Pages

Thursday, December 11, 2014

NDUGAI: CHENGE, NGELEJA KUENGULIWA JANUARI 2015

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
Wenyeviti wa kamati tatu za kudumu za Bunge, watavuliwa rasmi nyadhifa zao Januari, mwakani, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 321 katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Wenyeviti hao ni Andrew Chenge wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Bajeti, Victor Mwambalaswa wa Kamati ya Nishati na Madini na William Ngeleja wa kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema ni lazima Bunge litekeleze maazimio ya Bunge kwa viongozi husika kuondolewa kwenye nafasi hizo.
“Wakati wa vikao vya Kamati za Bunge vitakavyofanyika Januari, mwakani, ndipo hatua zitachukuliwa kwa kila kamati husika kuchagua mwenyekiti wa kujaza nafasi ya viongozi hao…maamuzi ya Bunge lazima yatekelezwe na yatatekelezwa kabla ya Bunge la Januari 27, mwaka 2015,” alifafanua Ndugai.
Katika Azimio namba tatu lilisema kuwa, kwa kuwa katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco);
Na kwa kuwa, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao.
Katika mialama ya Benki ya Mkombozi, ilionesha Chenge alipewa kiasi cha Sh. bilioni 1.6, Ngeleja Sh. milioni 40.  Mwambalasu ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Tanesco ambayo inatuhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’).
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment