Social Icons

Pages

Thursday, December 11, 2014

NEC KUANZA UANDIKISHAJI WA DAFTARI MWEZI UJAO

Makamu Mwenyekiti wa Nec, Mahamoud Hamid
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza kuanza kwa zoezi ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura kuanzia Januari 30 hadi  Aprili 4, mwakani.
Aidha Nec imetangaza kuanza zoezi hilo Januari 30 katika mikoa yote nchini na kukamilika Februari 28 isipokuwa mikoa ya Zanzibar, Dar es Salaam, Morogoro na Pwani  ambayo zoezi litaanza Marchi 15 na kukamilika Aprili 14.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salam jana na Makamu Mwenyekiti wa Nec, Mahamoud Hamid, katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa, waliokutana kupeana taarifa kuhusiana kuanza kwa shughuli za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Kumekuwepo na wasiwasi juu ya kufanyika kwa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Napenda kuwahakikishia viongozi wa vyama vya siasa na umma kwa ujumla kuwa, mchakato umeanza na zoezi hili litafanyika kwa uangalifu mkubwa na linategemewa kukamilika katika muda uliopangwa,” alisema Hamid.
Alifafanua kuwa zoezi hilo lilishindwa kuanza Septemba mwaka huu, kama Nec walivyotoa taarifa kwa viongozi wa vyama vya siasa kutokana na kuchelewa kupatikana kwa fedha kutoka serikalini.
Alisema zoezi hilo litaanza baada ya fedha kupatikana na kwamba litatunguliwa na majaribio ya uandikishwaji kuanzia Januari 30 hadi Februari 28, mwaka huu.
Alisema, Nec imepanga kufanya zoezi la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voter Registation (BVR).
Alisema majaribio hayo yatafanyika katika majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Kawe Jijini Dar es Salaam, Kilombero mkoani Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.
 “Tunatarajia kuanza zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika maeneo yote nchini na tunatarajia kuwa daftari litakuwa tayari Aprili 28 mwaka 2015,” alisema Hamid. Hamid alisema Nec imepokea vifaa vyote muhimu vya uandikishaji na vifaa vya BVR 107 na kwamba wanatarajia kuendelea kupokea vifaa vingine wiki hii.
Alifafanua hatua nyingine itakayofuata ni pingamizi zitakazojitokeza zitashughulikiwa na taarifa za Wapiga Kura zitakazohitaji marekebisho zitashughulikiwa.
“Baada ya zoezi hili zima kukamilika tunatarajia kuwa Daftari hili litakuwa lemekamilika rasmi Aprili 28 mwaka 2015,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: