Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda.
Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa umeingia sura mpya baada ya kusababisha mauaji ya watu
wawili katika matukio tofauti yaliyotokea katika Wilaya za Nzega mkoani
Tabora na Bukombe mkoani Geita.
Wakati tukio la Bukombe likihusisha mtu kuchinjwa
katika sherehe za ushindi wa mkewe kuwa mwenyekiti wa mtaa, huko Nzega
kijana moja alipigwa risasi na polisi wakati wa kusubiri matokeo ya
uchaguzi huo.
Bukombe
Mume wa mshindi wa kiti cha mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Kapela, wilayani Bukombe ameuawa baada ya kuchinjwa katika
hafla ya ushindi wa mkewe.
Mtu huyo, Bundara James (56), aliuawa usiku wa
kuamkia juzi katika Mtaa wa Kapela ulioko kwenye Kata ya Igulwa wilayani
Bukombe muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya kusherehekea
ushindi huo.
Mke wa marehemu ambaye sasa ni mwenyekiti wa mtaa
huo, Lusia Samwel alisema mumewe ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbogwe, alikutwa amechinjwa na watu wasiojulikana ambao
walitoweka baada ya tukio hilo wakiacha panga walilofanyia uhalifu
kwenye eneo la tukio.
Samwel aliibuka mshindi kupitia Chadema kwa kupata
kura 463 akimwacha kwa mbali mpinzani wake kutoka CCM ambaye alipata
kura 230.
Alisema baada ya ushindi huo, Chadema iliamua
kufanya sherehe ya kumpongeza nyumbani kwake na ilipomalizika, mume huyo
aliondoka nyumbani saa 1.13 jioni akiwa ameambatana na mwanaye wa kiume
kurudisha vyombo vya muziki walivyokodi kwa ajili ya sherehe hiyo.
Alisema wakiwa wanakula chakula cha usiku ndani,
mtoto alitoka nje na kurudi akikimbia: “Akasema mama kuna mtu amelala,
tulipotoka nje tulikuta mume wangu amelala chini akiwa amechinjwa
shingoni na panga limetelekezwa chini.” Alisema anaamini kuwa wauaji hao
waliusogeza mwili wa marehemu karibu na nyumba yake.
Mtoto aliyemsindikiza baba yake kurudisha vyombo
vya muziki, Rubeni Bundara alisema walifika salama na kukabidhi vyombo
hivyo na baba yake akamwambia awahi nyumbani.
“Baadaye baba aliniambia mimi nirudi nyumbani nikapumzike. Sikujua kama angekutwa na umauti,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo
alisema jitihada zinafanywa kuwasaka wahusika na ameagiza timu ya askari
kutoka mkoani humo kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment