Wafuasi wa Chadema mjini Nansio Wilaya ya Ukerewe, Mwanza wakishangilia 
ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi.  Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za
 Mitaa uliofanyika juzi, yanaonyesha kuimarika kwa upinzani nchini baada
 ya kupata viti vingi vya uenyekiti wa mitaa na vijiji, pamoja na mamia 
ya wajumbe wa Serikali husika.
Hayo yanaonyesha kuwa vyama hivyo vimeanza 
kuimarika katika ngazi za chini, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2009, 
katika uchaguzi ambao CCM kilipata ushindi wa kishindo wa asilimia 
91.72, huku wapinzani wakigawana asilimia 8.28 zilizobaki. Licha ya uchaguzi wa juzi kugubikwa na kasoro 
lukuki, upinzani umeonekana kuchomoza huku katika baadhi ya mikoa 
ukipata ushindi maradufu hasa katika ile ambayo una nguvu kubwa wakati 
katika maeneo ambayo ulikuwa na viti vichache au kutokuwa navyo kabisa, 
umeibuka na kuipokonya CCM baadhi ya mitaa na vijiji. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi 
(Ukawa); Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimejizolea viti vingi tofauti na 
awali, huku chama kipya cha ACT kikichomoza na kupata ushindi katika 
maeneo kadhaa ya mikoa ya Kigoma na Katavi. Mikoa ambayo upinzani umeonekana kuzoa viti vingi 
ni Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Kigoma, Mara, Kagera na Dar es 
Salaam, hali ambayo wachunguzi wa mambo wameielezea kuwa siyo dalili 
njema kwa CCM. Nguvu ya upinzani inaonekana kuongezeka siku hadi 
siku ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 1995 wakati ulipofanyika 
Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya siasa. Hii ni mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani 
kuonyesha ushindani mkubwa katika uchaguzi wa chini, hali ambayo inaweza
 kuwa ni jibu la ukosoaji ambao umekuwa ukifanywa kwamba vyama hivyo 
vimejikita mjini tu na kusahau kufanya siasa kwa wananchi. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) Iringa,
 Profesa Gaundence Mpangala alisema matokeo ya uchaguzi yanayoendelea 
kutangazwa, yanadhihirisha kuwa CCM itaendelea kukabiliwa na upinzani 
mkubwa hata kwa Uchaguzi Mkuu ujao mwakani. Licha ya mafanikio hayo, kwa upande wa upinzani, 
matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa bado CCM inaelekea kushinda kwa kupata
 mitaa na vijiji vingi ikilinganishwa na upinzani. CCM kinaendelea kuweka mizizi katika mikoa ya 
Tanga, Morogoro, Dodoma, Pwani na baadhi ya wilaya katika mikoa ya 
Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Mwanza. Katika uchaguzi wa mwaka huu, Chadema kinaongoza upinzani kwa 
kupata viti vingi mfano halisi ukiwa mkoani Mbeya ambako kimeshinda viti
 74 ikilinganishwa na viti tisa kilivyopata katika uchaguzi wa 2009. Mkoani Arusha, chama hicho kimeshinda viti 75, 
kutoka saba kilivyopata katika uchaguzi uliopita, wakati katika Manispaa
 ya Shinyanga kimeibuka kidedea baada ya kujizolea mitaa 29. CCM 
ikiambulia mitaa 26. Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Rashid Juma Idd 
alisema jana kuwa katika uchaguzi huo, licha ya Chadema kupata vivi 
hivyo 75, CCM kilipita bila kupingwa katika mitaa sita na kufanya kiwe 
na viti vya wenyeviti 78 hadi jana. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema 
alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na kwamba katika maeneo 
mbalimbali, kura zimezidi watu waliojiandikisha. Lema alisema katika moja ya vituo Kata ya Unga Ltd
 wapigakura walikuwa 800 lakini kura zimezidi na kufikia 1,200. Alisema 
kwa ujumla, Chadema kinaamini kwamba kimeshinda viti 104 kwani kuna 
mitaa ambayo wajumbe wote wa Serikali na viti maalumu wanatoka chama 
hicho na wenyeviti pekee ndiyo wanaotoka CCM. Chadema pia kimefanya vizuri katika Mji wa Kahama 
ambako Mkurugenzi Mtendaji wake alisema kimeshinda katika mitaa 18 kati 
ya 32 wakati CCM kilishinda mitaa 14. Katika Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, CCM 
kimeshinda mitaa 35 na upinzani viti 31. Katibu Msaidizi wa CCM, Abdul 
Kambuga alisema chama chake hakikufanya vizuri katika uchaguzi huo na 
kuwa ilihujumiwa wakati wa maandalizi ya kupiga kura. Mwenyekiti wa Chadema katika Manispaa hiyo, Victor
 Sherejei alisema ushindi huo mkubwa kwa upinzani unatoa somo kuwa 
wananchi wamekata tamaa baada ya kusubiri mabadiliko kwa muda mrefu. Kwa upande wake, CUF kimeviongoza vyama vya 
upinzani kuikaba koo CCM katika Manispaa ya Mtwara (Mikindani) ambako 
vyama hivyo vimepata viti 53 na kubakiza 58 mikononi mwa chama tawala. 
CUF kimeshinda mitaa 36, Chadema mitaa 16, NCCR Mageuzi minne na TLP 
mmoja. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani 
wameonekana kufurahia matokeo hayo na kwamba kama si kasoro ambazo 
wanadai kwamba zilipangwa na chama tawala, yangekuwa mazuri zaidi.
“Licha ya vikwazo vilivyolenga kuhujumu upinzani, 
Ukawa imepata mafanikio makubwa,” alisema
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum 
Mwalimu alisifu kile alichokiita mafanikio hayo ya upinzani katika 
uchaguzi huo. “Hii inaonyesha tumefanikiwa kulingana na tulikotoka 
ambako CCM ilikuwa inashinda kwa asilimia 96 na wapinzani kugawana 
asilimia 4 tu,” alisema. Kasoro ambazo ziliathiri uchaguzi huo ni pamoja na ukosefu wa 
vifaa vya kupigia kura, vituo kuchelewa kuanza kazi, wizi wa karatasi za
 kupigia kura, wapiga kura kukuta majina yao yameshatumika kupiga kura, 
wananchi kuzuiwa na wengine kutokuta majina yao kwenye vituo vya kupigia
 kura. Kadhalika, kulikuwa na matukio yaliyoashiria 
kuvunjika kwa amani yakiwamo wananchi kupigana, polisi kurusha risasi na
 mabomu ya machozi na tukio la uchomaji wa ofisi ya mtendaji katika moja
 ya Kata za Manispaa ya Sumbawanga, Rukwa. Kutokana na kasoro hizo, uchaguzi uliahirishwa katika maeneo kadhaa na umepangwa kufanyika kati ya kesho na Jumapili ijayo.
                
              
Hali halisi
Hali halisi
Msimamizi wa Uchaguzi katika Jiji la Mbeya, Musa 
Zungiza alisema CCM hadi jana ilikuwa imepata mitaa 103, Chadema 74 na 
NCCR-Mageuzi ilipata mitaa miwili. Mitaa miwili ya Kata za Itiji na 
Mwansekwa, ilitarajia kurudia uchaguzi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kata ya 
Igurusi CCM imeshinda vijiji saba, Chadema viwili na katika Wilaya ya 
Rungwe, Kata ya Kiwira yenye vijiji vitano, Chadema imeshinda vitatu CCM
 viwili. Chadema pia imeshinda viti vitatu katika Kata ya Ndato yenye 
vijiji vinne na CCM ina kijiji kimoja. Vijiji sita vya Kata ya Isongole vimechukuliwa na 
CCM pamoja na vijiji vingine vitano vya Kata ya Suma, huku wapinzani 
wakiambulia patupu. Kata ya Kyimo yenye vijiji vitano, Chadema imeshinda
 vitatu na CCM viwili. Matokeo Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, 
Kata ya Maendeleo yenye vijiji vitano CCM, imeshinda vinne na Chadema 
kimoja, wakati katika Wilaya Ileje CCM imeshinda vijiji sita vya Kata ya
 Ikunga, Chadema imeambulia viti viwili.
 
CHANZO: MWANANCHI 
No comments:
Post a Comment