Pages

Tuesday, December 16, 2014

WAMUOMBA JK KUTEUA MWENYEKITI TUME HAKI ZA BINADAMU

Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu (THRDC), umemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuteua mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ( CHRAGG) na makamishna ili kuuwezesha mtandao huo kufanya kazi  ikiwamo kuingilia kati uvunjifu wa haki za binadamu unaoendelea nchini.
Mratibu wa mtandao, Onesmo Ilengurumwa, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema baadhi ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vingeweza kuzuiliwa kama tume ingekuwa na viongozi wa juu. “Ni mwaka mmoja sasa tangu tume imekuwa ikifanya kazi bila  kuwa na mwenyekiti, mwenyekiti msaidizi na makamishna bila uongozi huo hapa ni sawa hakuna tume,” alisema.
Olengurumwa alisema Mwenyekiti na msaidizi wake ni viongozi wanaoteuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya kamati ya uteuzi chini ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na mapendekezo ya kamati ya uteuzi chini ya Katiba ambayo imeshafanya kazi yake.
Tume hiyo ilikuwa inaongozwa na Jaji Kiongozi Mstaafu, Jaji Amir Manento, ambaye amemaliza muda wake. Aidha, THRDC imelaani vikali kutishwa kwa watetezi wa haki za wafugaji walioko Loliondo wilayani Ngorongoro, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihamasisha haki ya ardhi kwa wafugaji baada ya wafugaji kutaka kuporwa ardhi yao na kupewa mwekezaji. 
Alisema vitisho hivyo pia vinafanywa kwa waandishi wa habari wanaoandika kwa undani mgogoro huo  pamoja na maeneo ya Kiteto, Hannang, Kilosa, Morogoro, Mbeya, Mara na Rukwa na chanzo kikubwa ni uwepo wa mwekezaji.
Alisema vitisho hivyo vinakwenda sambamba na madai ya kuwa wanaotetea wafugaji ni raia wa Kenya na wanapewa ufadhili na serikali ya nchi hiyo jambo ambalo siyo kweli.
Olengurumwa alilitaka jeshi la polisi kuchunguza tuhuma wanazotupiwa watetezi wa haki za wafugaji ikiwemo waandishi wa habari na kwamba ni wakati wa watetezi hao kujilinda na maadui wa haki kwa ajili ya usalama.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment