Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Freeman Mbowe.
Wakazi wa Kijiji cha Nronga kilichopo Wilaya ya Hai,
mkoani Kilimanjaro wamechanga zaidi ya Sh. milioni 170 kwa ajili ya
kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kalali-Nronga, yenye urefu wa
kilomita 6.6
Barabara hiyo inayojengwa na Kampuni ya Elerai Civil Engineering &
Constructions ya Arusha, itakapokamilika, itakuwa kichocheo kikubwa cha
kufunguka kwa fursa za kiuchumi zitakazowanufaisha wakazi Nronga na
vijiji jirani vya Wari na Foo, wilayani hapa.Diwani wa Kata ya Machame Magharibi (Chadema), Elibariki Lema alisema jana kuwa, kwa sasa ujenzi huo upo katika hatua za uumbaji wa barabara pamoja na uwekaji wa makalavati ili kupisha uwekaji wa lami nyepesi kwenye eneo la mradi. “Zaidi ya kilomita nne za barabara hii ni eneo korofi lisilopitika kwa urahisi wakati wa nyakati za mvua. Kutokana na adha hiyo, wananchi wa Kijiji cha Nronga waliamua wenyewe waanze kutafuta namna ya kukabiliana na hali hiyo; ndipo ikaamuliwa na vikao vya serikali ya Kijiji kwamba tuwashirikishe na wazawa waliopo nje ya mkoa wa Kilimanjaro ambao waliitikia wito huo na kutufikisha hatua hizo za ujenzi,”alisema Lema.
Kwa mujibu wa Lema, usanifu wa mradi huo, ulianza mwaka 2012 chini ya usimamizi wa Samweli S. Lema ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Elerai, inayojishughulisha na kazi za ujenzi wa barabara na ukadiriaji wa majenzi. Aidha, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Hai imewaunga mkono wananchi hao kwa kuwapa makalavati na kuwaondolea kodi ya malighafi ya ujenzi kwenye barabara hiyo.
Kuhusu mkakati wa kuiimarisha pia barabara ya Foo-Nronga kwa kiwango cha changarawe, Diwani huyo alisema Mbunge wa jimbo la Hai na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Freeman Mbowe, amewaahidi kuwapatia greda kwa ajili ya kuisafisha na kuimarisha miundombinu yake ili iweze kupitika kwa urahisi nyakati zote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Boniface Kwayu, aliiambia NIPASHE kwamba mradi huo utakapokamilika utavinufaisha kiuchumi vitongoji vya Nrwaa, Nkwamakya, Nkwamandaa, Maasen, Nkwelengya, Nkwakishu na Naluti ambavyo wakazi wake walio wengi ni wakulima na wafanyabiashara. “Tumefika katika hatua nzuri ya ujenzi ambapo mkandarasi yupo kwenye eneo la mradi, akiwa tayari ameshamwaga vifusi vya changarawe kwa ajili ya kushindilia baada ya kuweka makalavati na kuiumba barabara.
Hayo yanayofanyika kwa sasa ni maandalizi ya kupisha uwekaji wa lami baadae tutakapopata fedha za kutosha,”alisisitiza Kwayu. Alisema moja ya mambo atakayotekeleza kwa kipindi kifupi tangu kuchaguliwa kwake kukiongoza kijiji hicho ni kuunda kamati itakayokuwa na mammlaka ya kuratibu shughuli zote za kiuchumi ikiwamo kufungua akaunti maalumu ili kuiwezesha barabara hiyo kuwa mradi endelevu.
“Rai yangu kwa wadau wa maendeleo, serikali na wafanyabiashara wenye moyo wa kutuunga mkono, wasisite kufanya hivyo kwa kuwa nchi hii, tunaamini itajengwa na wenye moyo. Tunahitaji sapoti ya hali na mali kwa sababu kaya 713 za kijiji cha Nronga chenye wakazi zaidi ya 2,500 hawawezi peke yao,”alisema Kwayu. Awali, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho (VEO), Valerian Lema, alisema wakazi wake bila ya kujali itikadi za vyama vyao, kwa kauli moja wameridhia kila kaya kuchangia kiasi cha Sh. 10,000 kwa mwezi ambao hadi kufikia sasa wamekusanya zaidi ya Sh. 3,000,000 katika awamu ya kwanza ya mradi huo.
“Kila kaya inalazimika kuchangia kiwango hicho kama nguvu za wananchi, lakini pia wazawa wa Nronga ambao wanaishi nje ya mkoa wa Kilimanjaro, wanashiriki moja kwa moja kwenye kuuwezesha mradi huu kufanikiwa. Wananchi hawa wamejitoa kwa moyo mkunjufu kukikwamua kijiji chao kiuchumi kwa kuanza ujenzi wa barabara…Huu ni mwanzao mzuri wa kukumbuka walipotoka,”aliongeza Valerian.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment