Social Icons

Pages

Saturday, January 03, 2015

ARUSHA KUZUIA MATANGAZO YA SAUTI KUBWA BARABARANI

Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, (Chadema).
Halmashauri ya Jiji la Arusha, inatarajia kuanza mchakato kuzuia utoaji wa matangazo yanayotolewa kwa sauti barabarani kufuatia malalamiko ya wananchi kuwa matangazo ya aina hiyo yanavuga utulivu na ufanyaji kazi.
Akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani jijini hapa mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Iddi Juma, alisema mpango huo unatarajiwa kuanza hapo baadaye. Kwa muda mrefu Jiji la Arusha linakabiliwa na uchafuzi wa kelele zinazopigwa hovyo mitaani kama vile promosheni za miziki ya dansi, kwaya za dini, matangazo ya kuhamasisha watu kulipa Ankara za maji, mapato, kununua bidhaa madukani na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na dini na upigaji hovyo wa honi za daladala.
“Kwa hapo baadaye matangazo ya barabarani tutayazui kwa sababu wapo wananchi wanaolalamika kuhusu kelele zinazotokana na matangazo hayo wakati wa kazi,” alisema. Alisema kwa hapo baadaye watu watatakiwa kutumia radio za kijamii kutoa matangazo yao na utaratibu mwingine ambao utawekwa.
Kauli hiyo ilitokana na baadhi ya madiwani kulalamikia halmashauri hiyo kwamba haikutoa matangazo ya kutosha kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa kikao hicho.
Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita (Chadema), alisema matangazo yaliyotolewa kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa kikao hicho yalifanyika mjini na sio nje ya mji. “Jiji lina kata 25, matangazo yaliyotolewa hayakusikika kwa wananchi wengi wa kata hizo,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Moshono, Paul Mattyhsen, (CCM), aliunga mkono utaratibu wa kutumia vyombo vya habari badala ya kupiga kelele mitaani. Hata hivyo, Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, (Chadema), alitoa tahadhari kwa utaratibu huo mpya kama utatumika kwamba utawanyima fursa wanasiasa na watu wanaotaka kufanya mikutano ya hadhara ya kidini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: