Matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za
Mitaa yanaonyesha vyama vya upinzani vimevunja ngome za CCM kwa kupata
ushindi katika maeneo mengi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili
iliyopita umeacha alama isiyofutika katika maisha ya Watanzania –
watawala na watawaliwa. Utadhani uchaguzi ulilenga kutangaza kuwa, ni
‘uhalifu mchafu’ kwa chama kimoja kudumu madarakani kwa miaka 53; kana
kwamba hakuna watu wengine wenye akili nchini.
Mijini na vijijini, vyama vya upinzani vimezoa
ushindi, wenyeviti na wajumbe, tena kwa kura nyingi na maeneo mengine,
kupita kwa mbali. Hakika katika miaka 23 tangu kurejeshwa kwa mfumo
wa vyama vingi, wananchi hawajawahi kushuhudia vyama vya upinzani
vikikomba kura na viti katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kiwango
cha matokeo ya uchaguzi wa Jumapili iliyopita. Tunachoshuhudia kwa miaka yote hiyo, ni CCM
kuendelea kutawala kwa sheria, kanuni, utaratibu na tabia za mfumo wa
chama kimoja – ubabe mtindo mmoja. Sasa ujasiri huu umetoka wapi?
Tume ya Nyalali
Wakati Tume ya Jaji Francis Nyalali (1992)
ikitafuta maoni ya wananchi juu ya mfumo upi utumike wa chama kimoja au
vingi, wengi waliripotiwa kuonyesha kutaka chama kimoja.
Akifafanua, Jaji Nyalali aliwaacha watu wengi hoi
aliposema: wengine walikuwa wanasema hawataki vyama vingi kwa kuwa kile
kimoja kilichokuwapo kilikuwa tayari kimewachosha kwa kuwatoza kodi
nyingi.
Kwahiyo wengi na hasa vijijini, walidai kuwa, kama
kimoja kimewatisha, kimewakamua kwa kodi kiasi hicho je, vikiwa vingi
watakimbilia wapi? Woga huu ulikolezwa na watawala ambao hawakupenda
mfumo wa vyama vingi; hivyo kuendelea kufanya woga kuwa moja ya mitaji
mikuu ya watawala ya kutumia kujichimbia madarakani. Pamoja na woga unaotokana na ubabe na vitisho;
watawala wamekuwa na mitaji mingine miwili: ujinga na umaskini ambavyo
vimewasaidia pia kuzima kauli na vitendo vya wananchi kuendeleza
ukondoo. Sasa tusemeje kuhusu ‘moto wa tsunami’ wa Jumapili uliotishia
majigambo na ndweo za CCM na kupeleka msiba katika mahekalu ya watawala? Je, hirizi la watawala limeoza? Au ‘mganga’ wa watawala amefariki dunia na wao hawawezi kukumbuka alikowazindikia? Tsunami ya Jumapili inatokana na mwamko wa wananchi na ujasiri wa kusema, ‘sasa basi;’ ambao umesababisha wengi kuikataa CCM.
Ujasiri huu umetokana na nini? Hebu tuangalie katika maeneo matatu ambayo wananchi wamekuwa wakifutikwa. Kwanza, hirizi la ujinga limeanza kuyeyuka. Kuwapo kauli za wazi, zinazopingana na mfumo uliotawala kwa zaidi ya nusu karne. Kuwapo kwa vyombo vya habari vyenye kuandika
ukweli bila woga wala upendeleo; kumebomoa kuta za siri na kumewapa
wananchi silaha ya ufahamu. Si hivyo tu, vyombo hivi na taarifa zake, vimewapa
wananchi uwezo wa kudadisi na kujitafutia. Vimechochea kufikiri na
kuchambua. Uelewa umetandawaa. Pili, umaskini ungalipo. Wengi wanaishi kwa “mbinu
za kujikimu.” Katika kutafuta kusikoleta nafuu – mchana, usiku –
hatimaye wanakaa na kujiuliza, nani anakula hata kile kidogo
tunachopata?
Rasilimali za Taifa
Nani anakula dhahabu? Nani anakula Tanzanite? Nani
anakula almasi? Nani anameza gesi? Nani anachukua mazao yetu bila
kutulipa? Wanahoji. Wanabomoa ngome ya ujinga ili kupambana na umaskini.
Tatu, sasa wananchi wameanza kuwa na woga wa
kuogopa. Tuseme hivi: Wanaogopa kuogopa kwani kuogopa kumewadidimiza
katika utumwa wa wengine. Leo hii wananchi wanaaza kuwa na ujasiri wa
kuhoji: nani ameiba fedha za kodi ya wananchi. Nani amechota mabilioni
ya shilingi kutoka Benki Kuu (BoT). Nani ameibia shirika la umeme
nchini, Tanesco. Nani anauza wanyama hai kutoka mbuga za Taifa. Wanakwenda mbele zaidi. Wanauliza hayo yanatendekaje wakati
Serikali hujigamba kuwa ni “mkono mrefu?” Wakati polisi hujinadi kuwa
walinzi wa raia na mali zao? Hapa ndipo wanagundua mengi, kama siyo
yote, kwamba yanatendwa na walioko madarakani. Wanasikiliza “sauti iliayo nyikani” ile ya
wapinzani; tena mara hii ikitafuta umoja wa dhati ili kukabiliana na
watawala wasiopenda kustaafu au kung’oka kutokana na kashfa za wizi,
ufisadi, ubabe na uvunjaji Katiba na haki za binadamu. Wananchi wanapata uelewa na maarifa. Wanasikiliza
wasomi huru na wengine wenye ukomavu katika nyanja mbalimbali za taaluma
na maisha. Wanaerevuka. Acha iwadie siku ya uchaguzi. Wanathubutu kutenda.
Wanafanya hivi: Nataka huyu; sitaki yule. Na katika uchaguzi wa
Jumapili, wale waliopata nuru, wameonyesha wanachotaka na wasichotaka. Mitaji mitatu mikuu ya watawala – ujinga, umaskini
na vitisho; ambayo imetumika kwa miaka mingi na imewaweka wananchi
wengi katika giza, sasa imeanza kutota. Tayari wananchi wamegundua kuwa wapo mahali walipo
kwa kuwa watawala ndio wanataka wawe pale, katika ujinga, umaskini na
woga usiomithilika; woga wa kuwafanya misukule. Kura za uchaguzi huu wa serikali za mitaa,
zinaelieleza taifa na dunia kuwa wananchi wanataka mabadiliko. Kwamba
wanachukia wanavyotawaliwa na hawataki kutawaliwa hivi hivi milele na
katika utumwa huu huu wa ujinga, umaskini na woga. Na nguvu hii ya wananchi haizuiliki. Fikiria
Serikali ilivyokalia taarifa juu ya uchaguzi huu; ilivyoleta taarifa
kama kitu cha dharura na ilivyoleta masharti ya kipuuzi kama mgombea
kuchora nembo ya chama chake. Fikiria jinsi halmashauri, chini ya Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) baada ya kunusa gharika
zilivyokataa hata kupeleka vifaa vya kupigia kura kilometa moja au mbili
kutoka ofisi kuu! Sasa kumekucha. Mshauri wa CCM asimung’unye
maneno. Awaambie kumekucha na hakuna awezaye kuzuia utashi wa wananchi.
“Andiko la Jumapili” iliyopita linasomeka vizuri ubaoni.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment