Chimani ambaye alipata kura nyingi katika uchaguzi huo, aliwaaga wenzake waliokuwa wakisubiri kushangilia ushindi huo akiwamo dada yake kuwa anakwenda kujisaidia, lakini hakuweza hakurejea mpaka mwili wake ulipogundulika jana asubuhi.
Mwili wake ulikutwa ukielea katika shimo la choo kilichokuwa hakijafunikwa ndani ya uzio wa jengo lililokuwa linatumika kwa ajili ya kupigia na kuhesabia kura lenye urefu wa zaidi ya futi 30.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kuwapo tukio hilo na kueleza marehemu alianguka katika shimo hilo usiku na mwili wake kuopolewa na kikosi cha Zimamoto kisha kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Geita kwa uchunguzi zaidi.
Habari kutoka eneo la tukio zinadai, marehemu alikuwa amejizolea kura 248 kati ya 676 zilizopigwa na kuibuka kidedea katika nafasi ya ujumbe wa serikali ya mitaa kupitia Chadema.
Tukio hili limekuja huku Chadema ikiibuka na ushindi mnono kwa zaidi ya asilimia 50 kwa nafasi ya wenyeviti wa mitaa na vitongoji katika maeneo ya makao makuu ya wilaya Chato, Geita na mamlaka ya mji mdogo wa Katoro.
Wakati huo huo, Simeo Isaka (42), mkazi wa kijiji cha Ngokolo kata ya Bukomela tarafa ya Mweli wilayani Kahama, ameuawa kwa kukatwa na jembe kichwani wakati akishangilia matokeo ya ushindi wa Chadema.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana wakati Isaka akishangilia matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kamugisha alisema marehemu huyo alikuwa akishangilia ushindi wa Chadema ngazi ya mwenyekiti wa kijiji cha Ngokolo na ghafla alivamiwa na watu watatu wasiojulikana na ‘kuchepwa’ jembe kichwani.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment