Kwa hesabu za haraka haraka, urefu wa mita 829.8 (sawa na futi 2,722) ni sawa sawa na viwanja vinane vya mpira wa miguu.
Uwanja wa mpira wa miguu uliotimia vizuri, una
urefu wa mita 100, sasa vipangwe kwa mfuatano viwanja vinane halafu
ongeza mita 29.8, ni kama mita 30 ndipo unapata urefu wa jengo la Burj
Khalifa. Ni jengo refu kuliko yote duniani kwa sasa. Burj Khalifa lilijengwa katika eneo la ekari tatu
kama kivutio cha mji wa Dubai, lakini ikiwa na matumizi mbalimbali
ikiwamo makazi ya watu 30,000, hoteli kubwa tisa, maduka makubwa
yanayojulikana kwa jina la Dubai Mall, pamoja na eneo la ekari 12
lililojengwa bwawa linaloitwa ziwa la Burj Khalifa. Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Omar Rajab Mjenga
alisema katika mahojiano mafupi kuwa Dubai hawana mafuta wala mbuga za
wanyama, kinachofanyika ni kuwekeza kwenye majengo yanayovutia. Anasema kuwa kinachofanyika Dubai ni amri, kwamba
Mfalme wa Dubai akisema kitu kifanyike, kinafanyika na hakuna mjadala,
lengo likiwa tayari limeshapangwa. Mtawala alisema mbadala wa mafuta Dubai ni kuwa na kivutio cha utalii. Balozi Mjenga anasema majengo marefu, mpangilio wa
mji ni kivutio pekee cha utalii na sehemu kubwa ni fedha za wananchi
zinazotoka mifukoni mwao. “Wamefanikiwa na watu wengi wanakuja kupumzika Dubai na kufanya ununuzi,” anasema. Naye dereva teksi, mkazi wa eneo hilo, Markiz
Hamooud anasema kuwa imesaidia kuitambulisha Dubai kimataifa kuwa ni
nchi pekee duniani yenye jengo refu. Anasema kuwa katika jengo hilo, haijawahi kutokea
kukatika umeme na kwamba ikitokea watu wengi watakufa kwa kuwa sehemu
kubwa wanategemea nishati hiyo.
Uamuzi wa kujenga Burj Khalifa
Uamuzi wa ujenzi wa jengo hilo refu ni wa serikali
kwamba kwa kuwa Dubai haina mafuta, basi chanzo mbadala cha kuliingizia
taifa mapato ni kutengeneza kitu cha tofauti ili kuwa kivutio cha
watalii na ni jengo la Burj Khalifa. Inaelezwa kuwa Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al
Maktoum alitaka Dubai kuwa katika rekodi ya dunia kuwa ina kitu cha
pekee na amefanikiwa. Kinachofurahisha katika jengo hilo ni kwamba, lina
madirisha 24,348 ya vioo na vyuma na inachukua wiki nane kusafisha
jengo zima.
Ujenzi wake Burj Khalifa
Majengo marefu duniani
Kuna majengo mengi marefu duniani, katika nchi mbalimbali, lakini hakuna linalofikia Burj Khalifa. Jengo la Shanghai Tower lililopo China lina urefu
wa mita 632 ambalo ni fupi kwa mita 200 za Burj Khalifa wakati jengo la
tatu kwa urefu duniani ni Makkah Clock Royal Tower lililoko Saudi
Arabia. Lina urefu wa mita 601.
World Trade Center lililoko kwenye mji wa New York
Marekani lina urefu wa mita 541 ikiwa ni jengo jipya baada ya lile la
awali lililoshambuliwa na magaidi Septemba 11, 2001. Jengo la tano kwa urefu duniani ni CTF Finance
Centre, lililoko Guangzhou, ambalo linaendelea kujengwa na hadi
litakapokamilika mwaka 2016, litakuwa na urefu wa mita 530.
Ujenzi wake Burj Khalifa
Kazi ya kuchimba msingi wa Burj Khalifa ulianzia
Januari 2004 na kupitia changamoto nyingi hadi kuwa jengo linalovutia na
alama ya Dubai. Ilichukua siku 1,325 na saa 22 milioni kukamilisha uchimbaji msingi na kufanyia vipimo hadi ghorofa ya mwisho. Msingi ulikuwa imara na ilichukua zaidi ya 330,000
m3 za ujazo wa zege la msingi na vyuma tani 39,000 (43,000 ST; 38,000
LT), ambavyo sasa vimebeba tani 110,000.
Msingi wenyewe umekwenda chini, urefu wa mita 50.
Maboresho ya maeneo ya nje wakati ujenzi unaendelea, ulianza Mei 2007 na
kukamilika Septemba 2009. Makandarasi wenye sifa za hali ya juu 380 walishiriki katika maeneo mbalimbali ya jengo. Jengo hilo, hadi kukamilika kwake, sehemu kubwa limeimarishwa kwa vyuma vya aluminiam na vioo kwa urefu wa mita 512. Jumla ya aluminium iliyotumika kujengea Burj
Khalifa ni sawa na kujenga ndege tano aina ya A380 na urefu wa vyuma
vilivyotumika kuimarishia jengo ni mara 293 ya urefu wa mnafa wa Eiffel
ulioko Paris, Ufaransa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment