
Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kumfuta kazi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi,
amesimamishwa kazi.
Rais Kikwete alitangaza uamuzi wa kumfuta kazi Profesa Tibaijuka juzi
wakati akilihutubia taifa kupitia mkutano wake na wazee wa Mkoa wa Dar
es Salaam, kutokana na kuhusika kupokea mgawo wa fedha za akaunti ya
Tegeta Escrow Sh. bilioni 1.6. Uamuzi wa kumsimamisha Maswi ulitangazwa
jana jioni kupitia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu,
ambayo ilieleza kuwa:
“Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi
kwa muda Ndugu, Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini, ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na Rais Jakaya
Kikwete.”Taarifa hiyo ilieleza kuwa Balozi Sefue alimsimamisha kazi Maswi kuanzia jana kwa kutumia madaraka aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Taarifa hiyo iliongeza: “Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua hatua hiyo Kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa) ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.”
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na hatua hiyo, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi uchunguzi dhidi ya Maswi utakapokamilika. Taarifa ya Balozi Sefue pia ilikariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa juzi akisema kuwa: “Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Kadhalika taarifa hiyo ilieleza kuwa, Rais Kikwete ameelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa, Shirika la Umeme (TANESCO) waendelee na majadiliano na IPTL kuhusu uwezekano wa kushusha tozo la uwekezaji (capacity charge) zaidi ya punguzo la awali lililopatikana kupitia Kituo cha Kimataifa cha Kusuluhisha Migogoro ya Kimataifa (ICSID).
Kabla ya taarifa ya kusimamishwa kwa Maswi, watu mbalimbali walitoa maoni yao wakieleza kutofurahishwa kwao na hatua ya Rais Kikwete kumfukuza kazi Profesa Tibaijuka na kumuacha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Maswi.
Rais Kikwete juzi kupitia mkutano wake na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitangaza kumfukuza kazi Profesa Tibaijuka kutokana na kitendo chake na kupokea mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering & Marketing Limited, James Rugemalira. Fedha hizo zilitokana na mabilioni ya fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Walisema hatua ya Rais kumfukuza kazi Profesa Tibaijuka na kuwaacha Profesa Muhongo na Katibu Mkuu wake, Maswi, imeacha maswali mengi kwa Watanzania.
SLAA AWANG’ANG’ANIA MUHONGO, MASWI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeikosoa vikali hotuba ya Rais Kikwete huku kikitaka Profesa Muhongo, Maswi na majaji waliopewa mgawo wa Escrow, wawajibishwe. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema wamesikitika kuona Rais Kikwete kutumia saa mbili kurudia kufafanua masuala ambayo yameshaelezwa na Bunge kwa kina huku akishindwa kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wa serikali waliohusika katika utafunaji wa fedha za akaunti ya Escrow ya Tegeta.
Dk. Slaa alidai kuwa hotuba ndefu ya Rais Kikwete ilijikita katika kujibu maswali 21 ya mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira. "Hotuba ya Rais Kikwete ni kichekesho, ametumia vibaya muda wa saa mbili akifuja fedha za umma kulipia matangazo ya televisheni akirudia kueleza mambo ambayo yameshafafanuliwa na vyombo vya serikali vikiwamo Bunge na CAG.
Katibu Mkuu huyo pia alipinga uamuzi wa kumweka kiporo Profesa Muhongo, Maswi huku akikosoa pia uamuzi wa Rais Kikwete kulirejesha kwa Jaji Mkuu sakata la baadhi ya majaji kuhusika katika mgawo wa fedha za akaunti hiyo. “Taifa linapelekwa kaburini, juzi tulieleza namna hotuba ya Kikwete itakavyowatetea Muhongo na watendaji wengine wa serikali waliohusika na ufisadi wa akaunti ya Escrow, tutaendelea kushikilia msimamo wetu kuwaeleza wahisani wasitoe fedha za kusaidia bajeti ya serikali na miradi ya maendeleo mpaka pale mafisadi watakapowajibishwa,” alisema. "Tibaijuka ameachia ngazi, lakini tunataka tuone akirudisha fedha zetu na kufikishwa mahakamani. Pia tunataka Kikwete aeleze mchango wake mwenyewe katika sakata la Escrow. Anaficha nini yeye kama yeye?” alihoji Dk. Slaa.
DEUS KIBAMBA WA JUKATA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, alisema Rais Kikwete alitakiwa kuwawajibisha wahusika wote wa kashfa ya Escrow kwa kutoa maamuzi, badala ya kuamuru uchunguzi mpya. “Kama Rais ambaye ni Kiongozi Mkuu wa nchi ambaye katika maandiko ya dini anaweza kufananishwa na Kaisari, alipaswa kutoa maamuzi moja kwa moja na si kutoa uamuzi kwa mtuhumiwa mmoja, hawa walikuwa watimishi wa umma, Rais alipaswa atekeleza yale yaliyo ndani ya mamlaka yake,” alisema Kibamba.
Alisema kuwa kile kilichompata Profesa Tibaijuka, ndicho ambacho kingewapata Profesa Muhongo na Maswi. “Hivi kweli Rais kama kiongozi mwenye dhamana ya mwisho katika maamuzi ndani ya nchi hii anamfukuza Waziri Tibaijuka na kuwaacha Muhongo na Maswi ambao walipaswa kuwajibika kutokana na makosa yaliyotokea kama alivyofanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema?,"
alihoji Jonathan Baweje, mkazi wa jijini Tanga.
Naye Ramadhan Manyeko, pia mkazi wa jijini Tanga, alisema hotuba ya Rais ilionyesha kuwabeba Profesa Muhongo na Maswi na kwamba hayuko tayari kufanya maamuzi magumu dhidi yao. “Mama Tibaijuka katolewa tu mbuzi wa kafara kutokana na hali ilivyoanza kuchafuka, lakini kama umeifutilia vizuri hotuba nzima ya Rais, ililenga kuwasafisha,” alisema Manyeko.
Liundi wa TGNP Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, alisema Rais Kikwete alipaswa kumuwajibisha Profesa Muhongo ili kupisha uchunguzi ambao unaendelea. Alisema kitendo cha kumuondoa Profesa Tibaijuka ni jambo jema lakini pia alipaswa kumuondoa na Profesa Muhongo ambaye mazingira yanaonyesha kwamba alipaswa kuwajibishwa.
Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso) wamesema Rais Kikwete alitakiwa kuwajibisha mawaziri wote waliotajwa kuhusika katika sakata la Escrow badala ya kumuwajibisha Profesa Tibaijuka peke yake. “Kama Rais aliamua kuwaondoa mawaziri wote waliokuwa wametajwa kuhusika na sakata la Escrow, angewaondoa wote, hasa Wizara ya Nishati na Madini wanaotajwa kuhusika moja kwa moja katika sakata lile na kama aliamua kuwaacha angewaacha wote kwani inaonekana Profesa Tibaijuka amekuwa mbuzi kafara kwa wengine,” alisema Mwenyekiti wa Tahliso, Mussa Mdede.
Aliongeza kuwa hapaswi kuwaacha Waziri Muhongo na Maswi waliotajwa moja kwa moja. “Kama Rais aliamuliwa na kushauriwa pia na kuchukua maamuzi magumu, basi angewajibisha wote wanaotajwa kuhusika...hayo si maamuzi magumu na yenye tija tuliyoyategemea kutoka kwa Rais kama Mkuu wa Nchi na Watanzania hawawezi kuridhishwa na uamuzi huu unaoonekana kulenga mtu mmoja na kuacha wengine,” alisema.
Bisimba wa LHRC Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen-Kijo Bisimba, alisema ameshangazwa sana na maamUzi ya Rais Kikwete kumwajibisha Profesa Tibaijuka na kuwaacha Muhongo na Maswi. “Wananchi walitarajia angechukua maamuzi magumu dhidi yao, lakini cha kushangaza akafanya hivyo kwa Tibaijuka ambaye yeye alipewa pesa hizo kama mgawo na kuwaacha hao ambao waliamua fedha hizo zitolewe,” alisema Bisimba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Loisulie, alisema hatua ya kuwaweka kiporo Profesa Muhongo na Maswi, huenda ni njia ya kuwasafisha. Alisema jambo la msingi la kukumbuka maazimio ya Bunge yaliridhiwa na pande zote hivyo itasababisha mpasuko miongoni mwa wanasiasa hasa ndani ya chama tawala na mwisho wa siku kukigharimu kwenye uchaguzi.
Hata hivyo, alisema maamuzi ya aina hiyo yatawafanya watu wasiogope kuiba kwani hakuna hatua yoyote ya maana itakayochukuliwa. “Kwangu mimi yamesababisha mambo yafuatayo, moja ni mkanganyiko zaidi juu ya nani hasa mwenye makosa. Pili, imezidi kuibua maswali mengi juu ya kile kinachofahamika kuhusu suala husika na imeleta hisia kwamba wezi wanalindwa kwani hata kutolewa Profesa Tibaijuka ni kwa shingo upande,” alisema Loisulie.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) mkoani Dodoma, Kayumbo Kabutari, alisema pamoja na kutoa maamuzi hayo, ni vyema CCM ikawachukulia hatua viongozi watovu wa nidhamu na wasio na maadili.
“Jana (juzi), Kikwete alijitahidi sana kukitetea chama chake na kuwataka wabunge wake watetee chama wasiwaachie wapinzani huku akisahau kuwa CCM haitetewi na wabunge bali ni chama chenyewe kuchukua hatua za kimaadili na nidhamu ndani ya chama dhidi ya wanachama na viongozi watovu wa nidhamu na maadili,” alisema Kabutari. “Kama kweli CCM inachukia wizi, ufisadi kimewachukulia hatua gani wanachama wake wanaodaiwa kuwa watovu wa maadili akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge?” alihoji Kabutari.
MBUNGE EALA
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Angella Kizigha (CCM), amewataka Watanzania kuwa wavumilivu wakati uchunguzi wa Tegeta Escrow ukiendelea. “Nina imani na Rais hatasita kuwachukulia hatua za kuwawajibisha wale wote watakaobainika kama alivyofanya kwa Profesa Tibaijuka,” alisema.
Kuhusiana na kutenguliwa kwa uwaziri wa Profesa Tibaijuka, Kizigha alisema ni hatua ambayo Rais Kikwete ameona inafaa na kuwa hakukurupuka kutoa uamuzi huo. Msafiri Kimath, mkazi wa Morogoro, alisema maamuzi ya Rais ni mazuri, lakini siyo magumu kwa kuwa Watanzania walitegemea hata Waziri Muhongo angemuwajibisha kutokana kulifahamu sakata hilo vizuri tangu akiingia katika wizara hiyo.
Kimath alisema Rais pia amepuuza uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba ana wasiwasi na matokeo ya uchunguzi mpya alioamuru ufanywe na kuahidi kuuchukua. Alisema kutokana na taarifa za awali za Kamati ya PAC na sheria za utumishi zikihusisha utawala bora, Rais Kikwete alipaswa kumwajibisha Waziri Muhongo kutokana na kuhusishwa.
Mkazi mwingine wa Manispaa ya Morogoro, Johari Mohamed, alisema ni vema Rais angefanya maamuzi japo ni magumu, akawaondoa Muhongo na Maswi.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alihad Mussa Salum, alipongeza hatua ya Kikwete ya kumuengua Profesa Tibaijuka na kwamba kwa upande wa Profesa Muhongo na Maswi, anawaomba Watanzania wasubiri ahadi aliyotoa Rais baada ya kukamilika kwa uchunguzi na kwamba anaamini atatekeleza.
Asasi ya kiraia ya Smart Legal Professionals Clinic (SLPC) ya jijini Arusha, imesema kauli kwamba fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwamo za umma, si sahihi kutokana na taarifa zilizokwisha tolewa na CAG pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kueleza kuwa fedha hizo zilitakiwa kulipiwa kodi.
Mwenyekiti Mtendaji wa SLPC, Masesa Mashauri, alisema kwa mujibu wa maelezo hayo, inaonyesha kuwa fedha hizo ni za umma. Kuhusu kumuachisha kazi Profesa Tibaijuka, alisema ni uamuzi mzuri kwa sababu Rais ndiye aliyemteua. Hata hivyo, alisema kitendo cha kuwaacha Muhongo na Maswi kimeonyesha udhaifu mkubwa katika nyanja ya utawala bora.
MUKOBA WA TUCTA
Rais wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gratian Mukoba, alisema wananchi walitegemea Rais Kikwete juzi angechukua maamuzi magumu ya kumtimua kazi Waziri Muhongo na Maswi mara moja. Aidha, alisema kitendo cha Rais kumtimua ProfesaTibaijuka huku akiwaacha wengine waliohusika na udalali wa pesa za Escrow, kimeacha maswali vichwani mwa Watanzania.
Mukoba alisema katika hotuba hiyo, alimshangaa Rais Kikwete kwa kuwasifia wajumbe 19 waliounda Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyoshughulikia malalamiko ya Escrow kuwa ni wananchama wa CCM.
FRANCIS STOLLA
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Francis Stolla, alisema maamuzi yaliyochukuliwa na Rais Kikwete ni sahihi kwani walikuwa wameshakiuka taratibu za mwajiri wao (Rais).
Stolla aliongeza kuwa kutenguliwa uteuzi wa Profesa Tibaijuka na uchunguzi kuendelea dhidi ya Profesa Muhongo, ni sahihi kwani mazingira ya ukiukwaji wa sheria baina ya viongozi hao wawili ni tofauti.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment