Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa
habari, Dar es Salaam jana, kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyia Jumapili iliyopita. Kulia ni Naibu Mkurugenzi wa habari wa
chama hicho, Abdul Kambaya.
Mwenyekiti
Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe amesema
umoja huo utafanya tathmini ya maeneo ambayo wangeweza kushinda kwa
kusimamisha mgombea mmoja kila eneo ili kuwachukulia hatua viongozi
waliokiuka makubaliano hayo. Wenyeviti wa umoja huo wa vyama vinne CUF,
Chadema, NLD na NCCR Mageuzi, walisaini makubaliano kadhaa ikiwamo
kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na Ukawa katika chaguzi
zote kuanzia Serikali za Mitaa mpaka uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika Jumapili, katika baadhi ya maeneo, kila chama kilisimamisha
mgombea wake na matokeo yake kuipa nafasi CCM kushinda.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema
viongozi wote kutoka vyama hivyo waliohusika kukiuka makubaliano hayo
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Tutafanya tathmini ambayo itatupatia picha halisi
ya sababu zilizochangia baadhi ya maeneo kukiuka makubaliano.
Tutawachukulia hatua za kinidhamu. Tunajua hawakuwa na maandalizi na
muda wenyewe ulikuwa hautoshi lakini tutaangalia kwa nini hali hiyo
ilijitokeza,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema awali, viongozi wa ngazi za juu
katika umoja huo walitoa maagizo ambayo yalitakiwa kutekelezwa na
wagombea wote wanaounda Ukawa.
“Hakuna mwanachama asiyejua kama umoja ni nguvu,
kwa viongozi wa ngazi za juu tunalifahamu hilo kwa kiwango kikubwa
lakini hata ngazi za chini wanatakiwa kulitambua hilo,” alisema.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema changamoto hiyo imekuwa kikwazo ambacho kimesababisha kukosa
ushindi katika maeneo mengi ya uchaguzi huo.
Nyambabe alisema tathmini itakayofanyika ndani ya
umoja huo, itakuwa nafasi muhimu ya kujipanga kufanikiwa katika uchaguzi
mkuu ujao.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment