dunia
ghafla jijini Dar es Salaam. Hata hivyo Jukata ilipendekeza kuwa uchaguzi mkuu kufanyika
katikati ya wiki badala ya Jumapili, ili kuongeza idadi ya wapigaji
kura.
Alisema uchaguzi ufanyike siku za Jumatatu hadi Alhamisi badala ya
siku za Ijumaa, Jumamosi wala Jumapili kwani siku hizo ni za ibada za
waumini wa dini tofauti.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment