Pages

Wednesday, December 17, 2014

MWAMBULUKUTU: CCM ITAKAA MADARAKANI MIAKA MINGINE 50 IJAYO


Mzee Mwambulukutu amekuwa mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mbeya kwa vipindi tofauti na enzi za utawala wake alijijengea umaarufu mkubwa kutokana na kudhibiti wapinzani
Je, Chama cha Mapinduzi, CCM, kilipoamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi kilikuwa na wazo kwamba Chama kingine kinaweza kukiangusha? Je sasa kinaweza kukubali kushindwa kwenye chaguzi zinazoendelea nchini?
Haya ni miongoni mwa maswali yasiyo na majibu sahihi. Kiini cha maswali haya ni jinsi ambavyo chama hicho tawala na serikali yake vinavyoudhibiti upinzani katika harakati zake za kutaka kukiondoa madarakani.
Ni takribani miaka 20 sasa tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Lakini kwa kipindi chote hicho wapinzani wamekuwa na uwanja hafifu wa ushindani dhidi ya CCM.
Serikali kupitia vyombo vya dola imekuwa ikiweka mazingira magumu ya ushindi kwa kambi ya upinzani kuanzia ndani ya Tume ya Uchaguzi ambayo imekuwa chini ya viongozi ambao sio tu wanateuliwa na Mwenyekiti wa CCM, lakini wenyewe huwa makada wa chama hicho kinachotawala.
Majibu ya maswali haya yanaainishwa na muasisi na kiongozi mkongwe wa Chama hicho tawala mzee Isakwisa Mwambulukutu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Mwambulukutu aliyejizolea umaarufu mkubwa enzi za uongozi wake anaeleza msimamo wake kupitia mahojiano maalumu yaliyofanywa na Mwandishi wa gazeti la Mwananchi wa mkoa wa Mbeya, Lauden Mwambona.
Swali: Je CCM ilipoamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi , ilifikiria na kujiweka tayari kuondoka madarakani kama itatokea kikashindwa kwenye uchaguzi?
Jibu: Ndiyo ilijua inaweza kuondoka madarakani, lakini sasa nadhani haitakubali kuwaachia madaraka wapinzani wenye matusi.  Mimi naamini kama vyama vya upinzani vitaendelea na mwelekeo wa sasa wa matusi na kutishia kumwaga damu, CCM itakuwapo madarakani miaka mingine 50 ijayo.
Kinachoonekana sasa kwa viongozi wa vyama vya upinzani ni kwamba wanatafuta kula, siyo uongozi wa nchi. Wanapenda matusi na kutamka kauli za kumwaga damu jambo ambao sio tu CCM pekee inayolipinga, bali hakuna mtanzania atakayekubali nchi itumbukie huko.
Lakini vyama vya upinzani vikijirekebisha na kuingia kwenye uchaguzi kwa ustaarabu na kuacha kauli mbaya, CCM itakuwa tayari kuondoka madarakani.

Swali: Awamu ya nne ya utawala wa CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete itamalizika mwakani, je mambo gani wewe unaweza kusema unaona Rais Kikwete kayafanya vyema na ni wapi amekosea.
Jibu: Kwa kweli namshukuru Mungu kwamba nimeshuhudia kazi zilizofanywa na viongozi wakuu nchini kuanzia awamu ya kwanza hadi ya nne. Kila awamu zipo kazi kubwa zilizofanyika.
Hali kadhalika Rais Kikwete amefanya kazi nyingi za kuonekana . Kwa mfano  kajenga heshima kwa Tanzania kutambuliwa na mataifa mbalimbali duniani.
Rais Kikwete ameweza kuwakaribisha marais wa Mataifa makubwa duniani  kama Barack Obama wa Marekani, Rais  Xi Jiping wa China wamefika hapa katika taifa ambalo ni maskini. Mpaka sasa marais wastaafu wengi wa nchi hizo wanafika. Lakini pia Rais Kikwete amefanya makubwa katika kujenga barabara za lami. Nchi sasa imeunganishwa kwa lami maeneo mengi.  Hali kadhalika Watanzania wengi wameshuhudia umeme ukisambaa vijijini. Na hata maji yamesambazwa sana vijijini.
Rais Kikwete pia atakumbukwa sana kwa kujenga shule za sekondari na vyuo vikuu vingi kuliko wengine wote. Wapo wanaokosoa shule za kata, lakini fikiria zisingekuwapo shule hizo, watoto hao wangekuwa wapi? Kikwete sasa anaendelea na mradi wa gesi ya Mtwara na Lindi  ambayo bila shaka itaongeza kasi ya maendeleo nchini . Lakini siasa za uongo zilisema gesi inapelekwa  Bagamoyo, jambo ambalo ni propaganda za wapinga maendeleo. Kwa upande wa kasoro, mimi naamini kila binadamu anao udhaifu ambacho Mungu alimpatia. Kwa mfano naona Rais Kikwete ni mpole sana, hana ukali,  lakini wengine wamegeuza upole wa rais wakisema ni udhaifu, sawa, pengine huu ndio udhaifu wake.

Swali: Tunaelekea kwenye uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani. Wapo wana CCM waliotangaza nia zao za kugombea Urais. Nini maoni yako kuhusu wanaCCM waliotangaza nia.
Jibu:  Kwa bahati nzuri mimi ni mwanaCCM na nitakufa nikiwa CCM. Mimi naamini mgombea wa CCM bado. Hao waliojitangaza hawanisumbui kabisaa.  Sina mgombea, bali nasubiri atakayeteuliwa na CCM tu.
Lakini kikubwa kwa CCM lazima ateuwe mgombea safi, mwadilifu, mpenda watu, asiyeguswa na kashfa za aina yoyote ile . Mteule wa CCM lazima awe yule anayependwa na  Watanzania wote wakiwamo wa Upinzani na ambaye  anaogopwa na kambi ya upinzani.
Katika uongozi wa nchi  hawatakiwi watu wapenda rushwa wenye makundi bali sasa anatakiwa kiongozi mwenye hekima, mwadilifu wa hali ya juu mzoefu katika siasa za ndani na za kimataifa.
Kwa kweli naamini  mgombea wa CCM mwaka kesho atakuwa msafi anayependwa na Watanzania wote.

Swali: Kwa nini wazee waasisi wa siasa mkoani Mbeya hamjitokezi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala ya nchi?
Jibu: Hapana hatujakaa kimya. Tuliwahi kuwaomba waandishi  kupitia umoja wenu, na tulikaa nao Mbeya Peak Hotel  ambapo tulizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, lakini habari zetu hazikutoka .
Baadaye niliambiwa kwamba habari hazikutoka kwa sababu waandishi wa siku hizi wanataka fedha kwanza.  Nakumbuka ni gazeti moja tu ndilo lililoandika ingawa waliofika walikuwa vijana wengi wakiwamo wajukuu wangu.

Swali: Kwani  siku hiyo mlizungumzia kitu gani?
Jibu:  Kipindi hicho, Wazee wa Mbeya tulikuwa na mambo mawili  ambayo pamoja na kuwalaumu   Wabunge waliokuwa wakiwakashfu waasisi wa Taifa hili, hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Abeid Aman Karume. Pia tulitaka tumshauri Jaji msomi Joseph Warioba  aache kulijibu Bunge lilipokuwa likijadili rasimu ya Katiba Mpya.
Jaji Warioba na wajumbe wa Tume walifanya kazi nzuri na kuikabidhi kwa Rais Jakaya Kikwete, hivyo sisi wazee tulitaka tumshauri Jaji kwamba atulie wala asiingilie   mjadala  wa wabunge.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment