Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania
(KKKT) Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele, amesema iwapo rasimu ya Katiba
nayopendekezwa haitasambazwa na kuwafikia wananchi kote nchini mapema,
atatangaza kuwahamasisha wasiipigie kura ya maoni.
Kura ya maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa rasimu
ya katiba hiyo inatarajiwa kupigwa Aprili, mwaka huu, lakini hadi
kufikia jana, ilikuwa haijaanza kusambazwa kwa wananchi. Askofu Mengele alisema hayo katika hafla ya kukabidhi Shule ya
Sekondari ya Ruhuji iliyokuwa chini ya Balozi mstaafu wa Tanzania nchini
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Gidion Ngilangwa.
Alisema amezunguka sehemu nyingi nchini, lakini hajaona mahali ambako wananchi wanakosema kuwa wanaifahamu katiba hiyo. Askofu Mengele alisema wananchi wanatakiwa kuisoma na kuielewa ili
wapige kura kukifanyia maamuzi kile walichokisoma na kukielewa. “Sisi kama kanisa hatutakubali kuwaruhusu wananchi kupigia kura
katiba inayopendekezwa kama haitafikishwa kwa wananchi, kwani wanatakiwa
kuisoma na kuielewa kabla ya kuipigia kura,” alisema Askofu Mengele.
Aliongeza: “Endapo itafika tarehe 30 mwezi wa nne, tutawaambia wananchi wasiipigie kura na wasubiri waisome kwanza.” Alisema kanisa linajiuliza itakapofika Aprili 30, mwaka huu
wananchi watapigia kura ya ndiyo au hapana juu ya nini wakati hawajui
kilichopo ndani ya katiba hiyo.
Kwa mujibu wa Askofu Mengele, kamwe hawawezi kukubaliana na kitu
hicho na kwamba, watatangaza kwa umma ulimwenguni kote wajue, ikiwa ni
pamoja na kuwakataza kupiga kura. Hata hivyo, alisema wataungana na Watanzania wote kuhakikisha
kunakuwapo na amani wakati wote wa mchakato wa katiba na uchaguzi mkuu
wa mwaka huu.
“Sasa mwezi Januari karibu unaisha. Uandikishaji wapigakura
haujaanza. Muda uliopo ni mfupi kweli. Rais alikutana na maaskofu
tukamshauri kuwa apitishe mchakato huo mpaka uchaguzi upite, lakini
alishawishiwa na Bunge la Maalumu la Katiba na kutangaza kufanyika
upigaji wa kura ya maoni kabla ya uchaguzi mkuu,” alisema Askofu
Mengele.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, ambaye ni
Ofisa Tarafa ya Njombe, Lilian Kembele, alisema serikali ina mpango
mkakati wa kuhakikisha inasambaza Katiba inayopendekezwa kwa wananchi
kabla ya muda wa kuipigia kura haujafika. Aliwataka wanasiasa kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea
kwenye mchakato wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa ili kuepuka
kuiingiza nchi katika machafuko.
Alisema serikali haitakuwa na jinsi kama viongozi wa dini
watawazuia wananchi kuipigia kura katiba hiyo, kwani ile ya zamani ipo. Kauli hiyo ya Askofu Mengele, imetolewa siku chache baada ya
aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, kutamka kwamba hakuna uwezekano wa kura ya maoni kabla
ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Jaji Warioba alisema ameona taarifa inayoeleza kuwa kura ya maoni
inatarajiwa kufanyika Machi, mwakani na kusema kama kuna umakini, kura
hiyo haitawezekana kufanyika. Naye Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amewasilisha taarifa
kwa Katibu wa Bunge akitaka Bunge lijadili udhaifu wa katiba
inayopendekezwa na kupitisha azimio la kuahirishwa kufanyika kwa kura ya
maoni ya wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba hiyo.
Pia amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutangaza kufuta tangazo la
serikali la kufanyika kwa kura hiyo mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, hadi
uchaguzi mkuu utakapofanyika. Mnyika alisema kama ambavyo Rais Kikwete alitumia sheria kutangaza
upigaji kura hiyo, ni vema pia akafanya hivyo kuutengua kwa kuwa kuna
udhaifu katika mchakato mzima. Alisema zimebaki siku chache kufanyika mchakato huo, lakini hadi sasa elimu kuhusiana na suala hilo haijatolewa kwa wananchi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment