Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Margret Zziwa akisikiliza
uamuzi wa jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ)
wakati wa kesi yake Arusha jana.
Spika wa Bunge la
Afrika Mashariki (EALA), Dk Margret Zziwa huenda akang’olewa kwenye
nafasi yake katika kikao cha dharura cha Bunge hilo kinachofanyika
jijini Arusha leo.
Bunge hilo linakutana leo baada ya Mahakama ya
Afrika Mashariki (EACJ), kutupilia mbali maombi ya Spika Zziwa ya zuio
la muda dhidi ya kikao hicho kinachotarajiwa kupokea, kujadili na kuamua
taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Spika kutoka Kamati ya Sheria,
Kanuni na Madaraka ya Bunge.
Jopo la majaji watano wa EACJ, chini ya Jaji
Kiongozi, Jean Bosco-Butasi, lilitupa maombi hayo baada ya Spika Zziwa
kupitia kwa wakili wake, Jet Tumwebaze kushindwa kuishawishi mahakama
kuhusu madhara atakayopata iwapo kikao hicho kingefanyika.
Katika maombi yake, Spika Zziwa licha ya kudai
hoja ya kumwondoa madarakani inakiuka Katiba ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) baada ya Bunge kumteua Chris Okumu kuwa kaimu spika,
cheo ambacho hakipo kwenye Katiba. Spika huyo pia anadai kikao cha leo hakiko kwenye
kalenda ya vikao vya Eala na kwamba, amekuwa mtumishi wa umma kwa muda
wa zaidi ya miaka 14, hivyo kitendo cha kumwondoa madarakani
kitamshushia hadhi na kumletea madhara yasiyolipika.
Akisoma uamuzi wa Mahakama kwa niaba ya majaji
wenzake, Jaji Isaac Lenaola kutoka Kenya alisema kifungu cha 53(3) cha
Mkataba wa EAC, kimeweka utaratibu wa wabunge kumwondoa madarakani spika
wao na mahakama kama moja ya mihimili, haiwezi kuingilia suala hilo.
“Ni jukumu la mlalamikaji kuthibitisha kuwa
madhara atakayopata hayawezi kurekebishika katika shauri hili, lakini
mlalamikaji ameshindwa kuishawishi mahakama. Mahakama inajielekeza kuwa
madhara atakayopata mlalamikaji iwapo ataondolewa, yanaweza kulipika kwa
fedha kutegemeana na shauri alilolifungua mahakamani,” alisema Jaji
Lenaola. Majaji wengine waliosikiliza ombi hilo ni Fakihi Jundu (Tanzania), Monica Mugenyi (Uganda) na Faustin Ntezilyayo (Burundi). Jopo la majaji hao pia limepanga kusikiliza ombi la msingi kwenye keshi hiyo Februari 3, mwakani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment