Wakaazi wa Pakistan wanaomboleza msiba wa siku tatu na kuandaa mazishi
ya jumla jamala ya wahanga wa shambulio la kishenzi la kundi la
wataliban katika shule moja ya mji wa kaskazini magharibi -Peshawar.
Wapakistan wanaomboleza baada ya shule ya Peshawar kuvamiwa na watoto kuuliwa na wataliban
Sala za maiti zimefanyika kote nchini na katika shule huku wanafunzi
wakielezea jinsi walivyopata mshituko kutokana na mauwaji hayo ambapo
wanamgambo sabaa wa Taliban waliojifunga miripuko viunoni walivyoparamia
ukuta na kuingia katika shule hiyo inayosimamiwa na jeshi .
Wanafunzi walipigwa risasi na baadhi ya waalimu wakike walitiwa moto wakiwa hai.
Serikali imetangaza siku tatu za msiba kuanzia leo.Mazishi yameanza
tangu jana usiku lakini yale ya wanafunzi 132 na waalimu na watumishi
wengine 10 wa shule hiyo yanafanyika leo.Wanafunzi wengine 121 na
waalimu wengine watatu wamejeruhiwa.
Makatili hawana Dini
"Wametumia dakika tu kuangamiza kilicho muhimu nilichotumia
maisha yangu yote kukiimarisha,mwanangu wa kiume" amesema Akhtar
Hussain,anaefanya kazi ya kibarua huku machozi yakimtiririka,alipokuwa
anamzika mwanawe mwenye umri wa miaka 14,Fahad .
Mwenzake Mohammed Saleem anasema:"Msiba mkubwa huu kwetu sote.Hakuna sio
sisi waislam na hata wale ambao si waislam anaeuwa watoto.Hawana dini
yoyote hawa."
Shambulio hilo limelaaniwa na ulimwengu mzima.Hata wanamgambo wa Taliban
katika nchi jirani ya Afghanistan wamelaani mauwaji hayo na kusema
hayaambatani na mwongozo wa dini ya kiislam.
Serikali ya waziri mkuu Nawaz Sharif imesema inapanga kurejesha tena
adhabu ya kifo kwa kadhia zinazohusiana na ugaidi.Sheria hiyo ya adhabu
ya kifo ilibatilishwa tangu mwaka 2008.Tangu wakati huo mtu mmoja tu
ndie aliyeuliwa,mwanajeshi aliyekutikana na hatia na korti ya kijeshi na
kunyongwa novemba mwaka 2012. Waziri mkuu Nawaz Shariff ameahidi kuendelea na opereshini za kijeshi
wakisaidiwa na ndege zisizokuwa na rubani za kimarekani dhidi ya
wanamgambo wa Taliban. "Tutazingatia kila tone la damu la watoto wetu"amesema waziri mkuu wa Pakistan kabla ya kukimbilia Peshawar hapo jana.
Wahanga wa Peshawar wanakumbukwa pia India
Katika nchi jirani ya India ambako viongozi daima walikuwa
wakiituhumu Pakistan kuwaunga mkono wapiganaji wa chini kwa chini
wanaoipinga serikali ya New Delhi,wanafunzi katika shule zote walikaa
kimya dakika mbili hii leo kuomboleza mauwaji ya wanafunzi wenzao wa
Peshawar.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment