
Imani ya Watanzania wengi ni kuwa Serikali,
kupitia vyombo vunavyosimamia sekta ya elimu, imekuwa ikijipanga vilivyo
kuondoa madudu mbalimbali yanayoitia doa sekta hiyo mama.
Hivi ndivyo watendaji mbalimbali wa Serikali
wanavyojisifu mara kwa mara, wakituaminisha wananchi kuwa sasa mambo ni
shwari katika sekta ya elimu.
Lakini hali inaonekana kuwa si shwari. Taarifa
mpya ambayo gazeti hili limeichapisha jana inatupa wasiwasi wananchi
kuhusu mikakati ya Serikali ya kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili
sekta ya elimu.
Jana tuliandika katika gazeti hili kuwa wahitimu
344 waliomaliza darasa la saba mwaka huu mkoani Arusha, wamebainika kuwa
hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Kati yao wavulana ni 181 na
wasichana ni 163.
Bila shaka hii ni taarifa ya kustua hasa kwa
kuzingatia kuwa wengi tulifikiri tatizo la watoto kumaliza elimu ya
msingi bila ya kuwa na stadi hizi muhimu, lilishapatiwa ufumbuzi.
Tulifikiri hivyo kwanza kwa sababu ya kauli za viongozi wa Serikali na
pili kutokana na mikakati tuliyoshuhudia Serikali ikichukua kwa
watendaji wa shule ambazo mwaka 2011 zilibainika kuwa na wahitimu
wasiojua kusoma na kuandika.
Kwa kukumbushia ni kuwa Aprili mwaka 2012, Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini kuwapo kwa wanafunzi wa
sekondari 5,200 waliokuwa hawajui kusoma na kuandika. Wanafunzi hao
walikuwa sehemu ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2011. Kilichofuatia
ni kuwa walimu katika shule husika walichukuliwa hatua za kinidhamu kama
vile kuhamishwa shule na adhabu nyingine.
Wengi tulifikiri huu ulikuwa mwanzo wa Serikali
kujipanga kuhakikisha tatizo hili halijitokezi tena na hata likijitokeza
sio kwa ukubwa kama tulioushuhudia katika taarifa ya Arusha. Huu ni
mkoa mmoja tu ambao mpaka sasa angalau umetoa taarifa zake kuhusu
matokeo ya darasa la saba.
Ni dhahiri, hasa kwa kuzingatia hali ilivyo, matokeo katika mikoa mingine yanaweza kushabihiana na yaliyotokea Arusha.
Ukiondoa taarifa hii ya Arusha na ile ya mwaka
2012, ziko taarifa za mara kwa mara zinazoonyesha ukubwa wa tatizo hili.
Kwa mfano, mwaka 2010, asasi ya Twaweza ilitoa ripoti ya utafiti
iliyobainisha kuwa kati ya wahitimu watano wa darasa la saba, mmoja
hawezi kusoma hadithi ya kiwango cha darasa la pili.
Utafiti huo ulioitwa kwa Kiingereza ‘Are Our
Children Learning’ (Je, Watoto Wetu Wanajifunza), ulishirikisha sampuli
ya watoto 42,033 kutoka kaya 22,800 nchi nzima.
Baada ya matokeo haya ya Twaweza na hata yale ya
mwaka 2012, matarajio ya wengi ni kuwa Serikali ingestuka na kuweka
mikakati makini, lakini tunasikitika kupaza sauti kuwa hali haijawa
hivyo; tatizo linaendelea. Kilichotokea Arusha mwaka huu ni sehemu ya udhaifu
wa wahusika kutolishupalia tatizo hilo. Baadhi ya matukio hapa nchini
yanatupa wasiwasi kuwa huenda kuna mkakati maalumu wa kuacha hali hii
iendelee ili wachache wanufaike kwa kutumia migongo ya wale wanaokosa
elimu.
Kwa mfano, tunajiuliza kwanini wajumbe walio wengi wakati ule wa
Bunge Maalumu la Katiba, walipitisha kipengele cha elimu kwa wabunge
kuwa darasa la saba badala ya kidato cha nne kama ilivyopendekezwa
katika rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba?
Jambo moja ni dhahiri kuwa kuna watu katika
uongozi wa siasa wanaoridhika na hali hii. Kwao elimu sio muhimu, ndiyo
maana hawaguswi na matatizo yetu ya msingi kama hili la kuwa na wahitimu
mbumbumbu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment