Katuni
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametabiri kukwama kwa kura ya maoni kuhusu
Katiba pendekezwa, akieleza kuwa maandalizi hafifu ambayo yamefanyika
hadi sasa hayaruhusu zoezi hilo kufanyika.
Aidha, amesema iwapo kutatokea ujanja ujanja wowote wa kutaka kukiuka sheria ya kura ya maoni, nchi itaingia kwenye matatizo.
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE jana, Jaji Warioba alisema wiki
iliyopita, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walikutana
na majadiliano yao yalijikita kwenye maandalizi ya kura ya maoni kuhusu
Katiba pendekezwa.
Alisema sheria namba tatu ya mwaka 2014, ambayo inahusu kura ya maoni
inaeleza kuwa jambo la kwanza kufanyika ni uboreshaji wa daftari la
wapigakura, ambalo utafuatiwa na elimu kwa umma kwa miezi miwili kisha
kampeni kwa mwezi mmoja.
“Tukaona kuna umuhimu wa kufanya maandalizi kwa umakini mkubwa kabisa,
tumeichambua sheria hii ya kura ya maoni, tumeona mahitaji ya sheria hii
lakini utaratibu wa sheria hauanzi mpaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), imeanza aundikishaji wa wapigakura,” alisema.
ELIMU KWA UMMA
Akizungumzia msingi wa elimu kwa umma, Jaji Warioba alisema NEC inapaswa
kufanyakazi hiyo kwa kushirikiana na asasi za kiraia kwa kipindi
kisichopungua miezi miwili ili kuwaelimisha wananchi nini kilichopo
ndani ya Katiba na utaratibu wa kura ya maoni.
“Kwa hiyo tuna miezi mitatu, ratiba iliyowekwa na serikali inasema
wanakamilisha kuandikisha Machi kisha kampeni inaanza mara moja. Kipindi
cha elimu hakikuwekwa kwenye ratiba. Mimi nafikiri ni vizuri kufuata
sheria kwa sababu tukiendesha hii kinyume cha sheria inaweza kuleta
matatizo,” alisema.
Jaji Warioba aliongeza kuwa: “Na kama tukifuata sheria inavyosema, ni
kwamba NEC ikimaliza kazi Machi; Aprili na Mei itakuwa ni elimu, Juni ni
kampeni kwa hiyo kura ya maoni itakuwa ni Julai.” Hata hivyo, alisema kura hiyo kufanyika Julai ni matatizo kwa sababu ni
wakati ambao maandalizi ya uchaguzi mkuu yatakuwa yameanza na itakuwa
kipindi vyama vya siasa vinakuwa vinateua wagombea wake. “Ukafanye yote kwa pamoja inaweza kuleta matatizo lakini muhimu
tunalosema tuifuate sheria kuwepo na kipindi cha elimu kwa umma.”
KAMPENI
Alisema sheria hiyo inataka baada ya elimu kwa umma, ziundwe Kamati
mbili katika ngazi ya Taifa na ngazi ya jimbo, zitakazoendesha kampeni
kwa mwezi mmoja, huku moja ikiunga mkono Katiba pendekezwa na nyingine
ikiipinga.
“Kamati ya moja itakuwa inawaambia wananachi wapige kura ya ndiyo na
kamati ya pili itakuwa inawaambia waikatae wapige kura ya hapana,”
alisema.
Alisema kamati zote hizo zitatakiwa kuwa na viongozi wanajulikana na
ijulikane mapato ya kampeni yatatoka wapi na wananchi wajue kampeni
zitakavyoendeshwa.
“Hizi kamati hazijaundwa na ni lazima ziundwe na ziandikishwe kwenye tume ya uchaguzi,” alisema.
Jaji Warioba alisema maandalizi hayo hayajafanyika na haijulikani itafanyika lini na kwa namna gani.
UBORESHAJI WA DAFTARI
Alisema NEC inatumia utaratibu wa kuandikisha wapigakura kwa njia ya
kielektroniki (BVR), ambao alisema ni mzuri na unaoweza kuzuia
udanganyifu.
Alisema utaratibu wa BVR unafuta wapigakura wadanganyifu ambao wamekuwa
wakijiandikisha zaidi ya mara moja, lakini NEC italazimika kufanya
uhakiki baada ya kumaliza kuandikisha wapigakura.
Alisema uandikishaji huo ulitumika Malawi mwaka 2004, lakini uliibua
malalamiko kwa kuwa wakati wa uandikishaji serikali ya nchi hiyo
haikupata muda wa kuhakiki taarifa za wapigakura.
Alisema mfumo wa BVR unafuta majina ya wapigakura watakaojiandikisha
zaidi ya mara moja na kubakisha jina kwenye kituo atakachokuwa
amejiandikisha mara ya kwanza, hivyo ili kuepuka malalamiko hayo hata
hapa nchini ni vyema uhakiki ukafanyika. “Ukitumia utaratibu huu, ukimaliza unatakiwa uhakiki, bandika vituoni
kila mtu aone. Ambaye hataona jina lake mfumo huo utamwonyesha jina lake
lilipo,” alisema.
Alisema zoezi la uandikishaji unaofanywa sasa na NEC linawahusisha pia
vijana watakaoshiriki uchaguzi mkuu ambao ifikapo Oktoba watakuwa
wametimiza miaka 18.
“Ukiwaandikisha sasa hivi, wakijakupiga kura ya maoni watakuwa
hawajafikisha miaka 18, usipowaandikisha sasa hivi, ikifika Oktoba
hawatakuwa na haki ya kupigakura, tukaona hilo tatizo kwa hiyo tunaona
maandalizi yafanywe,” alisema.
Alisema bila kufanya maandalizi, kunaweza kuwa na wapigakura wasio na sifa au wanaweza wakakwama kushiriki uchaguzi mkuu.
Serikali imepanga kura ya maoni kufanyika Aprili mwaka huu, ingawa
makundi mbalimbali ya jamii yanaeleza wasiwasi kwamba kutokana na
maandalizi hafifu, uwezekano wa kufanyika kwa kura hiyo ni mdogo.
Baadhi ya mambo yanayohojiwa ni kutosambazwa kwa nakala za Katiba
inayopendekezwa kwenda kwa wananchi ili waisome na kuielewa Katiba
inayopendekezwa kabla ya kuipigia kura kuikubali au kuikataa.
WANANCHI VUNJO
Alisema kuhusu wananchi wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro ambao wamemchangia
ili akawape elimu ya Katiba, alisema wajumbe wa iliyokuwa tume yake
wataendelea kutoa elimu kwa kutumia rasilimali na uwezo usio na mashaka
na usioegemea upande wowote.
“Sisi tunafanya, lakini moja ambalo tuko makini kabisa hatutaki
kuonekana tunaungana na kundi lolote. Tunasema tukiwa na uwezo
tutaendelea kutoa elimu lakini uwezo ule ni uwezo ambao hauna mashaka,
hatutaki kuonekana tunajiunga na kundi lolote,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment