Kwa mataifa mengine sikukuu za mwisho wa mwaka
huwa ni za kutafakari yaliyotendeka ndani ya mwaka mzima na kujipanga
upya kwa mwaka unaofuata. Sina uhakika kama sisi Tanzania tunafanya hivyo.
Katika makala hii najaribu tu kidogo kuangalia mambo yanayoshangaza
ndani ya taifa letu na kujiuliza tatizo nini?
Ni wazi kuna mambo mengi tunayoyafanya vizuri, lakini kama mtu unataka kuendelea mbele ni lazima kuangalia pale unapojikwaa.
Tumemaliza sherehe za miaka 53 ya uhuru wetu. Ni vyema kusherehekea kwa mafanikio ama kwa kushindwa kufikia malengo.
Miaka 53 bado kuna mapungufu mengi, la kushangaza
hapa ni kwamba tumetumia fedha nyingi kwenye sherehe hizi wakati taifa
linayumba kiuchumi na kuna hatari bajeti isiweze kufikia mwisho wa mwaka
wa fedha. Kwa nini matumizi makubwa ya sherehe, wakati bado
kuna hitaji kubwa la kuboresha huduma za -kijamii? Je tatizo liko wapi
hapa? Ni uongozi? Ni kutokuwa na malengo ya mbali au hatuna wataalam wa
uchumi? Baada ya sherehe za uhuru tunawasikia viongozi wetu wakisema kwamba hali ya uchumi ni mbaya na maisha ni magumu!
Inashangaza baada ya kutumia fedha zote hizo
kwenye sherehe za uhuru tunalia kwamba maisha ni magumu. Huu ndio
utamaduni wetu wa kulalamikia ugumu wa maisha wakati tunateketeza fedha
kidogo tulizo nazo.
Tunalalamika maisha magumu wakati barabara zetu zimejaa magari hadi foleni hazitembei, magari hayo yanakunywa mafuta! Tunalalamika maisha magumu lakini watu wana simu
zaidi ya tatu, simu zote hizo zinakula fedha na kila ukipita watu wote
simu masikioni.
Tunalalamika ugumu wa maisha, wakati sehemu za
starehe na nyama choma watu wamejazana kibao, wanakula na kunywa, bei ya
bia inapaa na bei ya nyama inatisha.
Tunalalamika ugumu wa maisha wakati tunachanga
mamilioni ya fedha kufanya sherehe za arusi, na tunaendelea kulalamika
maisha magumu wakati majumba makubwa yanajengwa usiku na mchana!
Inashangaza!
Siku tatu zilizopita mvua ilinyesha kwa nguvu kubwa ndani ya
jiji la Dar-es-Salaam . Amini usiamini, baada ya saa moja mvua hii kubwa
kunyesha, nilishuhudia maeneo ya Tabata Chang’ombe watu wakienda
kununua maji ya chumvi na kuilaumu idara ya maji kwamba siku hizi haitoi
maji.
Inashangaza kabisa mvua kunyesha siku tatu mfulizo
na watu wakashindwa kuvuna maji ya mvua. Mtu anaweza kujiuliza: Je hapa
tatizo liko wapi?
Nyumba nyingi zimeezekwa kwa bati, mvua ikinyesha
maji yanatiririka kwenye bati, yanaingia barabarani, yanaharibu
barabara, yanaleta mafuriko. Tunashindwa kuyatumia maji haya, kupikia,
kuoga, kufua na kufanya shughuli nyingine.
Kule Rwanda, wametunga sheria ya maji ya mvua. Ni
kinyume cha sheria maji ya mvua kutiririka kwenda kwa jirani au kuingia
barabarani na kuleta uharibifu.
Kwa mujibu wa sheria kule Rwanda, kila mtu ni
lazima avune maji ya mvua. Sheria hii imesaidia watu kule Rwanda kupata
maji ya kutumia majumbani mwaka mzima, pia imesaidia kupunguza uharibifu
wa miundo mbinu na mafuriko. Nina imani kwamba kama nyumba zote za
Dar-es-Salaam zingekuwa na mfumo wa kuvuna maji ya mvua, ni wazi athari
ya mvua hizi ingekuwa ndogo.
Lakini jingine linaloshangaza ni madaraja kusombwa
na maji na barabara mpya ya Mandela, iliyofunguliwa juzi kwa mbwembwe
kubomoka. Mtu anaweza kujiuliza, madaraja haya yalijengwa
kwa kiwango gani? Na je hii barabara ya Mandela inayobomoka kwa mvua ya
siku tatu, itakuwa na hali gani miaka miwili mitatu ijayo?
Ni kweli maji yana nguvu kubwa, lakini wanaojenga
barabara hawalijui hili? Wanatengeneza mitaro ya kupitisha maji, wakijua
kwamba kuna siku maji yanaweza kuja kwa kasi kubwa, la kushangaza ni
kwamba mitaro hii ndiyo iliyobomoka! Inashangaza pia watu kujenga kwenye mkondo wa
maji. Watanzania wanaamini kwamba maji yanawakimbia watu! Sasa
wametambua kwamba maji hufuata mkondo wake.
Mtu anaweza kujiuliza je tatizo liko wapi, watu kujenga kwenye mkondo wa maji? Mbona Dar-es-Salaam bado ina maeneo makubwa?
Tukiachana na hili la maji ya mvua na mafuriko,
yako mambo mengine yanayoshangaza sana katika taifa letu na bora
kuyatafakari kwa pamoja na kutafuta tatizo lilipo ili tuweze kusonga
mbele kama taifa.
CHANZO: MWANANCHI
Hatujashuhudia polisi wakiendesha msako wa kuwashika “wakubwa”
na kuwapeleka mbele ya sheria; maana hawa ni wachochezi wakubwa wanataka
watu waichukie serikali yao na matokeo yake ni kuleta vurugu; watu hawa
wanahujumu uchumi wa nchi, mambo mengi yanakwama na uzalishaji
unazorota.
Mtu anaweza kujiuliza tatizo liko wapi? Kwanini
polisi wasiwakamate “wakubwa” hawa? Badala yake tunasikia waandishi na
wahariri wa vyombo vya habari wanakamatwa kwa uchochezi.
Badala ya kuwakamata watu wanaoficha mafuta,
wanaopandisha bei ya sukari, wanaoiba wanyamapori na kuwasafirisha nchi
za nje wanawakamata wanahabari, kwa kuandika makala ya uchochezi.
Makala kama hii ninayoiandika inaweza kuleta
uchochezi zaidi ya mtu anayeficha mafuta na kupandisha bei ya sukari?
Tatizo liko wapi hapa? Ni watanzania wangapi wataisoma makala hii
ninayoiandika sasa hivi? Nikikamatwa na kuwekwa ndani kwa uchochezi, ni
imani yangu kwamba idadi kubwa ya watu wataisoma makala hii. Tanzania ina mambo mengi ya kushangaza. Siku
chache kabla ya kamata kamata ya waandishi na wahariri Jukwaa la
wahariri Tanzania lilikutana kujadili amani.
Mkutano uliwashangaza wengi, maana ulionekana
kutokuwa na agenda. Waandishi wa habari wanaweza kudumisha amani kwa
kuandika ukweli bila kuongeza chumvi au kuegemea upande mmoja.
Nimetaja machache tu yanayoshangaza kwenye taifa
letu, lakini yako mengi mfano chama tawala CCM kutembea kifua mbele na
kujigamba kwamba kina ridhaa ya kutawala kutoka kwa watanzania.
Tupo Watanzania milioni 40, waliojiandikisha
kupiga kura ni milioni 20, waliopiga kura ni milioni 8, na CCM ikawapata
kama milioni tano hivi – ni asilimia ngapi ya watanzania? Mtu unaweza
kujigamba kwamba chama kinapendwa? Nimalizie makala hii kwa kutaja pia jambo hili
linaloshangaza zaidi la huu ugonjwa wa kutotaka kukosolewa. Huu ni
ugonjwa wetu sote watanzania. Ukimkosoa mtu, wewe ni adui! Hatupendi
kuambiwa ukweli! Wenye imani zao wanasema Ukweli, utatufanya Uhuru! Basi
wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka, tukae pamoja kama taifa na
kutafakari na kujifunza kukubali ukweli. Nawatakia wasomaji wangu
Christmas njema na mwaka mpya wenye baraka na mafanikio.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment