
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, Dk. Michael
Kadeghe, anadaiwa kuanza ‘kucheza rafu’ za uchaguzi mkuu ujao kwa
kutishia harakati za Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango
Malecela, kutetea kiti chake jimboni humo.
Hofu hiyo, ambayo imeibuliwa na Kilango mwenyewe, inadaiwa kuwa
inatokana na Kadeghe kuamua kupeperusha bendera ya taifa kwenye gari
lake jimboni humo na kuendesha vikao vya ndani vya siri vya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kutaka kumng’oa Kilango ubunge. Mtafaruku mkubwa ulizuka juzi mchana katika Kijiji cha Mamba-Miamba
jimboni humo, baada ya Kilango akiwa na baadhi ya madiwani wakikagua
barabara zilizokuwa zinajengwa kwa msaada wa Rais Jakaya Kikwete,
kukutana ana kwa ana gari la mkuu huyo wa wilaya, likiwa limeegeshwa nje
ya mgahawa wa mamalishe likipeperusha bendera hiyo.
Ghafla, Kilango alisimamisha gari lake aina ya Toyota Land Cruiser
na kushuka na kuanza kuhoji mbele ya umati wa wananchi kwamba, Kadeghe
aliyekuwa akitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za
usajili STK 3764, amepata wapi uhalali wa kupeperusha bendera ya taifa
kwenye eneo lenye mkuu wa wilaya mwingine na wakati huo huo akifanya
vikao vya siri vya kugombea ubunge. “Huyu Kadeghe, nimemshinda kwenye mbio za ubunge mara mbili, hivi
ananitaka nini? Anawatisha wananchi kwa kupeperusha bendera kwenye
wilaya, ambayo haiongozi. Au ndiyo anafakiri inaweza kuwa kete ya
kuwarubuni wapigakura? Mara kadhaa anafanya vikao vya siri hapa jimboni,
leo kanasa kwenye mtego…Ngoja nimpigie mkuu wa mkoa (Gama), DC Kapufi
na Mwenyekiti wa CCM Same ili niwaeleze faulo unazozicheza ,” aling’aka
Kilango.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Kilango alimshinda Dk. Kadeghe
kwa kura 389 dhidi ya kura 46 alizoambulia kwenye uchaguzi wa ndani wa
CCM na mwaka 2010, Kilango pia alimpiga mwereka mpinzani wake huyo
kwenye kura za maoni kwa kupata kura 7,900 dhidi ya kura 2,200 alizoambulia Kadeghe. Wakati Kilango akikwaruzana kwa maneno na dereva wake (Dk.
Kadeghe), Dk. Kadeghe alijitokeza na baadaye alipoona Kilango amekuwa
mkali, alikimbilia ndani ya mgahawa kunakodaiwa ndiko alikokuwa akifanya
kikao cha faragha na wapambe wake.
Hata hivyo, dereva huyo alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini
hakumshauri bosi wake asipeperushe bendera jimboni humo kwa kuwa siyo
eneo lake la utawala, alijibu kwamba, yeye siyo msemaji wake na kwamba,
anayetakiwa kuhojiwa kwa kosa hilo ni mkuu wa wilaya hiyo. Dk. Kadeghe alisema hakuwa na habari kama gari lake linapeperusha
bendera kimakosa, lakini pia alikuwa anabadilishana mawazo na jamaa zake
na wala hakuwa anafanya vikao vya kichama kwa ajili ya kuendesha
kampeni ya kung’oa kwenye ubunge Kilango.
“Siyo kwamba namtisha mheshimiwa mbunge. Mimi nimekuja likizo
jamani na wala sifanyi vikao vya kampeni kama inavyoelezwa. Halafu sina
habari kabisa kwamba, bendera inapepea. Ngoja nizungumze na dereva kwa
nini aliifunga bendera au inawezekana alikuwa anafanya usafi,”
alijitetea Dk. Kadeghe. Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, alisema taratibu zipo wazi
kabisa kwamba, mkuu wa wilaya akishavuka nje ya mipaka yake ya utawala
kwa mujibu wa madaraka ya ukuu wa wilaya chini ya sheria ya Tawala za
Mikoa namba 19 ya mwaka 1977 na Sheria ya Serikali za Mitaa namba 7 na 8
za mwaka 1982, Dk. Kadeghe amepotoka kupeperusha bendera kwenye wilaya,
ambayo siyo yake.
“Nina uhakika DC Kadeghe anaijua mipaka yake. Nimezipata taarifa na
ninataka nimhoji kama anaelewa au anafanya makusudi. Lakini kama
haelewi nitamrekebisha. Kwa kawaida niliyonayo mimi nikiendaga kwetu
Wilaya ya Nkasi, Rukwa nikifika tu, nakwenda kuripoti CCM, Ofisi ya Mkuu
wa Usalama wa Taifa wa Wilaya na hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa kwa sababu unaweza ukadharau halafu ukapata matatizo hawajui na
mambo yenyewe ndo kama haya,” alisisitiza Kapufi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment