Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
Hawa Ghasia amewasimamisha kazi wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali
kutokana na kuchelewa kuandaa na kupeleka vifaa vya kupigia kura
pamoja na uzembe katika kutekeleza majukumu yao katika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima Jumapili iliyopita.
Akizingumza na waandishi wa habari leo jijini Dar
es Salaam, Waziri Ghasia amesema uamuzi huo umefanyika baada ya Rais kwa
mujibu wa sheria kuridhia adhabu hizo zitolewe. Alisema wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni
watano ili kupisha uchunguzi zaidi wa kiwango cha ushiriki wao katika
kasoro zilizojitokeza kwenye halmashauri zao.
Wakurugenzi hao waliosimamishwa kazi na
halmashauri zao kwenye mabano ni Fotunatus Fwema (Mbulu), Issabela
Chilumba (Ulanga), Pendo Malabeja (Kwimba), Wiliam Shimwela (Sumbawanga
Manispaa) na Felix.T.Mabula (Hanang).
Kwa mujibu wa Ghasia, wakurugenzi ambao uteuzi wao
umetenguliwa ni sita na watapangiwa kazi za kufanya kutokana na
taaluma zao huku wakurugenzi watatu wakipewa onyo kali na watakuwa chini
ya uangalizi kama wanaudhaifu wachukuliwe hatua zaidi.
Aliwataja wakurugenzi watendaji waliotenguliwa
nyadhifa zao ni Benjamin Mjoya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi (Mkuranga),
Abdalla Ngodu (Kaliua), Masalu Mayaya (Kasulu), Goody Pamba (Serengeti),
Julius Madiga (Sengerema) na Simon Mayeye (Bunda).
Aliwataja wakurugenzi waliopewa onyo kali ni
pamoja na Mohamed Maje (Rombo), Hamis Yuna (Busega) na Jovin
Jungu (Muheza) na watakuwa chini ya uangalizi kubaini kama wana udhaifu
mwingine wachukuliwe hatua zaidi. Waziri Ghasia alionya kuwa ofisi yake haitasita
kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaokiuka maadili ya kazi au
watakaopungukiwa uwezo wa kutekeleza majukumu waliokabidhiwa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment