
Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi
Maarufu kwa jina la Mr. II Sugu, amewataka wananchi mkoani Mbeya
kuwashusha kwenye magari ya Serikali viongozi wa umma ambao wanavaa sare
za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kupanda magari hayo na kuzurura
nayo mitaani.
Sugu alitoa wito huo juzi wakati akihutubia wananchi wa Kyela katika
mkutano ambao uliandaliwa maalum kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa
kuchagua wenyeviti wengi wa Serikali za Mitaa wa Chadema kiasi cha
kukiwezesha chama hicho kuongoza Halmashauri ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa
Kyela.Alisema kuwa kumekuwapo na baadhi ya viongozi wa Serikali hususani Wakuu wa Wilaya ambao wanatumia vibaya rasilimali za umma kwa manufaa ya CCM badala ya masilahi ya wananchi wote. Alisema kuwa kuanzia sasa wananchi wenyewe wanastahili kulinda mali zao kwa kuwazuia viongozi wa aina hiyo kutumia magari ya umma kwa maslahi ya CCM.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa Mkuu wa Wilaya kuvaa sare za CCM kisha anapanda gari la Serikali, mukimuona Mkuu wenu wa wilaya hapa amefanya hivyo, mshusheni kwenye gari la Serikali mara moja,” alisema Sugu.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Sugu alichafua hali ya hewa katika jimbo hilo la Kyela ambalo linaongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, baada ya kupokewa kwa maandamano makubwa, huku wananchi hao wakiimba nyimbo mbalimbali za kumdhihaki Dk. Mwakyembe.
Mapokezi hayo yalisababisha shughuli za wakazi wa mji huo kusimama kwa muda, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa barabara kuu ya Kyela – Itungi kwa takribani saa moja kupisha msafara wa maandamano ambayo hayakuwa rasmi kutokana na kutokuwa na kibali cha Polisi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment