Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia imeiagiza mikoa yote nchini kuwasilisha taarifa kuhusu
kasoro zilizojitokea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa juzi ili
iwachukulie hatua watendaji watakaobainika kuhusika.
Imesema kushindwa kusimamia uchaguzi na
kusababisha kasoro, ni moja ya makosa makubwa na kuwa watakaobainika,
watachukuliwa hatua kali kulingana na uzito na kiwango cha kuhusika kwao
na kwamba wanaweza kufukuzwa kazi, kuvuliwa madaraka, kushushwa cheo au
kukatwa mishahara.
Uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi na
kuahirishwa katika baadhi ya maeneo kutokana ama kukosekana kwa majina
ya wagombea, baadhi yao kuwekewa nembo za vyama wasivyotoka au uhaba wa
vifaa vya kupigia kura. Hata hivyo, halmashauri 145 kati ya 162
zilizofanya uchaguzi huo hazikuwa na dosari, tatu hazikufanya uchaguzi
kabisa kutokana na vifaa kuchelewa, 14 zilikuwa na kasoro katika baadhi
ya vijiji, vitongoji na mitaa na uchaguzi wake kuahirishwa mpaka Desemba
20 na 21. Akitoa taarifa ya awali ya uchaguzi huo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema pamoja na kasoro
hizo, uchaguzi huo umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80. “Katika uchaguzi huu hakukuwa na vitambulisho vya
mpigakura kama ilivyo katika Uchaguzi Mkuu. Uchaguzi huu unafanyika
katika mtaa au kitongoji hivyo ni rahisi watu kutambuana na pia mtu
akishapiga kura si rahisi kurudia mara ya pili na tuliagiza mpigakura
awe ama na kitambulisho cha kazi, leseni au kile cha kupigia kura katika
Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kutambulika,” alisema. Alisema malalamiko na kasoro zilizoripotiwa katika
vyombo vya habari haziwezi kujibiwa wala kutolewa ufafanuzi na Tamisemi
hadi baada ya kupata ripoti kutoka mikoani. Akizungumzia malalamiko ya wananchi kutoyaona
majina yao, Ghasia alisema ulitolewa muda wa siku tatu kwa wananchi
kufanya uhakiki lakini wengine hawakufanya hivyo. “Kuhusu majina kubadilishwa au kuisha kwa wino na
kukosekana kwa vitu vidogovidogo hilo linaweza kuwa limefanyika kutokana
na uzembe tu. Ndiyo maana tumeagiza tupewe taarifa rasmi.” Akizungumzia kasoro zilizobainika katika karatasi
za kupigia kura, alisema utaratibu wa kuandaa vifaa hivyo ulikuwa
ukifanywa na halmashauri husika na si Tamisemi, hivyo ni vigumu kwa
wizara hiyo kuagiza walioandaa vifaa wachukuliwe hatua. “Mfano Temeke na Ilala walimtumia Mpigachapa Mkuu
wa Serikali. Awali, aliwapelekea vifaa vyenye matatizo, hata
walipovirejesha ili avirekebishe, vilirudishwa vikiwa bado na kasoro.
Mpiga Chapa aliingia mkataba na manispaa na ndiyo aliyepewa zabuni,”
alisema. Alisema suala hilo linafanyiwa uchunguzi ili
kubaini kama kasoro katika wilaya hizo zimesababishwa na Mpiga Chapa wa
Serikali au wilaya husika. Alipotafutwa mpiga chapa mkuu wa serikali, Cassian
Chibogoyo kuzungumzia kuhusu tuhuma za ofisi yake kuwa sehemu ya dosari
za uchaguzi katika manispaa za Ilala na Temeke, alisema tuhuma
amezisikia na kwamba atawasiliana na wizara kabla ya kutoa majibu yake
leo. Ghasia alipoulizwa kama yuko tayari kuwajibika, alijibu, “Kama
ikibainika kuna halmashauri imefanya vibaya katika uchaguzi huu kwa
sababu yangu nitakuwa tayari kuwajibika. Tamisemi tulijipanga kimkoa pia
ilikuwa ngumu kwa kila kituo cha kupigia kura kuwa na polisi.
Tutahakikisha kasoro hizi hazitokei katika mitaa ambayo uchaguzi
utarudiwa,” alisema. Aliitaja mikoa ambayo haikuwa na dosari katika
uchaguzi huo kuwa ni Arusha, Mbeya, Kagera, Njombe, Singida, Lindi,
Ruvuma, Katavi, Geita, Iringa, Dodoma na Mtwara.
Mikoa yenye kasoro
Alisema mikoa ambayo baadhi ya halmashauri
zimeahirisha uchaguzi katika baadhi ya maeneo ni Kilimanjaro, Manyara,
Morogoro, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Mwanza, Tabora, Tanga, Mara, Rukwa,
Dar es Saalam na Pwani. Mkoa wa Kilimanjaro uchaguzi haukufanyika katika
kata nne za Ngoyo, Holili, Chela na Kindikati zilizopo Halmashauri ya
Wilaya ya Rombo pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Hai katika Kata ya
Machame Kaskazini. Mkoa wa Manyara uchaguzi haukufanyika katika Kata
nane za Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ na Halmashauri ya Mbulu katika
kata nne za Gehandu, Bargish, Yaedampa na Maretadu. Mkoa wa Morogoro ni Halmashauri ya Ulanga katika
kata nane za Mtimbila, Usengule, Chilombola, Itete Njiwa, Ruaha, Ilagua
na Sofi na Kata ya Dakawa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero. Mkoa wa Shinyanga ni kata za Nyaya, Mtombo,
Bulyangulu, Bulige, Mwaketa, Kashishi, Ikinda na Bugala zilizo
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Mkoa wa Simiyu ni kata za Lamadi, Igalukilo,
Malili na Mkula zilizopo ni Busega pamoja na Kata ya Mbita iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima. Mkoa wa Kigoma ni halmashauri nzima ya Kasulu na
Mkoa wa Mwanza ni kata 18 za Halmashauri ya Kwimba na kata 28 za
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema. Mkoa wa Tabora uchaguzi umeahirishwa katika
halmashauri yote ya Kaliua. Pia katika kata za Wela, Buge, Janija,
Milambo Itogo na Mwakanshahagha zilizopo Nzega. Katika Mkoa wa Tanga uchaguzi umeahirishwa katika kata 20 za
Magoloto, Kicheba, Msozwe, Magilla, Mlingano, Pandedarajani, Ngomeni,
Pungwe, Kumba, Bwembela, Topwe, Lusanga, Mpapaya, Mhamba, Songe,
Kasungo, Mtindilo, Kilulu, Mkuzi na Kwakifua. Mkoa wa Mara ni katika Kata ya Mihingo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Kata 13 za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Mkoa wa Rukwa ni katika Kata za Momoka, Msua,
Ntendo, Mafulala, Sumbawanga, Izia, Chanji na Kizwite za Halmashauri ya
Manispaa ya Sumbawanga. Mkoani Dar es Salaam uchaguzi haukufanyika katika
kata nne za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na mitaa kadhaa katika
Manispaa ya Ilala na Pwani ni katika Halmashauri yote ya Wilaya ya
Mkuranga.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment