
Katuni
Tathmini mbalimbali zimetolewa juu ya mchakato mzima
wa uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji uliofanyika Jumapili
Desemba 14, mwaka huu.
Ukiachilia mbali vurugu na matumizi ya nguvu za dola, uchaguzi huo
ulikuwa na dosari kubwa ambayo imesababisha wilaya tatu na kata 127
kushindwa kufanya uchaguzi.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
–Tamisemi, Hawa Ghasia, ikiwa ni wizara yenye dhamana ya usimamizi wa
uchaguzi huo juzi ilithibitisha kuwako kwa kasoro hizo na kutofanyika
kwa uchaguzi katika maeneo hayo.Jana katika safu hii tulisema kuwa ni vema kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo zikafanyiwa kazi ili kusaidia taifa hili walau kuwa na sifa ya kuendesha uchaguzi huru na wa haki kwa vigezo vya kimataifa.
Hata hivyo, wakati tukijua vilivyo kuwa wahusika wakuu wa suala hili ni Tamisemi, Waziri Ghasia, akizungumza kwa niaba ya mwenye ofisi hiyo, yaani Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni kutokana na kasoro mbalimbali ikiwamo kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura vituoni. Pia alisema kasoro nyingine ni karatasi ya kupigia kura katika nafasi ya mwenyekiti wa kijiji kuunganishwa na nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji, nembo za vyama kuwekwa kwa mgombea wa chama kingine, majina ya wagombea kukosewa, kukosekana kwa majina ya wagombea, karatasi za kupigia kura kuwa chache kuliko idadi ya walioandikishwa na kukosekana kwa majina ya wapigakura.
Alitoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu uchaguzi umeahirishwa kwa sababu ya kuchanganya karatasi za kupigia kura mfano karatasi za Kata X kupelekwa kwenye Kata Y. Wilaya ya Kaliua uchaguzi umeahirishwa kwa sababu ya ucheleweshaji wa vifaa na kasoro katika karatasi za kupigia kura.
Ghasia alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga haikufanya uchaguzi kwa sababu ya ucheleweshaji wa vifaa na mchanganyiko wa majina. Kutokana na udhaifu uliodhihirika alisema kwamba watakaobainika kufanya uzembe na kusababisha dosari kwenye uchaguzi huo watachukuliwa hatua kali ikiwamo kukatwa mshahara, kushushwa cheo au kufukuzwa kazi. Ingawa Ghasia alisema kuwa tamko hilo linatokana na taarifa ya awali ya yaliyojitokeza, pia mikoa imetakiwa iwasilishe taarifa rasmi na kamilifu kuhusu kilichojitokeza katika Halmashauri, ili Wizara izichambue kubaini wote waliosababisha kasoro, hivyo hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Kulingana na taarifa ya Waziri Ghasia, halmashauri 145 zimefanya uchaguzi huo bila dosari, Halmashauri 15 ndizo zenye kasoro kwenye baadhi ya maeneo na tatu hazijafanya kabisa na kuahidi kwamba uchaguzi huo utafanyika Jumapili ijayo. Kwa maana hiyo, Halmashauri za Wilaya na idadi ya Kata ambazo zitarudia uchaguzi Jumapili ijayo alizitaja kuwa ni Rombo (4), Hanang' (8), Mbulu (4), Ulanga (8), Mvomero (1), Msalala (8), Busega (4), Itilima (1), Kwimba (18), Sengerema (28), Muheza (20), Bunda (1), Serengeti (13), Sumbawanga (8) na Temeke (4).
Ukisikiliza kwa makini kauli ya Waziri Ghasia ni kama yeye na Waziri Mkuu Pinda na wizara nzima wametimiza wajibu wao. Tatizo kwa maelezo na uelewa wake uko chini kwenye halmashauri. Ingawa ni kweli kwamba halmashauri ndizo zilikuwa na wajibu wa kusimamia moja kwa moja uchaguzi huo, bado Waziri Ghasia anasahau kuwa Tamisemi ndiyo yenye dhima yote ya usimamizi wa uchaguzi huo.
Kwa jinsi hiyo, haieleweki ni kwa jinsi gani Ghasia na Pinda wanavuka kigingi hiki cha uzembe, kutokuwajibika na kwa kweli kukataa kusikiliza ushauri wa wadau mbalimbali kuhusu muda wa kufanyika kwa uchaguzi huo. Aliyetoa tangazo la uchaguzi huo ni Waziri Mkuu Pinda, alijua kwamba muda wa kutosha wa kujiandaa haukuwako. Alijua wazi kwamba wadau mbalimbali walikuwa wameshauri kwamba uchaguzi huo ufanyike mwakani, lakini hawakujali. Walipuuza na walitumia tu mamlaka yao kuitisha uchaguzi huo na mwishowe madudu haya yanatokea mbele yao. Kila tunapotafakari tunashindwa kujua katika mazingira ya kuvurugika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji katika maeno hayo hapo juu, matumzi ya fedha za kodi za wananchi, usumbufu kwa wananchi vyote vikionyesha uzembe wa dhahiri wa Tamisemi, hivi wakuu wa wizara hii wanabaki kwenye ofisi ya umma wakisubiri nini? Ni wakati wa kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika nchi hii ili tukwamuke hapa tulipokwama.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment