Wakulima wa vijiji vya
Ibingu na Kisongwe, Kata ya Lumbiji wilayani hapa wamelalamikia
kukithiri kwa vitendo vya wafanyabiashara kununua mazao kwa kutumia
vipimo visivyokubalika kisheria.
Malalamiko hayo waliyatoa mjini hapa jana kwa
nyakati tofauti na kuongeza kuwa licha ya vipimo hivyo, ambavyo ni
Lumbesa na Makokoro, kupigwa marufuku, bado vinaendelea. Walisema wanunuzi hao wamekuwa wakienda katika
maeneo ya vijiji hivyo na kutaka kuuziwa mahindi na mpunga kwenye
magunia yaliyojazwa kupita uzito wa kawaida wa kilo 100. Mmoja wa wakulima hao ambaye ni mkazi wa Kijiji
cha Kisongwe, Cecilia Simon alisema kuwa ni vyema Serikali ikaingilia
kati tatizo hilo ili wafanyabiashara hao wasiendelee kuwanyonya wakulima
wakati wanaponunua mazao.
Alisema ununuzi wa mazao hayo kwa kutumia vipimo
hivyo hauwanufaishi wakulima ambao wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na
muda mrefu katika kuzalisha, badala yake huwapa faida wafanyabiashara.
Simon aliitaka Serikali kuwachukulia hatua watakaobainika kukiuka utaratibu na kutumia vipimo hivyo.
“Tunaiomba Serikali iendelee kusimamia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaowalaghai wananchi,” alisema Simon. Mkazi wa Kijiji cha Ibingu, Patrick Machemba
aliiomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwafundisha mbinu bora
za usindikaji wa mazao yao ili wayaongezee thamani.
Mwakilishi wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa
Misitu Tanzania (Mjumita), Elida Fundi alisema Shirika la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na mtandao huo wanaangalia uwezekano wa
kuwapatia wakulima mbinu bora za kilimo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment