
Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF, Christine Lagarde amesema
kushuka kwa bei za mafuta na kuimarika kwa uchumi wa Marekani
havitatosha kuboresha mwelekeo wa uchumi wa dunia mwaka huu wa 2015.
Lagarde alisema wakati mafuta ya bei nafuu yatasaidia watumiaji katika
sehemu nyingi za dunia, Marekani ndiyo itakayo kuwa nchi pekee yenye
uchumi mkubwa itakayoepukana na udhaifu katika sekta ya uwekezaji na
ununuzi. Katika hotuba inayoangazia ripoti ya IMF kuhusu matarajio ya uchumi wa
dunia, inayotarajiwa kutolewa wiki ijayo, Lagarde alisema kanda
inayotumia sarafu ya euro na Japan zingali katika hatari ya kutwama
katika kipindi cha muda mrefu cha ukuaji dhaifu na mfumko hatari wa bei.
Hatari ya kupungua ukuaji wa uchumi
Kitisho cha kupunguza fedha kwenye mzunguko, kushuka kwa bei za bidhaa
na viwango vya mishahara, vinaendelea kuwa hatari kwa bara la Ulaya,
Lagarde aliliambia baraza ya Uhusiano wa nje la Marekani. Wakati huo huo
IMF imesema kuna uwezekano wa kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi
katika mataifa yanayoinukia, yakiongozwa na China. "Maswali ya wazi tuliyonayo wakati huu ni je, kushuka kwa bei za mafuta
na uchumi imara nchini Marekani vitupe matumaini kuhusu uchumi wa dunia?
Jibu ni hapana, hapana, hapana, kwa nini? Kwa sababu kuna masuala
chungu mzima, athari za mgogoro wa kiuchumi ambazo bado tunazo, na
ambazo zinadhofisha uchumi wetu," alisema Lagarde katika hotuba yake kwa
baraza la masuala ya kigeni la Marekani.
Alisema kupungua kwa bei za mafuta ni jambo zuri sana kwa uchumi wa
dunia, lakini uchumi huo uko katika hali mbaya sana, na hilo
halitasaidia. Alisema kupungua kwa bei ya mafuta kunasaidia kupandisha
uwezo wa wananchi kununua bidhaa, kunaongeza mahitaji binafsi ya mafuta
katika mataifa yanayonunua kutoka nje, na kutegemea ni kwa muda gani bei
zitaendelea kuwa chini, hili linaweza kutoa mchango katika ukuaji wa
uchimi wa dunia kwa muda. Kuimarika kwa uchumi wa Marekani pia kunaelekea kuwa maumivu kwa baadhi
ya mataifa. Wakati data za Marekani kutoka Desemba zimewasukuma
wawekezaji kuamini kuwa benki kuu ya nchi hiyo itasubiri pengine hadi
mwezi Oktoba kupandisha viwango vya riba, Lagarde alisema kukazwa kwa
sera ya fedha kunakotarajiwa kunaweza kuvuruga masoko ya fedha, hasa
katika mataifa masikini zaidi ambako mabenki na makampuni yamekopa dola
zaidi katika miaka ya karibuni.
Rais wa Benki Kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi, amesema benki hiyo
imeyaanda masoko ya fedha kwa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha ili
kukabiliana na kuongezeka kwa fedha katika mzunguko.
Bei za mafuta kushuka zaidi
Kushuka kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine tayari kumeziweka katika
shinikizo Nigeria, Urusi na Venezuela, alisema Lagarde. Mafuta ghafi
yamepoteza karibu asilimia 60 ya thamani yake tangu mwezi Juni, na
wachambuzi wanasema bei za mafuta zitaendelea kushuka angalau kwa
kipindi chote cha nusu ya kwanza ya mwaka huu. Matamshi ya Lagarde yalikuja wakati benki kuu ya Ulaya ECB, ikiyaanda
masoko ya fedha kwa jaili ya mpango wa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha
ili kukabiliana na hatari ya kuongezeka kwa fedha kwenye mzunguko. Siku
ya Jumatano, rais wa ECB Mario Draghi alisema benki hiyo ilikuwa na
njia chache mbadala kwa mpango huo.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment