
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda
Wakati Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) ikiwa imetangaza kufanya uchunguzi kubaini sababu
zilizopelekea kujitokeza kwa dosari nyingi kwenye uchaguzi wa serikali
za mitaa, wasomi, wanasiasa na wananchi wamemtaka Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda na wasaidizi wake kujiuzulu mara moja.
Wametoa maoni hayo jana wakati wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati
tofauti kuhusiana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo
uliofanyika Jumapili ya wiki iliyopita na kusababisha maeneo kadhaa
uahirishwe hadi Jumapili ijayo.DAR ES SALAAM
KAIMU Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda, alisema Waziri wa Tamisemi, Ghasia ajiuzulu kabla ya kuanza kuwawajibisha waliokwamisha zoezi hilo. Mwakagenda alisema wizara hiyo ina majukumu mengi hivyo haikupaswa kupewa kazi ya kusimamia uchaguzi huo kwani ni jukumu kubwa.“Tulitarajia matokeo kama haya, pamoja na kushauri kwamba zoezi hili lisifanywe na Tamisemi bado wamelazimisha, wizara ambayo ina majukumu mengine na wanajipa jukumu kubwa, malengo yao yametimia,” alisema. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana (pichani chini), alisema mambo yaliyotokea katika uchaguzi huo yanaonesha jinsi gani Watanzania wameelimika katika demokrasia ya kuchagua viongozi wao. “Kilichotokea kinaonyesha Watanzania wamejua wajibu wao wa kumuwajibisha kiongozi au chama kinachoshindwa kuwatekelezea matakwa yao kama walivyoahidi,” alisema. Bana alisema katika maeneo mengi ambayo CCM imeshindwa, ilikuwa ni ngome zao za siku nyingi ambazo walijiweka, lakini kutokana na wananchi kupata elimu juu ya kiongozi anayefaa, imewafanya kuonyesha kuwa wanaweza kuiondoa CCM madarakani. Mhadhiri katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk. Wineaster Anderson, alilaani kasoro hizo huku akishangazwa na mamlaka husika kutangaza kufanyika kwa zoezi hilo wakati maandalizi hayajakamilika. “Unapoandaa uchaguzi kuna vitu vinaitwa ‘fair’ na ‘objective’…unapotangaza uchaguzi, tunatarajia kila kitu kuwa kimekamilika. Huu ni uzembe ambao kwa namna nyingine ukionekana kumnufaisha mtu fulani…ni jambo la kulaumiwa sana,” alisema Dk. Wineaster. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Agustino, Prof. Mwesiga Baregu, alisema serikali inapaswa kulaumiwa kwani inajua vyema kuhusu taratibu na kanuni zinazosimamia masuala ya uchaguzi nchini. Prof. Baregu alisema wakati Watanzania wakiweka kipaumbele katika uchaguzi huo, lakini haikuwa hivyo kwa serikali.Katibu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), David Mwasote, alisema anayehusika na suala hilo ni wasimamizi wa uchaguzi huo huku muda uliowekwa kwa ajili ya maandalizi ukiwa mdogo. Mwenyekiti Jukata, Deus Kibamba (pichani kulia), alisema uchguzi huo ulikurupushwa na kwamba haiwezekani Rais kuacha makubaliano yaliyofikiwa kati yake na vyama vya siasa katika kikao cha pamoja na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Mhadhiri wa Idara ya Isimu na Fasihi ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Eliza Gwajima, alisema kilichoendelea kwenye uchaguzi huo ni changamoto kwa serikali na chama tawala kijifunza kuhusu masuala ya demokrasia ndani ya mfumo wa vyama vingi. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya, alisema serikali haikujipanga kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka huu. Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi ndio inapaswa kuwajibishwa kutokana na kuharibika kwa zoezi la upigaji wa kura wa serikali za mitaa.Mgaya alisema serikali haikujipanga vizuri katika zoezi hilo ndio maana matatizo mengo na ya kizembe yalijitokeza zikiwamo vurugu. “Ni jambo la kushangaza wala haiingii akilini kuambiwa eti Dar es Salaam na Morogoro hapa karibu, vifaa vya kupigia kura havikufika, hili suala ni la uzembe wa hali ya juu, na kama kuwajibika Waziri mwenye dhamana anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu,” alisema Mgaya. Magaya alisema wananchi wameamka, hivyo serikali inapaswa kuhakikisha inakuwa makini katika zoezi la uchaguzi ili isije ikawa ni njama ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kujitafutia ushindi kupitia uzembe huo.
ARUSHA
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Arusha wamesema Wizara ya Tamisemi inapaswa kubeba lawama kwa kuvurugika uchaguzi huo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.Mkazi wa Mbauda, Said Njuki, alisema kwa asilimia 100 Tamisemi inapaswa kubeba lawama. Alisema wasimamizi wa uchaguzi pamoja na watendaji wamehusika kuvuruga uchaguzi huo ama kwa uzembe au kwa kupewa maagizo na CCM.Njuki alitoa mfano katika kijiji cha Salami wilayani Kondoa, jina la mgombea wa CUF, Yahaya Said Yahaya, halikuwamo kwenye orodha ya karatasi za wapiga kura na badala take lilikuja jina tofauti na kusababisha malalamiko ya wananchi. Kwa upande wake mkazi wa Mianzini, Calist ole Mollel, alisema CCM ndiyo wanaoharibu uchaguzi kutokana na tabia yao ya kutaka kudhibi vyama vya upinzani.Mollel alisema ili chaguzi ziwe huru kunatakiwa kuwepo na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo haitakuwa na upendeleo wa upande fulani. “Watu bado wana hasira ya uchakachuaji wa Katiba inayopendekezwa na suala la wizi wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow,” alisema.
MOROGORO
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge (CPW), Dk. Albanie Marcossy, alisema inashangaza Waziri wa Ghasia kueleza kuwa uchaguzi huo umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 wakati kumetokea kasoro zilizosababisha vurugu katika ngazi ya halmashauri. Dk. Marcossy alisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu mengi ikiwamo ya kukosekana kwa vitendea kazi pamoja na baadhi ya maeneo kutofikiwa na wasimamizi wa uchaguzi hadi saa 5:00 asubuhi. “Waziri Ghasia hawezi kukwepa katika hili yeye ndiyo waziri mwenye dhamana ya kusimamia hao watendaji wa halmashauri waliovulunda huo uchaguzi lazima awajibike kwanza yeye na wengine wafuate,” alisema. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Joel Mmasa, alisema anashangazwa mpaka sasa kwanini Waziri Ghasia hajachukua hatua za kujiuzulu wakati anafahamu kuwa yeye ndiye chanzo cha kuvurugika kwa uchaguzi huo. Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Umoja Mashirika yasiyo ya Kiserikali (Ungo), Malupo Maliki, alisema kuwa Waziri Ghasia asitake kukwepa tatizo la kuvurundwa kwa uchaguzi huo wa Serikali za mitaa na vijiji kwa kuwa ofisi hiyo ndio ilipewa jukumu hilo na wao waliamua kushusha katika ngazi za Halmashauri ambazo ndio wanazozisimamia. Alisema kuwa suala la uchaguzi huo lilishafahamika kwa muda mrefu na wizara hiyo kupewa majukumu hivyo walipaswa kujipanga ili kufanikisha, lakini matokeo yake zimejitokeza dosari nyingi ikiwamo ya baadhi ya vituo kupangiwa mawakala wachache wakati kuna idadi kubwa ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura.
DODOMA
WANANCHI wa kada tofauti mkoani Dodoma, wamemtaka Waziri Ghasia, ajiuzulu kutokana na uzembe uliosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Mkazi wa Tabata Mtambani, Daniel Ngowi, alihoji ushahidi unaosubiriwa na waziri huo ni upi wakati hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam uchaguzi umeshindikana kufanywa kutokana na alichokiita uzembe. “Hapa kwetu wameleta fomu hazina majina ya wagombea wa ujumbe kwa tiketi ya Chadema, waliwezaje kuchapa fomu na kuidurufu bila kuihakiki kwanza? Hicho ni nini kama siyo uzembe? Anataka hili nalo liundiwe tume? ajiuzulu tena bila kuchelewa,” alieleza Ngowi. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Emmanuel Kilatu, alielezea kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo kuwa kwa ujumla zimetokana na maandalizi mabovu. Alisema kauli zilizotolewa na viongozi wa Tamisemi, ni kukwepa aibu kwasababu mwenye mamlaka ya kuwajibisha wakurugenzi wa halmashauri siyo Tamisemi bali Waziri Mkuu.
Alisema, ikiwa Waziri Ghasia ameona umuhimu wa yeye kuwajibika ikiwa itathibitika, hana haja ya kusubiri kwa sababu tayari wilaya tatu zimethibitika kuahirisha chaguzi na kwamba huo ni uthibitisho tosha kwamba kuna uzembe umefanyika. “Hata Mwinyi (Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi) alipojiuzulu baada watumishi kwenye wizara yake kuua watu, haikumaanisha kuwa yeye alipiga risasi mtu, bali aliangushwa na watu wake vivyo hivyo Ghasia awajibike kama alivyosema kwani siyo siri kwamba watu wake wamemwangusha,” alieleza Kilatu.
MWANZA
WANANCHI wa Jiji la Mwanza kwa upande wao wamesisitiza Waziri Ghasia ajizulu kwasababu wananchi wengi wamekosa haki ya kuchagua viongozi wao kutokana na kasoro zilizojitokeza. “Waliamini hii mbinu ya kuwahisha uchaguzi itawapa wakati mgumu wapinzani, lakini badala yake wamesababisha matatizo chungu mzima…hata hii taarifa ya Waziri Ghasia (Tamisemi), haina maana yoyote zaidi yakutakiwa kutangaza kujiuzulu,” alisema mwanasheria William Bernad. Bernad alisema waziri Ghasia alitakiwa awe wa kwanza kujiuzulu kutokana na awali kutangaza maandalizi yote yamekamilika na uchaguzi utafanyika bila kuwapo na kasoro. Naye John Nyalapa mkazi wa Kiseke jijini Mwanza, alisema serikali ilifanya haraka kutangaza uchaguzi kufanyika Desemba wakati ikiwa haijajipanga. “Wangejiandaa hizi kasoro zilizojitokeza zisingekuwapo, serikali ilikurupuka kutangaza uchaguzi huo kufanyika mapema ukilinganisha na maombi ya wapinzani ufanyike Februari mwakani,” alisema Nyalapa. Hata hivyo, alisema ili kuepukana na migongano na vurugu katika uchaguzi ujao, lazima serikali ijipange vizuri kwa kufikisha vifaa kwa wakati vituoni.
GEITA
Peter Ngelela mkazi wa Geita alisema watendaji waliohusika na uzembe na kushindwa kuwajibika wakiwamo wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya husika wawajibike. “Ni wakati wa kutoleana uvivu na si kubebana, maandalizi ya uchaguzi huu yalifayika mapema na wizara husika (Tamisemi) iliwahakikishia wananchi kila kitu kipo vizuri, sasa hili lililotokea nani kafanya,” alihoji Ngelela. Alitoa mfano wa jimbo la Buchosa lililopo wilayani Sengerema kutofanya uchaguzi huo kutokana na kushindwa kufikiwa na vifaa vya kupigia kura wakati tangu awali tarehe husika ikifahamika. Ngelela alisema haingii akilini kuambiwa mzabuni wa kutengeneza karatasi za kupigia kura anapatikana Mwanza wakati Sengerema ni wilaya kubwa ambayo vifaa kama hivyo vinaweza kupatikana kwa urahisi. Naye Asnath Mussa wa mjini hapa, alisema mchakato wa uchaguzi huo utakuwa fundisho kwa Tamisemi, lakini kubwa ni kuadhibiwa wale wote waliosababisha uzembe na kasoro kuonekana. “Inawezekana kulikuwa na ajenda za siri ili kuvuruga uchaguzi huo…sasa ni wakati wa kuwajibika waliosababisha uzembe huo,” alisema Mussa. Kwa upande wake Juma Nyangi alisema vituo vingi ambavyo havikupiga kura, vitasababisha kuathiri kisaikolojia wagombea ambao wataingia katika kinyang’anyiro cha ‘kiporo’.
SHINYANGA
Baadhi ya wananchi wa mkoani Shinyanga, walisema uchaguzi huu umefanikiwa kwa robo tatu kutokana na watu kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka licha ya kasoro zilizojitokeza. Akizungumza na NIPASHE jana, Wenceslaus Modesi, alisema katika kasoro hizo majina ya wagombea wa vyama vya upinzani ndiyo yalionekana na dosari ukilinganisha na wagombea wa chama tawala, kwa kuchanganywa nyadhifa ama majina kupelekwa kituo kingine.
Hata hivyo, alisema uchaguzi huo umefanyika mapema mno kabla ya kufanyika maandalizi na maboresho yake, hivyo kusababisha kuibuka kwa matatizo mengi. “Uchaguzi huu ulikuwa na maandalizi ya zimamoto, hizi kasoro zilizojitokeza zilikuwa zimepangwa ili chama tawala kipitishe wagombea wake kwa urahisi, lakini mambo yamewashika,” alisema Saganda Saganda.
Naye Mkurugenzi wa Tamisemi, Khalist Luanda, akizungumza katika kipindi cha kumepambazuka kinachorushwa na Redio One, alisema sehemu kubwa ya uchaguzi huo imefanyika bila kuwepo kasoro, lakini vyombo vya habari vinaripoti maeneo tu ambayo kasoro zimejitokeza. “Vyombo vya habari vinaripoti kasoro tu zilizojitokeza, lakini ukifanya tathmini sehemu kubwa uchaguzi umefanyika vizuri ukilinganisha na maeneo ambako kumetokea matatizo,” alisema. Sagini alisema Wilaya za Kariua, Kasulu na Mkuranga, zimepelekewa wataalamu kutoka wizarani ili kuhakikisha uchaguzi utakaorudiwa Jumapili ijayo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment